Kifahamu Kilimo cha Alizeti na Faida yake Kiuchumi kwa Mkulima na Taifa

Jamii Africa

Alizeti ni mojawapo ya mazao muhimu ya biashara yanayochangia kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla. Asili yake, ingawa kwa sasa zao hili limeenea sehemu nyingi duniani, ni nchini Marekani.

Mbegu za zao hili hutoa mafuta ya kupikia, wakati makapi yanayotokana na mbegu hizo, maarufu kwa jina la mashudu, yakitumika kama chakula bora kwa ajili kulishia mifugo.

Taarifa kutoka Kitengo cha Mbegu za Mafuta katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Uyole, Mbeya, zinaeleza kwamba katika kila hekta moja ya shamba, mkulima huweza kuvuna kati ya magunia matatu hadi matano ya alizeti.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, zilizowekwa kwenye mtandao wa kijamii na FikraPevu kuziona, upandaji wa alizeti hutegemea sana hali ya hewa ya eneo husika. Katika maeneo yenye mvua nyingi, zao la alizeti huanza kupandwa mwishoni mwa Januari hadi katikati ya Februari, wakati katika maeneo yenye mvua kidogo huanza kupandwa mwanzani mwa Desemba hadi katikati ya Januari.

Inaelezwa kwamba kiasi cha kilo tatu hadi nne za mbegu za alizeti, zinatosha kupanda eneo la ekari moja. Kutokana na hali hiyo, mkulima anashauriwa kupanda mbegu tatu au nne katika kila shimo moja, kwa kuacha nafasi ya sentimita 75 kutoka mstari hadi mstari na sentimita 30 kutoka shimo hadi shimo.

“Shimo la mbegu liwe na kina cha sentimita 2.5 – 5. Wiki mbili baada ya kuota, mkulima anashauriwa kupunguza miche katika kila shimo, na kubakiza mche mmoja tu,” inaeleza taarifa hiyo ya Taasisi ya Utafiti ya Uyole, Kitengo cha Mbegu za Mafuta cha mkoani Mbeya.

Mbolea inayofaa kwa kilimo cha alizeti

Mbolea zinazofaa kutumika kwa kilimo cha zao hilo la alizeti kwa mujimu wa wataalam, ni zile za kupandia na kukuzia, hasa kwenye maeneo yasiyo na rutuba. Wakati wa kupanda, mkulima anashauriwa kutumia nusu mfuko kwa ekari moja ya mbolea ya kupandia, wakati mbolea ya kukuzia inashauriwa kupunguzwa mara mbili ya hiyo.

Nusu ya kwanza iwekwe wakati wa kupanda, na nusu ya pili iwekwe wiki mbili baadaye. Na inashauriwa wakati wa kuweka mbolea, ni muhimu kuhakikisha mbolea hiyo haigusani na mbegu au mche wa alizeti, kwa sababu mbolea hiyo huweza kuunguza mbegu au mche wa alizeti.

Alizeti hukua taratibu katika wiki chache za mwanzo. Hivyo wataalamu wa masuala ya kilimo na utafiti wanashauri palizi ya alizeti kufanyika mapema, ili kupunguza hasara.

Katika maeneo yaliyo na magugu machache, palizi moja tu inatosha. Aidha, katika maeneo yenye upepo mkali, wakati wa kupalilia inashauriwa kutengeneza kitu kama mfano wa matuta ili kuzuia kuanguka kwa mashina ya zao hili.

Wadudu waharibifu wa alizeti.

Alizeti hushambuliwa zaidi na ndege ambao huweza kuteketeza hadi asilimia 50 ya mazao shambani, ndiyo maana inashauriwa kutopanda alizeti karibu na msitu au pori.

Kutokana na uharibufu huo wa ndege, alizeti inashauriwa kuvunwa mapema mara tu chana la mbegu linapobadilika rangi na kuwa manjano. Inashauriwa kuweka ulinzi wa ndege kwa mutumia sanamu, makopo na au kuweka watu wa kufukuza makundi ya ndege, maana bila hivyo ndege wanaweza kupukutisha shamba zima la alizeti.

‘Americana Bollworm’ ni aina nyingine ya mdudu mharibifu za zao hilo, ambaye kwa wenyeji au wakulima wanamwita funza wa vitumba. Funza huyu hutoboa mbegu changa mara tu vitumba vya maua vinapofunguka na kuifanya mbegu kuharibika.

Aidha, zao la alizeti huweza kushambuliwa na magonjwa mengine mbalimbali, ukiwemo wa madoa ya majani, kutu, kuoza kwa mizizi, shina, kichwa na kushambuliwa na virusi.

Ili kuepukana na magonjwa ya aina hiyo, inashauriwa kutumia kilimo cha mzunguko wa mazao, kupanda mbegu safi zilizothibitishwa na wataalamu, kuchoma masalia ya msimu uliopita. Mkulima anashauriwa kutumia dawa yoyote ya kuulia wadudu ili kupambana na ugonjwa huu.

Kwa kawaida, alizeti iliyokomaa kichwa hubadilika rangi kutoka kijani kibichi na kuwa rangi ya njano. Uvunaji wa zao hili ni kwa njia ya kukata vichwa na kuvianika juani ili vikauke vizuri. Vikishakauka, vichwa hivyo hupukuchuliwa kwa kuvipiga na aina fulani ya mwiko au fimbo.

Akizungumzia kilimo hicho cha alizeti kwa wakulima wa Mwanza, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Evarist Ndikilo, amesema: “Asilimia kubwa ya ardhi ya mkoa huu inakubali kilimo cha alizeti. Kule Kwimba, Sengerema na kwingineko, watafiti wamebaini kwamba ardhi yake inafaa sana kwa kilimo cha alizeti.

Utafiti unaonyesha kwamba mkulima anaweza kupata magunia kati ya 10 na 12 ya alizeti kutoka katika ekari moja. Kwa hapa nchini, zao hili hustawi vizuri katika mikoa ya Singida, Mwanza, Shinyanga, Tabora, Kigoma, Rukwa, Katavi, Pwani na maeneo mengine nchini.

Faida ya mafuta ya alizeti

Dk. Raelk Mhlinyo, anayejitambulisha kama mtafiti wa tiba za asili kutoka Mkoa wa Singida, ameiambia FikraPevu kwamba amekuwa akitumia mafuta ya alizeti kwa ajili ya kutibu watu wanaokabiliwa na magonjwa mbalimbali, yakiwemo magonjwa sugu yaliyoshindika kutibaka kwa kutumia dawa za hospitalini.

“Nilipata utaalamu huu wa kutumia mafuta ya alizeti kwa ajili ya tiba kutoka kwa mtaalamu wa tiba za asili kutoka nchini Botswana, ambaye anayetwa Dk. Banaye Mwililowe. Mtaalamu huyu alikuja Tanzania mwaka 1998 kwenye maonyesho, nikakutanaye kwenye maonyesho hayo mimi nikiwa na dawa zangu za asili,” anasema Dk. Mhlinyo.

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, amekuwa akisisitiza Watanzania kuwekeza katika sekta ya kilimo, hasa katika zao hilo la alizeti, akisema bado halijapewa kipaumbele katika maeneo mengi nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *