Ekari 550 zilivyozolewa na mafuriko Mpwapwa. Ni yale yaliyoua watu wanne

Daniel Mbega

JENERALI Kutona (32), mkazi wa Kijiji cha Ilolo wilayani Mpwapwa, analiangalia shamba lake kwa masikitiko baada ya kufunikwa na mchanga ulioletwa na mafuriko makubwa yaliyotokea usiku wa Januari 31, 2017 na kusababisha vifo vya watu wanne, wakiwemo watatu wa familia moja.

Nyanya chungu ambazo alikuwa anataka anaanze kuzivuna kwenye shamba hilo la ekari mbili na kuzipeleka sokoni zote zimesombwa na maji na zilizosalia hazifai hata kwa matumizi ya binadamu.

“Huu ni umaskini mwingine, kwa sababu nilitegemea niuze nyanya chungu hizi ili kuikimu familia yangu, mvua zenyewe zimechelewa kunyesha na kuna ukame wa kutisha, wengi tulitegemea kilimo hiki cha umwagiliaji walau kutunusuru na baa la njaa,” anasema Jenerali akiieleza FikraPevu.

Jenerali ni miongoni mwa wakulima takriban 200 ambao mashamba yao yanayokadiriwa kufikia ekari 550, zikiwemo ekari 350 za umwagiliaji, yalizolewa na mafuriko hayo na mashamba kujazwa mchanga.

Katika mashamba ya umwagiliaji, wakulima wengi wamepata hasara kubwa, kwani mboga walizopanda pamoja na mahindi ambayo tayari yalikuwa yamekomaa, vyote vilizolewa na maji.

Dastan Lumolwa (72) anasema nusu ya shamba lake la ekari 14 limezolewa na mafuriko hayo wakati tayari mahindi yalikuwa yameota, wakati shamba jingine la umwagiliaji lenye ukubwa wa ekari 5, ambalo alikuwa amepanda bamia, pilipili hoho na nyanya lilizolewa lote na kufukiwa na mchanga.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mshango, William Sumisumi, amekiri kwamba zaidi ya wakulima 200 hawana mashamba baada ya mafuriko kuharibu na kuyafunika kwa mchanga, huku mazao mengi yakizolewa.

Sumisumi amesema kwamba, asilimia 90 ya mashamba yaliyoharibiwa na mafuriko hayo hayafai tena kwa kilimo, hali ambayo inaashiria baa la njaa na maisha magumu kwa kaya hizo hata kama mvua zitaendelea kunyesha.

“Mchanga unaouona hapa umeletwa na mafuriko ya mwaka huu na umeyafunika mashamba yote ambayo yalikuwa yanafaa kwa kilimo, kikiwemo cha umwagiliaji.

“Hapa unapopaona ni palikuwa na mazao yaliyostawi vyema na mengi yalikuwa tayari kuvunwa na kupelekwa sokoni, lakini sasa ufukara umeingia,” Sumisumi aliieleza FikraPevu.

FikraPevu ilitembelea eneo lililokumbwa na mafuriko na kujionea uharibifu mkubwa uliotokea.

Sumisumi, ambaye pia ni mwenyekiti wa umoja wa wakulima wa umwagiliaji katika eneo hilo, alisema wameanza kuorodhesha wakulima wote walioathirika na mafuriko hayo ili kuiwasilisha orodha hiyo katika Serikali ya Wilaya kuona kama wanaweza kupatiwa eneo jingine la kilimo.

“Kwa kweli tunaiomba serikali itufikirie kwa kutupatia eneo lingine, tunajua msimu huu tumechelewa, lakini hata kama itakuwa mwakani, ni vyema tukapata eneo jingine tuendeshe kilimo chetu ambacho ndiyo ajira kuu,” alisema Sumisumi.

Mvua hizo zilizonyesha usiku wa kuamkia Januari 31, 2017 zilisababisha maafa ambapo watu wanne, wakiwemo watatu wa familia moja, walisombwa na mafuriko.

Waliopoteza maisha katika tukio hilo ni Martha Mbega (66) na wajukuu zake wawili wa kike Shukuru Donald Chinyanya (16) aliyekuwa akisoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Mwanakiyanga na Bernadeta Mabula Sumisumi (9) aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Ilolo.

Wajukuu wengine wawili wa marehemu, Beka Mlami Ulanga (10) na Joseph Meli Sumisumi (8), ambapo Joseph alikutwa akiwa amekwea mti yapata kilometa mbili kutoka eneo la tukio huku mwenzake akikimbilia  kwenye nyumba ya jirani umbali wa meta 800.

Jesca Lubeleje (19), mkazi wa Kijiji cha Chinyika, naye alipoteza maisha baada ya kusombwa na mafuriko.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *