Katavi: Maiti wataabika, majokofu mabovu

Jamii Africa

MAJOKOFU ya kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Mkoa wa Katavi ni mabovu. Hali hiyo inasababisha maiti wanaohifadhiwa katika chumba maalum kutunzia miili ya wafu, kuharibika mapema.

FikraPevu imeshuhudia hali hiyo na kuthibitishwa na mhudumu wa chumba cha maiti, George   Nsalamba, ambaye amekiri kuwa ubovu huo unafanya kazi yake kuwa ngumu.

“Nakueleza kwa kuwa nakuheshimu, kwamba hali ndani ya chumba nachofanya kazi ni ngumu, ikiwa maiti zitakaa ndani kwa zaidi ya siku moja, basi hali haikaliki,” anaeleza Nsalamba.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kuwa chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo kina uwezo wa kuhifadhi maiti 12 kwa wakati mmoja, kwa maana kwamba yamo majokofu yenye milango 12. Kimsingi, kila mlango una uwezo wa kuhifadhi miili 12. Imebainika milango tisa kati ya 12, imeharibika na haiwezi kutengeneza na kuhifadhi ubariki ambao ni muhimu kwa kutunza miili ya wafu.

Muhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, George Nsalamba (kushoto) akitoa maelezo juu ya ubovu wa majokofu hayokwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Raphael Muhuga, wakati wa ziara yake hospitalini hapo hivi karibuni

Nsalamba ameiambia FikraPevu kwamba sababu za kushindwa kufanya kazi kwa majokofu hayo ni kuharibika kwa mfumo wa umeme ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti, hivyo kuharibu majokofu hayo.

Swali kutoka FikraPevu: Kwanini umeme uharibu sehemu tu ya majokofu 12, wakati yanatumia mfumo mmoja?

Jibu la Nsalamba: Kimsingi ilipiga radi, sasa sijui hata mimi kwanini sehemu  tatu ziendelee kufanya kazi na zingine tisa zizimike kabisa, kwa kweli sijui maana sio fundi wa umeme.

FikraPevu ina taarifa kuwa hali ya ubovu huo wa majokofu ilianza tangu Januari, mwaka huu na hakuna jitihada za kurekebisha ili maiti wapewe heshima ya kuhifadhiwa kabla ya kwenda kuzikwa.

Meya wa Manispaa ya  Mpanda, Willy Mbogo ameiambia FikraPevu kwamba amepatahabari za kuharibika kwa majokofu hayo, ingawa hakuwa na “taarifa za ndani zaidi,” hivyo anafuatilia. Kwa mujibu wa taaluma ya tiba, maiti anatakiwa kuhifadhiwa kwenye majokofu kwa muda usiozidi siku saba, huku mwili huo ukiwa umewekwa dawa ili usiharibike.

“Mwili wa binadamu aliyekufa unaweza kuhifadhiwa siku moja tu kama haukuwekwa kwenye jokofu lenye ubaridi wa kutosha, lakini mwili huo ukiwekwa dawa na kuhifadhiwa ndani ya baridi kali, una uwezo wa kutoharibika hata kwa siku 40,” anaeleza Dk. Issa Omary, bingwa wa magonjwa wa binadamu.

Pamoja na kwamba haijafahamika mapema wagonjwa wanaohudumiwa na hospitali hiyo ya Mpanda kwa siku, lakini inaonekana kuzidiwa na wagonjwa wengi, hivyo kuhitaji upanuzi wa haraka.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wakati alipotembelea Katavi, aliuangiza mkoa huo kuharakisha upanuzi wake ili iwe na hadhi na uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi na kwa ufanisi. Hospitali hiyo ya manispaa ndio inatumika kuwa Hospitali ya  Rufaa ya Mkoa wa   Katavi kutokana kutokuwepo hospitali yake.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *