Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa angalizo kwa watumiaji wa simu za mkononi duniani kuwa waangalifu kwani matumizi ya muda mrefu ya simu hizo yaweza kusababisha kansa. Angalizo hilo la WHO ambalo lilitolewa jana na jopo la watalaamu wa Shirika hilo ambao walipitia matokeo ya tafiti mbalimbali (ambazo zimeshawekwa hadharani na zile ambazo bado) zilizoangalia uhusiano wa matumizi ya simu za mkononi na kansa lilifikia kutoa angalizo hilo kama hali ya tahadhari kwa watumiaji wa simu za mkononi. WHO imependekeza utafiti zaidi unahitajika kufanyika ili kuweza kuthibitisha uhusiano huo.
Taarifa hiyo ilipokewa kwa mshtuko mkubwa kila kona duniani huku maana yake hasa ikizua mjadala zaidi hasa kutokana na uzito wa chombo ambacho kimetoa angalizo hilo. Wengi wanakumbuka kuwa hata matumizi ya tumbaku kabla haijathibitika kuwa inasababisha kansa ilidhaniwa tu kuwa “yaweza kusababisha” kansa.
Jopo hilo liliongozwa na Dr. Jonathan M. Samet mtaalamu wa magonjwa makubwa kutoka Chuo Kikuu cha California na mjumbe wa Bodi ya Ushauri wa Masuala ya Kansa chini ya Ikulu ya Rais Barack Obama. Pamoja naye walikuwepo wataalamu wengine 30 kutoka nchi 14 ambao walifikia hitimisho hilo na kufanya angalizo hilo kuwa habari kubwa ambayo imepamba magazeti mbalimbali duniani.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari Dr. Samet alisema kuwa baada ya kupitia matokeo ya tafiti mbalimbali zilizokwisha fanyika huko nyuma wameona ni vizuri kuweza simu za mkononi kwenye kundi la vitu ambavyo “vinaweza kusababisha kansa” yaani “possible carcinogens”. Hii ni kwa ajili ya kutofautisha na vitu ambavyo vinajulikana wazi kusababisha kansa kama tumbaku na asbestos.
Hivyo simu za mkononi zimewekwa kwenye kundi B2 ambalo lina vitu mbalimbali ambavyo vinadhaniwa kuwa vyaweza kusababisha kansa japo hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa vinasababisha kansa. Kundi hili lina vitu maarufu kama dawa ya DDT, moshi wa mashine au magari, risasi na madawa kadhaa ya viwandani. Kwenye kundi hilo hilo vipo vitu kama kahawa vile vile.
Kutokana na kuwa kwenye kundi hilo makampuni ya simu hayakuchelewa kutoa angalizo la upande wao wakisema kuwa hakuna “ushahidi wowote” kuwa simu za mkononi zaweza kusababisha kansa. Bw. John Walls Makamu wa Rais (anayeshughulikia mawasiliano ya umma) wa Chama cha Wenye Makampuni ya simu alitoa kauli kuelezea kuwa “ripoti ya jopo la wataalamu halijasema kuwa simu za mkononi zinasababisha kansa” huku akikumbushia kwamba Mamlaka ya Mawasilino ya Marekani pamoja na Mamlaka ya Vyakula na Madawa ya nchi hiyo vyote vimeshawahi kutoa kauli kuwa hakuna ushahidi wa kisayansi wa mahusiano ya kansa na matumizi ya simu za mkononi.
Utafiti ambao umengaliwa hadi hivi sasa na jopo hilo la wataalamu unaonesha kuwa matumizi ya simu za mkononi hasa kuishika karibu na sikio kwa muda mrefu kunasababisha mawimbi ya radio kutoka kwenye simu kuongeza msisimko wa ubongo kitu ambacho kinadhaniwa kwa muda mrefu chaweza kusababisha kansa.
Hata hivyo kutokana na uzito wa Shirika la Afya Duniani mapendekezo yao kuwa watumiaji wa simu za mkononi wawe waangalifu hasa kutumia vitu kama spika za masikioni au kutumia spika za simu wakati wa kuzungumza kuliko kuweka simu masikioni muda mrefu. Prof. Henry C Lai wa Chuo Kikuu cha Washington ameliambia gazeti la New York Times kuwa “mjadala utaendelea lakini hii ni kauli ya kwanza kutoka WHO ambayo inatuonya kuwa waangalifu katika matumizi ya mionzi inayotoka kwenye simu za mkononi” akiongeza kuwa “kundi hili linawasomi mahiri na kama kuna mtu anasema kuwa jopo hili halifai basi itabidi tujiulize nani anafaa”.
Mwandishi Wetu