Tanzania yaikalia kooni China usafirishaji wa ngozi ya punda

Jamii Africa

Hatimaye China imeanza mpango wa kuzalisha mazao ya punda katika miji yake ili kukabiliana na zuio la baadhi ya nchi za Afrika ambazo zimepiga marufuku usafirishaji wa nyama na ngozi ya punda kwenda katika nchi hiyo.

Tanzania imeungana na nchi nyingine za Afrika kama vile Uganda, Botswana, Niger, Burkina Faso, Mali, na Senegal kupiga marufuku biashara ya kuuza punda kwasababu inatishia kutoweka kwa wanyama hao ambao wanatumiwa na wakazi wengi wa bara hilo katika shughuli za kiuchumi ikiwemo kusafirisha mizigo na kulima.

Uamuzi wa kuzalisha punda wengi nchini China umefikiwa na kampuni ya Dong-E-E-Jiao ambayo inajihusisha na uagizaji wa ngozi ya punda kutoka nchi mbalimbali duniani ili kutengeneza dawa ya asili ijulikanao kama ‘ejiao’.

Akihojiwa na gazeti la Financial Times, Makamu rais wa kampuni hiyo, Liu Guangyuan amesema wanaagiza ngozi 450,000 za punda kila mwaka ambapo bei yake imepanda maradufu hadi kufikia Dola za Marekani 473 (Tsh. Milioni 1.065) kwa ngozi moja.

Kutokana na ongezeko la mahitaji ya ngozi wanapanga kufungua vituo vya uzalishaji wa mazao ya punda ili kukidhi mahitaji ya wateja wa dawa ya ‘ejiao’.

“Dong-E-E-Jiao imewekeza kwenye vituo vya uzalishaji katika majimbo 3 ya Kaskazini mwa China, ikitumia upandikizaji wa mbegu wa punda wakubwa ambao ngozi yake ni kubwa kuliko punda wa kawaida” amesema Liu na kuongeza kuwa,

“Hadi 2020 vituo vya uzalishaji vitatengeneza ngozi ya punda ya kutosha kukidhi mahitaji ya msingi”.

Amebainisha kuwa wakati wanaendelea kujenga vituo vya uzalishai, wamezigeukia nchi za Amerika ya Kusini ikiwemo Brazil, Colombia na Mexico ambazo zimefungua milango ya kuuza ngozi ya punda ili kujipatia faida kubwa.

 

Kwanini Ejiao?

Dawa ya Ejiao ambayo hapo awali ilikuwa inatumika kuzuia kuvuja kwa damu lakini wakati huu matumizi yake yameongezeka ambapo hupunguza uzee, kuongeza nguvu za kiume, kuzuia ugumba, kuharibika kwa mimba na kusawazisha hedhi kwa wanawake.

Licha ya dawa hiyo kuwepo kwa miaka mingi, lakini ilijipatia umaarufu mkubwa mwaka 2010 baada ya kampuni ya Dong-E-E-Jiao ya nchini China inayotengeza ejiao kuendesha kampeni ya kuitangaza dawa hiyo ambayo imewavutia watu wengi wanaokabiliwa na matatizo ya uzazi. Miaka 15 iliyopita ejiao ilikuwa inauzwa kwa Dola 9 lakini sasa imepanda hadi Dola 400 (Tsh. 900,800).

Kampuni za China zilianza kununua ngozi ya punda kutoka nchi za Afrika baada ya nchi zilizoendelea kuzuia biashara hiyo kwenye nchi zao ili kuepusha kupotea kwa myama huyo.

Ngozi ya punda inafika China kupitia nchi mbalimbali ikiwemo Kyrgyzstan, Brazil na Mexico. Lakini Afrika ndio kitovu cha biashara hiyo ikiongoza kwa punda wanaochinjwa na madhara yanayopatikana kwenye uchumi na mazingira.

Punda wanaonunuliwa katika nchi za Afrika Mashariki husafirishwa hadi Kenya ambako kuna kiwanda cha kusindika ngozi ya punda kijulikanacho kama Goldox Kenya Limitedambacho husafirisha bidhaa hiyo mpaka China ili kukidhi mahitaji ya soko ya ejiao.

Kutokana na uchache wa wanyama hao, bei yake imeongeza mara dufu ambapo vijana hutumia fursa hiyo kuingia katika vijiji na kuiba punda hao na kuwasafirisha hadi Kenya ili kujipatia fedha nyingi ambazo hutolewa na kampuni hiyo.

Pia biashara hiyo imeathiri shughuli za kiuchumi hasa katika mikoa ya kaskazini ya Arusha na Manyara ambayo iko karibu na Kenya.  Inaelezwa kuwa mwaka jana punda zaidi ya 475 waliibwa ili kusafirisha nchi jirani lakini waliookolewa ni 175 pekee.

Hali hiyo imewalazimu wakazi kutembea umbali mrefu kufuata maji na kutumia jembe la mkono kulima kutokana na kuadimika kwa punda katika maeneo yao.

                                               Dawa ya asili ya Ejiao inayotumika zaidi nchini China kwa kutibu magonjwa mbalimbali

 

Tishio la kutoweka kwa Punda  duniani

China ambayo ilikuwa inaongoza kuwa na  punda wengi  duniani, lakini idadi hiyo inapungua kila mwaka ambapo punda waliopo katika nchi hiyo ni milioni 6 kutoka milioni 11 na kwa makadirio ya chini inaweza kufikia milioni 3.

Tofauti na wanyama wengine kama nguruwe na ng’ombe, punda hawazaliani sana ambapo jike huzaa mara moja kwa mwaka na wana hatari ya mimba kuharibika kutokana mazingira na kazi ngumu wanazofanya.

Inaelezwa kuwa kuna punda milioni 44 duniani kote, lakini kila mwaka punda milioni 1.8 huchinjwa kwa ajili ya kutengeneza ejiao, hii ni kulingana na ripoti ya taasisi ya Donkey Sanctuary iliyopo Uingereza.

Mwaka 2017, watafiti wa Chuo Kikuu cha Misitu cha China walionya kuwa mahitaji ya ejiao yanaweza kusababisha punda kutoweka kabisa kama alivyo kwa mnyama pangolin.

“China imeamua kuagiza punda kwa gharama kubwa kutoka maeneo mbalimbali duniani, jambo linaloweza kuitumbukiza dunia kwenye mgogoro mkubwa wa punda”, imeeleza  ripoti hiyo iliyochapishwa kwenye jarida la Equine Veterinary.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *