“JAPOKUWA mtaji umekuwa changamoto, lakini nitaendelea na mradi huu wa Green House, maana una manufaa makubwa,” ndivyo anavyoanza kuelezea Dk. Sophia Mlote, mkazi wa Kinyerezi Zimbili jijini Dar es Salaam.
Dk. Mlote ni miongoni mwa wanawake wachache ambao licha ya kuwa na ajira wameamua kuanzisha ujasiriamali kwa lengo la kuongeza kipato.
“Mtaji ni shida, lakini nimeamua kuanzisha mradi huu kama maandalizi yangu ili nitakapostaafu nisibweteke, bali niwe na shughuli ya kufanya,” aliiambia FikraPevu.
Yeye na akinamama wenzake wa kikundi cha Kijani Kibichi wameamua kujikita katika kilimo cha bustani kwa kutumia Green House ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa kiasi kikubwa yamesababisha ukame.
Anasema, kwa kuwa anakaribia kustaafu, na kwa elimu ya kilimo na uchumi aliyonayo pamoja na utaalamu alioupata, ameona ni vyema aanzishe mradi ambao siyo tu utampatia kipato, lakini pia utasaidia kutunza mazingira pamoja na kuwa msaada kwa jamii kutokana na mazao yatakayovunwa.
“Niliamua kuwaelimisha wanawake wenzangu katika mtaa huu na kuwashawishi waunde kikundi hiki na tayari wamekwishapata mafunzo ya kutosha ambapo kila mmoja amekuja na wazo la kuanzisha bustani ndogo nyumbani kwake ya mtindo huu kwa mazao ambayo anaona yanafaa,” anaongeza Dk. Mlote, ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa Wizara ya Kilimo, Chakula, Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi.
Kilimo hiki kinaendana na Malendo Endelevu ya Dunia (SDG) katika kukabiliana na mabadiliko hayo ya tabianchi, uharibifu wa mazingira, kupambana na umaskini, kuhakikisha usalama wa chakula, kuongeza ajira na kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Dk. Mlote anaonekana akiendelea kushughulikia nyanya zake ndani ya banda kubwa lililoezekwa na kuzungushiwa platiki maalum huku akiwa ameongozana na mtaalamu wa kilimo, Abdon Hamaro.
Pembeni ya banda hili lenye ukubwa unaokadiriwa kuwa wa meta 8 kwa 12, akina mama kadhaa wamezunguka wakitazama ustawi wa zao hilo huku Bw. Hamaro akiendelea kutoa maelekezo ya namna ya kuendesha kilimo cha ndani ama kilimo hai (Green House) ikiwa ni sehemu ya mafunzo ya vitendo ya akinamama hao katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuongeza kipato kama njia ya ujasiriamali.
Tofauti na nyanya ambazo watu wamezowea kuziona zikilimwa katika mashamba makubwa na bustani za wazi, nyanya hizi zinalimwa ndani ya banda ambalo ukubwa wake utategemea pia na eneo lililopo pamoja na uwezo wa mhusika katika kulijenga banda hilo.
“Mtu yeyote anaweza kuendesha kilimo cha mazao mbalimbali kwa kutumia Green House hata katikati ya Jiji la Dar es Salaam kama tunavyoona, ni rahisi na rafiki wa mazingira kwa sababu unaweza kuendesha hata kwenye ua wa nyumba yako kama hivi,” Bw. Hamaro anaendelea kuwaeleza akinamama hao, ambao ni wanakikundi cha ‘Kijani Kibichi Kinyerezi’ walioamua kupambana na uharibifu mazingira.
Mbali ya kutunza mazingira, Bw. Hamaro kutoka Chama cha Wakulima wa Bustani Tanzania (TAHA) anasema, kilimo hai kinasaidia kuzalisha vyakula visivyo na kemikali ambavyo ni rafiki kwa afya ya binadamu.
Katikati ya Jiji la Dar es Salaam watu wamekuwa wakishuhudia kilimo cha mboga mboga kwenye mabonde ya mito midogo, ambacho kinatumia umwagiliaji wa maji machafu na yenye kemikali za kutoka viwandani, ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu.
“Mbegu zinazotumika zimetengenezwa maalum na hazifanani za zile GMO zinazopigiwa kelele, lakini pia unatakiwa kutumia mbolea za asili kama mboji na samadi, kwa sababu ukitumia kemikali nyingi kwenye udongo, mimea inanyonya na kemikali hizo zinabaki kwenye vyakula na hatimaye kuingia miilini mwetu,” anafafanua Hamaru.
Vile vile, Hamaro anasema kilimo cha Green House kinaweza kutumika hata kwa matunda na kwamba kinatumia maji kidogo huku kikimpunguzia gharama mkulima hasa kwa kuepukana na magonjwa mbalimbali ambayo yanasababishwa na wadudu.
“Kwa kuwa banda limefunikwa na kukingwa, hakuna wadudu waenezao magonjwa ya mimea wanaoweza kuingia, lakini faida nyingine ni kwamba, unaweza kudhibiti hali ya hewa kwa kupunguza ama kuongeza joto ili kuifanya mimea kukua vizuri,” anaongeza.
Dk. Mlote anasema ameamua kuanzisha kilimo hicho kwa kushirikiana na wanawake wenzake majirani wa mtaa huo baada ya kupata mafunzo na ufadhili kupitia mradi wa Green Voices.
Yeyé ni miongoni mwa wanawake 15 waliopatiwa mafunzo ya kuongeza ujuzi wa jinsi ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yaliendeshwa nchini Hispania chini ya ufadhili wa taasisi inayojihusisha na maendeleo ya wanawake wa Afrika, ijulikanayo kama Foundation for Women of Africa ambayo inaongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, María Teresa Fernández de la Vega.
“Mimi niliamua kuchagua mradi huu kwa sababu, kwanza ni rahisi kuuendesha kwa kuwa shughuli zote zipo hapa nyumbani na hata kama nitarudi usiku kutoka kazini, bado ninaweza kuingia humu shambani na kuhudumia mimea kwa kuwa banda hili lina taa,” anaeleza.
Kikundi cha ‘Kijani Kibichi Kinyerezi’ kinaundwa na wanawake 10, ambao hivi sasa baadhi yao wanaendesha kilimo cha nyanya, kabichi, hoho, matango na matikiti maji.
Christina Lwiza, mmoja wa wanakikundi ambaye anajishughulisha na biashara ya uuzaji vinywaji kwenye grocery yake mwenyewe, anasema ameshawishika kuanzisha kilimo cha nyanya nyumbani kwake ambacho kinaweza kumpatia mapato ya nyongeza pamoja na kukidhi mahitaji ya nyumbani.
“Sijawahi kulima nyanya, lakini kwa mafunzo niliyoyapata, hakika naweza kuendesha kilimo hicho bila shida,” anasema Christina.
Karibu wanakikundi wote wamehamasika, ambapo kila mmoja ameamua kubuni zao ambalo linaweza kumfaa.
Malengo ya dunia
Kilimo hai kinaendana na masuala mtambuka ya mazingira pamoja na kukabiliana na uhaba wa chakula na kupunguza umaskini kama inavyoelezwa kwenye Malengo Endelevu ya Dunia yaliyopitishwa mwaka 2015.
Kwa mujibu wa malengo hayo, mataifa mbalimbali yamekubaliana kuhakikisha yanatokomeza umaskini kwa namna zote pamoja na kukomesha njaa na kupata uhakika wa usalama wa chakula na kuboresha lishe kwa kuhimiza kilimo endelevu.
“Kilimo hai ni endelevu kwa sababu unaweza kulima wakati wowote hivyo kinaweza kukabiliana na njaa na uhakika wa chakula ni mkubwa, lakini pia kitasaidia familia kuongeza kipato kwa kuuza ziada ya chakula kitakachozalishwa,” anasema Hamaro.
Lakini pia kwa kutumia kilimo hai, lengo namba sita la dunia linaweza kutimia, kwani ni kilimo ambacho kinatumia maji kidogo, hivyo kuhakikisha utunzaji mzuri wa vyanzo vya maji na matumizi sahihi ya maji yaliyopo.
Aidha, kilimo hai pia kinaweza kukidhi lengo namba 13 la dunia linalohimiza kupambana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake.
Sera ya Kilimo
Kilimo hai ni sehemu ya mapendekezo yanayotajwa kwenye Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013 ambayo inaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea mwaka 2025 kwa kuhimiza kilimo chenye tija pamoja na utumiaji mzuri wa rasilimali zilizopo, hususan ardhi na maji.
Kwa maana nyingine, kuhamasisha kilimo hai ni sehemu ya utekelezaji wa malengo, dhima na dira ya sera hiyo hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, ambayo serikali pia imeainisha mikakati yake katika Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2007.