WAKAZI wa kijiji cha Lipokela wilayani Songea mkoani Ruvuma wanamuomba waziri wa ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi Profesa Anna Tibaijuka kuwasaidia kuirejea ardhi yao yenye ukubwa wa zaidi ya hekari 5000 iliyochukuliwa kinyemela na mwekezaji.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika kijiji hicho baadhi ya wananchi walidai kuwa mwekezaji mwenye asili ya Asia anayefahamika kwa jina moja la Merali tangu mwaka 1985 alipewa ardhi kinyemela bila Baraka za wananchi na kusababisha ardhi hiyo kuingia kwenye mgogoro mkubwa.
Wananchi wamedai kuwa mwekezaji huyo alipewa ardhi hiyo katika mazingira ya kifisadi kupitia aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji hicho Joseph Komba pamoja na aliyekuwa katibu wake Gervas Mbonde .
Hata hivyo walisema mwekezaji huyo alipewa ardhi kwa maamuzi ya wananchi yenye ukubwa wa hekari 1000 mwaka 1984 na kwamba mwaka 1985 aliomba tena ardhi hekari zaidi ya 5000 ambazo alipewa bila Baraka za wananchi na kuleta mgogoro ambao unaendelea hadi sasa.
“Kuanzia mwaka 1985 wananchi wa kijiji cha Lipokela hawakujua kama ardhi yao ya hekari 5000 amepewa mwekezaji hadi mwaka jana takriban miaka 25 ndipo ilipofahamika na kusababisha wananchi zaidi ya 250 wanaolima mashamba pamoja na makazi kwenye eneo hilo kuambiwa kuwa eneo hilo ni mali ya mwekezaji wa kiasia”, walidai wananchi hao.
Akizungumza kwa niaba ya wenzao mwenyekiti mstaafu wa kijiji hicho Faustine Komba alibainisha kuwa ardhi hiyo yenye mgogoro ilianza kutumika na wananchi kuanzia mwaka 1993 ambao walipimiwa kihalali na uongozi wa kijiji na kuendelea kuitumia mwaka hadi mwaka bila kutambua kuwa amepewa mwekezaji kinyemela.
Komba alisema mwekezaji alipewa kisheria hekari 1000 tu upande wa kulia mwa barabara ya Songea – Mbinga na kwamba eneo lenye hekari zaidi ya 5000 upande wa kushoto ambazo mwekezaji huyo anadai kupewa kinyemera sio zake kwa kuwa ni mali ya wananchi ambazo walipewa kihalali na serikali ya kijiji.
Uchunguzi ambao umefanywa na wanakijiji wanadai wamebaini kuwa mwekezaji huyo kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa kijiji hivi sasa amekuwa dalali wa kuwauzia ardhi wawekezaji wengine kutoka nchini Afrika ya kusini na Marekani hivyo wameiomba serikali na hasa waziri wa ardhi kuingilia kati mgogoro huyo.
Wananchi hao wakiwemo Gofrey Lupindu,Agustino Komba,Filbert Kinunda, Vestina Hyera, Bomba Nchimbi wakizungumza kwa uchungu mkubwa ,walidai kuwa hivi sasa pia hawana imani na mwenyekiti wa kijiji aliyopo madarakani John Nchimbi ambaye anadaiwa kumsaidia mwekezaji badala ya kuwasaidia wananchi waliomweka madarakani.
Uchunguzi umebaini kuwa iwapo serikali haitachukua hatua za makusudi katika kutatua mgogoro huo wa ardhi kuna hatari ya kutokea machafuko makubwa kutokana na ukweli kuwa wananchi wa kijiji hicho wamedai hawapo tayari kuona mwekezaji anapora ardhi yao kinyemela na kusababisha wananchi kuwa wakimbizi katika ardhi yao.
Uchunguzi mwingine ambao umefanywa katika kijiji hicho umebaini kuwa mwekezaji huyo ambaye alipewa hekari 1000 na wananchi katika kipindi cha miaka mitatu alifanikiwa kulima hekari 15 tu na kitendo cha kutaka kuchukua hekari nyingine zaidi ya 4000 kinawapa mashaka kuwa kijiji hicho kipo katika hatari ya kuuzwa kwa kisingizio cha uwekezaji.
Afisa wa ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Japhet Mungashwa amekiri kwamba mwekezaji huyo amemilikishwa eneo la hekari 5000 kihalali kwa kipindi cha miaka 99 kwa sheria ya ardhi ya mwaka 1923 ambayo inawaruhusu wajumbe wa kijiji kupitisha maamuzi bila kushirikisha maamuzi ya wananchi wote kama ilivyo katika sheria mpya ya ardhi ya mwaka 1999.
Wananchi hao wametoa mwito kwa serikali ya wilaya ya Songea, mkoa wa Ruvuma pamoja na waziri wa ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi kufika katika kijiji hicho ili kujionea hali halisi ya ardhi ya mashamba na makazi ambayo wameporwa na mwekezaji.
Sheria ya ardhi ya vijiji namba tano kifungu cha tano ya mwaka 1999 inasema kuwa Halmashauri ya kijiji haitagawa ardhi au kutoa hakimiliki ya kimila bila ya kwanza kupata idhini ya mkutano wa kijiji ambapo katika kifungu cha sita katika sheria hiyo kinaeleza Halmashauri ya kijiji italazimika kutoa taarifa na kuzingatia maoni ya mkutano wa kijiji kuhusu uendeshaji na usimamizi wa ardhi ya kijiji.
Inabidi shauri hili lichunguzwe kwa kina kwa faida ya wa Tanzania wote.
inabidi serekali iwe makini kwenye mambo kama haya kwani aridhi ni mali ya watanzania na siyo ya watu wachache.