Baada ya Kilio cha Muda mrefu: Kero ya maji Kimara kufikia ukingoni

Jamii Africa

WAKAZI wa Kimara, Dar es Salaam, hasa eneo la Kitunda, wamekuwa na kilio cha muda mrefu kutokana na kukumbwa na adha ya ukosefu wa maji ya kutosha katika baadhi ya maeneo kwa takribani miaka sita sasa.

Licha ya kuwepo kwa mikakati za viongozi na huduma mbalimbali za serikali kutekeleza sera yake ya maji kumwezesha kila mwananchi anaondokana na uhaba wa maji nchini, lakini bado idadi kubwa hainufaiki na huduma hizo katika maeneo mbalimbali ya Kimara.

Katika Jiji la Dar es Salaam, eneo kubwa linalopata maji linahudumiwa na Kampuni ya Dawasco, ambayo iko chini ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam, Dawasa.

FikraPevu imefika katika Kata ya Saranga, Mtaa wa Kimara Matangini, eneo la Kwa-Salema na kushuhudia mabomba yaliyowekwa kwenye baadhi ya nyumba yakiwa kama mapambo kwa kukosa maji kwa kipindi kirefu.

Beatrice James (65), ameiambia FikraPevu juu ya kilio cha maji mtaani humo na kwamba kukosekana kwa muda mrefu kumewafanya wakazi “kuzoea tu.”

“Kweli tumekata tamaa, tumepeleka malalamiko yetu kwa viongozi wa serikali za mitaa, hasa wajumbe wetu ambao ndio wanaoonekana kuwa karibu na kuyasikiliza matatizo yetu, lakini hali bado ni ileile kwani ikitokea tatizo kupatiwa ufumbuzi huwa ni kwa muda mfupi na baadaye hali hujirudia” anasema Beatrice

Aidha, anasema kukosekana kwa maji kumefanya maeneo mengi kuwa machafu na kutishia kuwepo kwa magonjwa ya milipuko, hasa kipindupindu.

Beatrice anasema pia ukosefu wa maji huhatarisha usalama wa wanawake, hasa wanapoadamka kwenda kusaka maji kwa ajili ya matumizi ya familia.

Wanawake wengi hulazimika kuamkausiku wa manane au alfajiri kutafuta maji kwa ajirani au kuyafuata visimani.

Idadi kubwa ya wakazi wa eneo hilo, hupata maji mara moja tu kwa wiki, siku ya Alhamisi na hutoka kwa saa chache, mara nyingi zisizozidi nane na pengine hayatoki hadi Dawasco wasemwe sana au watu kuandamana.

Vilevile, mkazi mwingine anatoa masikitiko yake kuhusu bei ya maji isiyoendana na hali halisi ya kipato cha wakazi wa maeneo hayo, ambao wengi wana kipato cha chini. Katika maeneo haya dumu la lita 20 huuzwa kwa Sh. 500 hadi 1,000, huku mnunuzi akitakiwa kuongeza Sh. 200 kwa kila dumu kama ghalama ya ubebaji.

Hali hii inamsukuma kuiomba serikali kulifumbulia macho suala hili kwa kuwezesha miundombinu haraka ya kuweza kuwafikishia maji ya uhakika inatekelezwa.

FikraPevu ilipozungumza na mjumbe wa shina namba 16 Kimara Matangini eneo la kwa Salema, Anyingisye Mwasaga, anaulalamikia uongozi wa Dawasco, hasa mkoa wa maji Kimara kwa kushindwa kutekeleza majukumu ya kazi zake wakati wanapopelekewa matatizo kutoka kwa wananchi.

“Ndani ya mwaka huu, nimeandika barua mbili, nikiwataka Dawasco kuwapatia maji wananchi, ambao tayari wamefungiwa mita kwa muda mrefu bila huduma,

lakini hadi sasa wako kimya ” mjumbe huyo ameijulisha FikraPevu

Anabainisha pia kupokea malalamiko ya wakazi anaowaongoza katika eneo lake kwa kuletewa bili za maji zinazoonekana kuwa juu kuliko maji yanayotumika au bila kutumika kabisa.

Kwa upande mwingine, anatoa kilio chake kwa uongozi wa Dawasco kwa kuwahamisha wafanyakazi wake mara kwa mara, hali inayosababisha ufuatiliaji wa malalamiko ya wananchi kuanza upya kutokana na ugeni wa watumishi na mfumo mbovu wa kuweka kumbukumbu.

Vilevile, Mwasaga anaoanisha tatizo la kutokuwa na diwani wa kata na adha ya maji, kwamba ni kigezo kimojawapo cha kutosikilizwa vyema pindi akiwasilisha malalamiko Dawasco, kwani barua zake huonekana kutokuwa na nguvu na hivyo kutekelezwa.

Pia wakazi wa Kimara wanatoa mwito kwa mbunge wao wa Jimbo la Kibamba, John Mnyika kulifatitilia kwa karibu suala hili na kumtaka kusikiliza kilio chao kwani tangu aingie madarakani, hajawahi kuwatembelea kusikiliza kero zao.

FikraPevu haikuishia hapo, imefika ofisi za Dawasco – Mkoa wa Maji wa Kimara na kukutana na meneja wake, Emmanuel Zabron ambaye anakubali kuwepo kwa upungufu wa maji unaosababisha kero katika kata hiyo, lakini analitaja kuwa tatizo la mtu mmojammoja na sio kwa wakazi wote wa Kimara Matangini.

Pia analaumu uwasilishwaji wa malalamiko kutoka kwa wananchi yanayoletwa kupitia viongozi wao na badala yake anahimiza kila mwananchi anapaswa kufika ofisini na malalamiko binafsi kwani kila nyumba inakuwa na matatizo tofauti na nyingine.

“Inatuwia ngumu kushughulikia malalamiko ya watu kwa ujumla kupitia viongozi wao kwa njia ya kutuandikia barua, kwani mara nyingi mahitaji yanakuwa tofauti, ni vyema mtu akafika ofisini kueleza shida yake binafsi, hii itakuwa rahisi pia kumfikia kwa haraka”

Aidha, Emmanuel anakanusha kwamba ofisi yake imekuwa haifuatilii kero za maji na anaitupia lawama jiografia ya eneo hilo  kutokuwa rafiki kwa watendaji wake, kuwa sehemu ya Kimara  ni mabonde, miinuko na vilima.

Hali hii anaitaja kuwa chanzo kikubwa cha uhaba wa maji, kwani wakazi wanaoishi sehemu za vilimani ni vigumu kutokana na uchache wa maji uliopo mitamboni, ikilinganishwa na idadi ya watumiaji kuwa wengi.

Akiongelea suala la wateja wanaodai kulipishwa kiasi kikubwa cha Ankara (bili), anasema kwa sasa wamefungiwa mita mpya ambazo zinasoma maji kwa usahihi.

Emmanuel anaifahamisha FikraPevu juu ya kukoma kwa kero ya maji Kimara kabla ya Desemba 25, mwaka huu kutokana na kupanuliwa kwa chanzo cha Ruvu Juu na ujenzi wa bomba kuu hadi matanki ya Kibamba na Kimara.

“Hivi sasa miundombinu imekamilika, mabwawa tayari yamejengwa na yatapata maji kutoka bomba jipya la Ruvu juu. Kazi imebaki kwa mkandarasi, ambaye anaunganisha umeme wa kutosha kusukuma maji.”

Endapo kauli ya Emmanuel itakuwa sahihi, ni wazi kuwa wakazi wa Kimara watanufaika na kudhihirisha kuwa dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 inatekelezwa kwa vitendo kuhusu huduma ya maji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *