UTAFITI: Wananchi 70% wanaamini Vyombo vya Habari havitumii vibaya Uhuru wake

Jamii Africa

WANANCHI saba kati ya 10 (70%) wanaamini na kupenda kuona Vyombo vya Habari nchini Tanzania, vinatangaza maovu ya watendaji wa serikali na wanayaamini yanayoandikwa na kuongelewa na vyombo hivyo.

Hata hivyo, watu watatu kati ya 10 wanahofia utoaji wa taarifa hizo unaweza kuathiri nchi.

Wakati Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ikiwa imepitishwa, takwimu za Sauti za Wananchi na Afrobarometer zinaonesha kuwa wananchi wanaunga mkono wajibu wa vyombo vya habari katika kuiwajibisha serikali

Kwa mujibu wa utafiti wa Afrobarometer, asilimia 65 ya wananchi wangependa vyombo vya habari vitoe taarifa za maovu yanayofanywa na serikali, ikiwemo vitendo vya rushwa. Hata hivyo, asilimia 31 wanasema utoaji wa taarifa hizo utaiathiri nchi.

vyombo_habari_vitoe

Ni wananchi 8 kati ya 10 (asilimia75) wanaosema kuwa vyombo vya habari vinafanya kazi nzuri ya kufichua maovu na rushwa, huku wananchi 2 kati ya 10 (18) wakisema havifanyi kazi nzuri.

Kwa upande wa uhuru wa kutangaza habari, asilimia 53 wanasema vyombo vya habari viwe huru kutangaza habari yoyote, huku asilimia 44 wakisema serikali iwe na mamlaka ya kufungia magazeti.

Vilevile, asilimia 65 wanasema vyombo vya habari havijawahi au kama vimeshawahi, ni mara chache sana vimekuwa vikitumia vibaya uhuru wake kwa kutangaza vitu ambavyo si vya kweli.

Wananchi wanaunga mkono kwa kiasi kikubwa uhuru wa maoni na kupata taarifa?

Karibu wananchi wote (asilimia 95) wanasema wananchi wawe huru kuikosoa serikali pale ambapo wanaona imekosea.

serikali ikosolewe ikikosea

Wananchi pia wanaunga mkono demokrasia. Takwimu za Sauti za Wananchi za hivi karibuni zinaonesha asilimia 69 ya wananchi walichagua demokrasia kuliko aina nyingine ya serikali.

Uungaji mkono huu wa demokrasia pia unadhihirika kupitia takwimu za Afrobarometer (2014) zinazoonesha asilimia 79 ya wananchi wakisema kuwa serikari inayoongoza kidemokrasia ndiyo aina ya serikali wanayoipenda zaidi na asilimia 81 wakisema ni vyema wachague viongozi wao kupitia uchaguzi huru wa kidemokrasia.

Je, kupatikana taarifa ni muhimu kwa wananchi?

Asilimia 77 wanasema wananchi wa kawaida wawe na uwezo wa kupata taarifa zinazoshikiliwa na mamlaka za umma, huku asilimia 23 wakisema ni wale tu wanaofanya kazi kwenye mamlaka za umma ndiyo waruhusiwe kupata taarifa hizo.

Asilimia 80 wanasema upatikanaji wa taarifa hizo kwa wananchi utasaidia kupunguza vitendo vya rushwa, huku asilimia 20 wakisema watumishi wa umma watatafuta njia nyingine za kuficha maovu yao.

Vipi kuhusu suala la kuunga mkono haki yao ya kupata taarifa za serikali?

Karibu wananchi wote (asilimia 92) wanasema ni muhimu kwa vipindi vya bunge kurushwa moja kwa moja kupitia luninga na redio.

Asilimia 79 wanapinga uamuzi wa serikali kusitisha matangazo hayo na asilimia 88, wanasema bunge lirushwe moja kwa moja bila kujali gharama.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *