Elimu ya Tanzania yasababisha kuibuka kwa matabaka ndani ya jamii

Jamii Africa

ATHARI mojawapo ya uwepo wa matabaka ni kukosekana kwa amani, kitu kinachosababishwa na kundi moja kuwa na uwezo wa kupata mahitaji na jingine kushindwa.

Hali hiyo hufanya ombwe la watu wenye nacho na wasio nacho kuongezeka.

FikraPevu inaona kwamba, hali hii inaweza kusababishwa na idadi kubwa ya watu kutokupata maarifa kwa ufasaha kutokana na ukosefu wa elimu inayostahili kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari.

Kwa hapa Tanzania, watu wengi wenye kipato cha chini hupeleka watoto wao shule za sekondari za serikali kutokana na unafuu wakati wale wenye nacho hupeleka watoto wao shule za binafsi zenye vitendea kazi na mazingira bora na walimu wa kutosha.

Tangu mfumo wa kuruhusu watu binafsi kuwekeza kwenye sekta ya elimu, shule hizi zimekuwa na matokeo mazuri kulinganisha na shule za serikali.

Hali hii hufanya watoto wengi wa kimaskini kushindwa kuendelea na masomo na hivyo kufanya ombwe la kimaarifa kati ya wenye nacho na wale wasio nacho.

Mfano, matokeo ya mwaka ya 2016 matokeo ya jumla ya taifa yalionyesha shule 10 zilizoongoza zote ni za binafsi na kati ya shule 50 bora za kitaifa hakuna shule ya serikali hata moja, lakini zilizoshika mkia zote ni shule zinazomilikiwa na serikali.

Mbali na hayo, hata wanafunzi bora kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita walitoka kwenye shule za kibinafsi, kwa bahati mbaya hakuna wanafunzi wa shule za serikali ambao wamewahi kutokea katika orodha ya wanafunzi bora kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Hali hii inafanya wanafunzi waliomaliza shule za binafsi kupata kuwa na nafasi kubwa ya kufanya kazi ambazo zinahitaji ujuzi wa kielimu ambazo mishahara mara nyingi huwa ya uhakika na ya kueleweka tofauti na kazi zisizohitaji ujuzi wa kielimu na mwisho wa siku ombwe la kipato kuendelea kuongezeka.

Kwa bahati mbaya ada vyuo ngazi ya cheti na kuendelea bado ni kubwa kiasi kinachosababisha wazazi wengi kutokuwa na uwezo wa kuwapeleka watoto wao kwenye vyuo hivyo, kwa hiyo bado inafanya uwezekano wa kuwepo kwa matabaka ndani ya jamii kuwa kubwa.

Utafiti uliofanywa na Richard Lynn na wenzake unaonyesha idadi kubwa ya watu ambao hawakupata elimu na maarifa ya kutosha ni rahisi kujiingiza katika uhalifu wa kutumia silaha, na kwa maana hiyo pia ni rahisi vijana wengi kushawishiwa na kujiingiza katika mambo ambayo yanavunja amani ya nchi.

Kuna vitu vingi sana ambavyo vimesababisha shule za serikali kutokufanya vizuri ambazo zimeshaelezwa vya kutosha, lakini bado kumekuwa na maboresha yaliyo ya taratibu sana hasa kwenye mikoa kama Mtwara na wilaya za mkoani Ruvuma, kwani huko ni kawaida kukutana na shule yenye mazingira yasiyoridhisha.

Kwa kuwa watu wengi wenye kipato cha chini watoto wao wanasoma shule za umma ambazo nyingi hazina walimu na vitendea kazi ni duni hivyo hakuna budi serikali iwe na nia ya dhati ya kutatua changamoto zote ambazo zinazikumba shule hizo ili kupunguza hatari inayolinyemelea taifa.

Kuwepo kwa watu wengi ambao hawana elimu ya kutosha kutokana na uzembe wa serikali juu ya uboreshaji elimu kunatengeneza mazingira ya kazi fulani kuonekana kwa ajili ya matajiri na kazi zingine ni kwa ajili ya watu maskini, jambo ambalo halipaswi kuwa hivyo kwa jamii yetu ya Kitanzania.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *