MIGOGORO wa ardhi inazidi kuwa kero kubwa miongoni mwa wakazi wa Jiji la Mwanza ambapo wiki jana ( Mei 6) zaidi ya wananchi 100 kutoka mtaa wa Sumba ‘B’ katika wilaya ya Ilemela Jijini hapa waliamua kuandamana hadi ofisini kwa Mkuu wa Mkoa, Abbas Kandoro ili aweze kuwasaidia.
Aidha, baada ya kukoswa majibu waliyokuwa wakiyatarajia wananchi hao wameamua kuandika barua kwenda kwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi.
Viongozi wa kamati maalumu iliyoundwa na wananchi hao wameiambia FikraPevu kwamba mgogoro huo ulianza tangu mwaka 2008, baada ya maafisa wa ardhi katika sekretarieti ya mkoa wa Mwanza kuanza zoezi la upimaji na uthaminishaji pasipo kuwashirikisha wakazi wa mtaa huo .
” Ni kweli tuliandamana June 6 mwaka huu majira ya asubuhi; kutoka mtaa wa Sumba ‘B’ hadi katika eneo la ofisi za Mkuu wa Mkoa” alisema mwenyekiti wa kamati iliyoundwa, Ramadhani Mohamed wakati alipofika katika ofisi za geti hili mwanzoni mwa wiki hii.
Mohamed alisema huduma waliyopewa na Mkuu wa Mkoa haikuwaridhisha kwa vile waliambiwa amewasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela ili aweze kutoa majibu sahihi kuhusiana na mgogoro.
” Jambo jingine ambalo linatushangaza sisi ni kwamba awali tuliambiwa kuwa wanapima viwanja kwa ajili ya makazi ya pamoja na eneo la wazi kwa magari ya wafanyakazi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa, lakini tunashangaa upimaji wa viwanja umefanyika na tayari Wachina wameanza kufika na kuoneshwa viwanja” aliongeza Mwenyekiti wa kamati maalumu iliyoundwa na wakazi hao kwa ajili ya ufuatiliaji, Ramadhan Mohamed .
Alisema upimaji na uuzaji wa viwanja katika eneo hilo umeghubikwa na utapeli kwa vile hata stakabadhi zilizotolewa kwa ya kugarimia malipo ya fidia ya na kupimiwa viwanja hazina nembo ya serikali .
Alizitaja baadhi ya hatua zilizofikiwa na kamati yake katika kutatua mgogoro huo ni pamoja na kuitisha vikao kwa ajili kukutana na watuhumiwa na kwamba kila mara wahusika.
” Mheshimiwa Waziri, sisi wananchi hatutaki kumwaga damu tunakuomba uje mwenyewe ili uweze kuujua na kuutatua mgogoro huu; kwani mara kadhaa tumefuatilia hadi kwa Mkuu wa Mkoa bila mafanikio” inasema sehemu ya barua hiyo (nakala tunayo).
Wananchi hao wanamuomba Waziri kutoa majibu yake kabla wao hawajafikia hatua ya kujichukulia sheria mkononi.
” Ni matumaini yetu kuwa tutapata jawabu kutoka kwako kabla ya maamuzi ya wananchi, nyaraka zilizopo nyuma ya barua hii ni baadhi tu ya wananchi wanaopinga ifisadi huu” wanaendelea kudai wananchi hao kupitia barua hiyo ambayo pia nakala yake imetumwa kwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza.
Wananchi hao wanadai katika barua hiyo yenye kichwa cha habari ‘mgogoro wa ardhi’ kwamba wametapeliwa maafisa kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa vile hawakushirikishwa kabla ya zoezi la upimaji na uuzaji wa viwanja vyao kuanza.
Kwa mujibu wa barua hiyo ambayo imepewa kumbukumbu namba 2/yenye vikao 10/2008/2011, Afisa ardhi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye ametajwa kwa jina moja la Tegambwa na mwenzake aliyetajwa kwa jina moja la Beni pamoja na mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, Yusto Mleka, ndio chanzo cha mgogoro huo.
Barua hiyo iliyoandikwa Mei 6 mwaka huu inadai kuwa ardhi yao imeporwa na maafisa ardhi wa mkoa wa Mwanza pasipokuwepo na mihtasari yoyote inayoonesha ushirikishwaji na wananchi hao.
Alizitaja baadhi ya hatua zilizofikiwa na kamati yake katika kutatua mgogoro huo ni pamoja na kuitisha vikao kwa ajili kukutana na watuhumiwa na kwamba kila mara wahusika hukacha kwa kisingizio cha kuwa na kazi nyingi za kiofisi.
Mkuu wa Mkoa, Abbas Kandoro amekiri kwa njia ya simu juu ya kukutana na wananchi hao.
Alikiri pia kwamba suala hilo limedumu kwa muda mrefu sasa na kwamba amelikabidhi katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa kwaa ajili ya kushughulikiwa.
” Ni kweli mgogoro huo ninautambua, na nilikutana na wawakilishi wa wananchi hao siku ya Ijumaa iliyopita; kwa ufupi ni kwamba nimelikabidhi suala hilo katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili litafutiwe ufumbuzi” alikiri Kandoro.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Yusto Mleka alikiri kwa njia ya simu kuhusu kuutambua mgogoro huo ingawa alikanusha kuwa yeye hana uhusiano wowote na maafisa ardhi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Alifafanua kuwa mgogoro huo ulianza kabla yeye hajachaguliwa kuwa mwenyekiti wa mtaa huo.
Diwani wa kata hiyo, Margareth Chenyenge (CHADEMA) amekiri kuwepo kwa mgogoro huo na kuongeza kwamba umeanza kusababisha hofu na uvunjifu wa amani ndani ya mtaa huo.
Alisema tayari ameanza kufanya vikao na wakazi wa mtaa huo kwa ajili ya kupata ufumbuzi.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe aliliambia gazeti hili kwamba yeye hana taarifa kuwepo kwa mgogoro huu.
Habari hii imeletwa na mwandishi wetu Juma Ng’oko aliyeko mkoani Mwanza