WANANCHI wa Kijiji cha Kyota, Kata ya Kimwani, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera wameukataa mradi wa kilimo cha umwagiliaji wenye thamani ya Shs. 234.7 milioni uliokamilika tangu Juni 2015 baada ya kupata hasara ya mavuno ya mpunga.
Mradi huo ulilenga kumwagilia jumla ya ekari 300.
Hasara imetokea baada ya mkandarasi wa mradi kuzima mashine za kusukuma maji mashambani mara tu baada ya mpunga kupandwa akitaka kwanza halmashauri ya wilaya imlipe fedha iliyobaki ili akabidhi mradi.
FikraPevu imearifiwa kwamba, hali hiyo ilisabababisha mpunga kunyauka kwa kukosa maji baada ya kuwekwa mitaro inayovuna hata maji ya mvua na kuyapeleka mtoni ili yasukumwe kwa mashine yatakapohitajika mashambani.
Wakulima hao wanasema kwamba, kabla ya ujio wa mradi huo na kujengwa kwa miundombinu ya umwagiliaji walivuna magunia 20 hadi 25 ya mpunga kwa ekari moja.
“Katika mavuno ya mwaka huu tumepata kati ya gunia 2 hadi 5 kwa ekari moja baada ya mpunga kukauka kwa kukosa maji,” wamesema wakulima hao wakati walipozungumza na FikraPevu.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mjugu ulipo mradi huo, Batani Gwanamba, alisema baadhi ya wakulima wamemchukuliwa nyumba na mashamba waliyoweka dhamana na kuchukua mkopo na matajiri, ambapo walitegemea kulipa baada ya mavuno.
“Kuna familia 14 nyumba na mashamba yao yamechukuliwa baada ya kupewa mkopo na matajiri wakitegemea wangelipa baada ya mavuno, mpunga ulikauka baada ya kukosa maji na wakulima hawajui hatma ya msimu unaokuja,” alisema Gwanamba.
Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo katika mradi huo, Dismas Mathias, alisema hasara itasababisha mahitaji makubwa ya chakula na kuwa baadhi yao walichukua mkopo wa fedha kwa ajili ya kilimo wakitarajia mavuno ya kutosha.
“Kama wameshindwa kukubaliana tupewe ruhusa ya kubomoa mitaro na kutoa mabomba ili tuendelee kutegemea mvua kama zamani, wanavuna hata maji yetu ya mvua na kuyapeleka kwenye mto,” alisema Mathias.
Mmoja wa wakulima hao, Thobias Nteminyanda, alisema kuwa katika ekari moja amevuna magunia mawili tu tofauti na ilivyokuwa kabla ya kuanzishwa kwa mradi wa umwagiliaji unaotegemea maji ya Mto Kigoga zilikofungwa mashine.
Alisema walikuwa na matarajio makubwa na kukodi trekta kutoka wilaya jirani ya Chato kwa Shs. 70,000 kwa ekari moja baada ya trekta walilokodi kutoka halmashauri yao kuharibika. Walikuwa amelikodisha kwa Shs. 60,000 wakitanguliza nusu ya malipo.
Utata wa mradi wa kilimo cha umwagiliaji Kyota pia umehojiwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali katika taarifa yake ya mwaka 2015, ambapo alishauri mradi ukamilike na uanze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.
Majibu yaliyowasilishwa kwenye mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani Agosti 23, 2016 kuhusu hoja ya CAG, ilielezwa jumla ya ekari 100 za mpunga zimelimwa katika mradi wa Kyota na mavuno yalikuwa mazuri.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Chrisant Kamugisha, alisema mradi huo hautumiki kwa kuwa mkandarasi anataka alipwe na kuwa fedha za mradi huo zilihamishwa bila utaratibu na kupelekwa kwenye ujenzi wa maabara.
“Fedha ya mradi wa Kyota ilihamishwa bila utaratibu na kupelekwa kwenye matumizi ya ujenzi wa maabara, mkandarasi amefungia mashine hazitumiki na mradi haujakabidhiwa kwa ajili ya kuanza kutumika,” alisema Kamugisha.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Muleba, Emmanuel Sherembi, alisema suala la Mradi wa Kyota ameanza kulishughulikia na ameagiza kupewa taarifa ya kina kutoka kwa Mweka Hazina na Ofisa Kilimo na mchanganuo wa matumizi ya fedha.
Mkandarasi kupitia kampuni ya DRK Ltd, Najimu Kasange, hakuwa tayari kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu tatizo hilo akisema majibu yote yenye uhakika kuhusu mradi wa Kyota yako kwa Mkurugenzi wa Halmashauri.
Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17 uliotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango, kilimo cha umwagiliaji kitaimarishwa ili kuongeza uhakika wa chakula kwa kujenga skimu 78 za umwagiliaji wa mpunga.