Magugumaji Ziwa Victoria yaelekea kuishinda serikali, wafadhili

Jamii Africa

ZAIDI  ya miaka 25, tangu kuanza kumea kwa magugumaji katika Ziwa Victoria, hasa upande wa Tanzania – eneo la Mwanza, bado serikali, kwa kushirikiana na wafadhili, inahangaika kuyaondoa.

Kuhangaika huko, kumeigharimu serikali pamoja na wadau wake wa maendeleo, muda na fedha nyingi, lakini bado magugumaji hayo yapo. Yamegoma “kufutika” juu ya uso wa maji hayo.

Mimea hii ilianza kukua na kuongezeka kwa kasi kati ya miaka 1992 na kudhihirka kuwa ni tatizo kubwa mwaka 1998, kwa kuchukua eneo la hekta 1440 mwaka huo.

Miongoni mwa madhara makubwa ya magugumaji ni pamoja na kuharibu mazalia na maisha ya samaki na viumbe wengine majini, kuzuia mfumo wa usafiri, kupunguza hewa ya oksijeni majini na kuharibu taratibu za uchumi zinazofanywa na binadamu.

Matukio ya magugumaji pia huziba mfumo wa kusambaza maji katika Jiji la Mwanza.

Magugumaji yanapokuwa mengi huwa ni kivutio cha magonjwa, hasa malaria kwani mbu wanaosababisha ugonjwa huo huishi kwenye mimea hiyo na kuzaliana, hivyo kuwa chanzo kikubwa cha kusambaa kwa ugonjwa huo.

Magugumaji huweza kuwa kichocheo cha ugonjwa mwingine, ikiwamo kichocho. Asilimia Zaidi ya 40 ya wakazi wa maeneo ya ziwa hilo hutumia maji yake moja kwa moja na kuyatumia bila kuchemsha.

Ni kutokana na sababu hizo na hatari, Tanzania kwa kutumia fedha zake na zile za washirika wa maendeleo (wafadhili) ilianza jitihada za kuokoa Ziwa Victoria.

FikraPevu ina taarifa kuwa zaidi ya dola za Marekani milioni 90 (zaidi ya shilingi bilioni 200.07), zimetumika hadi sasa, zikiwa fedha za washirika wa maendeleo katika kupambana na uharibifu wa mazingira katika ziwa hilo linalofaidisha wananchi wa nchi tatu za Afrika Mashariki; Kenya, Tanzania na Uganda.

Jumla ya dola za Marekani milioni 65 zilipangwa kutumika katika awamu hii ya Pili ya Mradi wa Hifadhi ya Mazingira ya Bonde la Ziwa Victoria, (LVEMP II), ikiwa ni kwa kipindi cha miaka minane.

Kati ya fedha hizo, dola milioni 32.50 zilitumika katika muhula wake wa kwanza wa kipindi cha miaka minne ya kwanza; kwa maana ya 2009 hadi 2013 na fedha iliyobakia imetumika katika muhula wa pili ambao ni kati ya mwaka 2014 hadi mwaka huu.

Ujerumani, Sweden na Norway ni miongoni mwa nchi zinazofadhili mradi huo, sambamba na Benki ya Dunia (WB) serikali inawajibika kuchangia dola za Marekani milioni moja kila mwaka katika bajeti yake ikiwa ni kwa ajili ya kugharamia malipo ya ndani yanayohusiana na mradi huo.

Mradi huu, kwa awamu hii ya pili, unamalizika baadaye mwaka huu, lakini bado magugumaji hayajatokomezwa.

Mikakati kadhaa imekuwa ikitumika kudhibiti magugumaji, ikimwao kutumia mbinu za kibaiolojia kwa kuweka wadudu maalumu waitwao mbawakavu, kuyaondoa kwa mashine na kwa mikono kutumia vikundi vya wananchi, hasa wanaoishi pembezoni mwa zikiwa hilo; likiwa na makazi ya viumbehai na samaki maarufu Sato, Sangara, Nembe, Mumi na wengine.

FikraPevu imeelezwa na wakazi wa maeneo ya Mwaloni, Mwanza na Kitaji, Musoma, mkoani Mara kwamba kazi ya kuondoa magugumaji ziwani humo ilikuwa ikifanywa na wananchi kupitia vikundi vyao kwa muda mrefu, kwa kujitolea kabla ya miradi ya serikali na wafadhili kuanza, lakini hakukuwa na mafanikio makubwa.

“Sisi tulikuwa tukijitolea kuyaondoa magugumaji, lakini yalitushinda, sasa baadaye ikaingia serikali nayo sijui kama watayamaliza, maana huongezeka mara kwa mara,” anaeleza Mashiku Jilala, mvuvi wa samaki eneo la Mwaloni, Mwanza.

Magugumaji ni aina ya mimea yenye asili kutoka Amerika Kusini inayomea kwenye maji ambayo ina hasara nyingi kuliko faida kati ya mimea yote ya majini.

Historia inaonesha kuwa iliingia Ziwa Victoria kupitia Mto Kagera kutokea Rwanda, kwa mujibu wa maelezo ya wataalamu wa LVEMP na kwamba imesambaa zaidi ndani ya ziwa hilo kutokana na kuwepo kwa shughuli za kibinadamu na upepo.

Mmea mmoja wa magugumaji unaposafirishwa unaweza kukusanya zaidi ya mbegu 300 ambazo zinachepuka kwa haraka na ndani ya muda mfupi, kitu kinachofanya majani yake kusambaa.

Katika ripoti ya utafiti uliofanywa na Thomas P Albertright na wenzake ya mwaka 2004 inaonesha kuwa Mto Kagera ambao ndio mkubwa kuliko mito yote inayopeleka maji ziwani humo, unaingiza kiwango cha magugumaji kinachochukua eneo la hekta 0.2 mpaka 1.5 kwa siku na kufanya magugumaji kuwa na uwezo wa kuchukua eneo la hekta 300 kwa mwaka kwenye ziwa hilo.

Wakati mradi mkubwa wa LVEMP II unafikia ukingoni, ni muda muafaka sasa kwa Tanzania na nchi zingine zinazotumia na kufaidi uwepo wa Ziwa Victoria, kujipanga na kuendeleza vita dhidi ya magugumaji, ili kulinda mazingira na viumbehai waliomo kwa manufaa ya wananchi na uchumi.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *