Wakulima wa mahindi kuunganishwa kwenye mnyororo wa thamani

Jamii Africa

Imeelezwa kuwa kukosekana kwa  teknolojia ya kisasa na masoko ya mazao  ni miongoni mwa changamoto zinazokwamisha  ukuaji wa sekta  ya kilimo nchini. Changamoto hizo zinachochewa na  uwekezaji mdogo wa rasilimali watu na fedha  kwenye huduma muhimu za kilimo.

Kwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, serikali inawajibika kuwawezesha wakulima nchini kupata pembejeo na teknolojia ya kisasa kuhakikisha wanazalisha mazao yenye ubora yanaweza kushindana kwenye soko la kimataifa.

Kwa kutambua hilo serikali ilianzisha benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kuhakikisha wakulima wanapata fedha kutoka taasisi hiyo kuendesha shughuli zao. Lakini tangu kuanzishwa kwake, benki hiyo haijawafikia wakulima wengi, jambo linalowakosesha fursa ya kupata mikopo na ushauri wa kiteknolojia.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji amesema  serikali imeitaka benki hiyo kuongeza matawi  ili kuwafikia wakulima wengi ambao wanahitaji mikopo kuongeza tija kwenye kilimo.

Amesema tayari benki hiyo imefika mkoa wa Dodoma na hadi kufikia Juni 30, 2018 itakuwa imefunguliwa ili kuwahudumia wakulima wa kanda ya kati  inajumuisha mikoa ya Dodoma, Singida.

“Baada ya ufunguzi wa ofisi ya Kanda ya Kati kukamilika Benki Itafanya uchambuzi wa fursa zilizopo Kikanda na hivyo kuchukua hatua na taratibu za kufungua ofisi nyingine kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha”, alisema Dkt. Kijaji.

Ameongeza kuwa TADB inatekeleza mpango wa miaka mitano (2017- 2021), wa kusogeza huduma karibu na wateja kwa kuanzisha ofisi za Kikanda katika Kanda ya Kaskazini, Kusini, Kati, Ziwa, Nyanda za Juu Kusini na Zanzibar kwa awamu mbalimbali.

Dkt. Ashatu amesema mikopo itakayotolewa kwa wakulima itatumia mfumo wa makundi; kundi la kwanza litahusisha wakulima wadogo wadogo kwa riba ya asilimia 8- 12, kundi la pili la miradi mikubwa ya kilimo kwa asilimia 12 – 16 kwa mwaka. Kundi la mwisho ni mikopo ya ushirika ambapo riba yake inaendana na hali ya soko la matumizi ya mkopo.

Amebainisha kuwa serikali inafanya majadiliano na wadau wa kilimo ili kupunguza kiwango cha riba ili kuwavutia wakulima wengi kukopa na kufaidika na kuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Thomas Samkyi alisema kukosekana kwa masoko ya mazao ya kilimo ni changamoto nyingine inayorudisha nyuma maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

Katika kutekeleza majukumu ya Benki hiyo, serikali imeanza kutoa huduma kwa kulenga minyororo michache ya ongezeko la thamani katika kilimo cha mahindi kwa kutoa mikopo ya ununuzi wa pembejeo, vifaa na vifungashio vya kisasa vya kuhifadhia mahindi na teknolojia ya uhifadhi wa mahindi ili kukidhi mahitaji ya soko la kimataifa.

“Kwa sasa tumejikita katika mnyororo mzima wa uongezaji wa thamani kuanzia uandaaji wa shambani hadi kwa upatikanaji wa masoko, ikiwemo mahitaji ya uzalishaji wenye tija kwenye sekta nzima ya kilimo kuanzia hatua za awali za utayarishaji wa mashamba.

“Kupima ubora wa udongo na virutubisho vinavyohitajika kwenye uzalishaji wa mahindi, upatikanaji wa pembejeo za kilimo zikiwemo mbegu bora, mbolea, madawa na vifaa na teknolojia mbali mbali za umwagiliaji na fedha kwa ajili ya kulipia gharama mbalimbali za uzalishaji wa mahindi,” alisema.

Samky alisema usaidizi na mikopo itakayotolewa itakuwa kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya kilimo katika kuimarisha minyororo ya thamani katika kilimo

“Inajumuisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na mitambo ya umwagiliaji, uchimbaji wa visima vya maji ya umwagiliaji, ujenzi wa mabawa ya uvunaji maji ya mvua, ujenzi wa maghala bora ya kuhifadhia mahindi na ujenzi wa miundombinu ya masoko,” alisema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *