Kilimo cha viazi lishe kukabiliana na baa la njaa wilayani Ukerewe

Jamii Africa

WANANCHI wilayani Ukerewe katika Mkoa wa Mwanza wamejikita katika kilimo cha viazi lishe (viazi vitamu vya njano) kama njia ya kuongeza uhakika wa chakula.

Wakizungumza na FikraPevu kwa njia ya simu kutoka mjini Nansio, wananchi hao wamesema hamasa hiyo imetokana na agizo la Mkuu wa Wilaya hiyo, Estomih Chang’a, aliyewataka watendaji wote wa serikali kuhamasisha kilimo hicho kwa lengo la kujikimu kwa chakula lakini pia kuliongezea thamani.

“Tumejitahidi licha ya mvua kuchelewa kunyesha msimu huu, lakini walau kila kaya imepanda ekari moja ya viazi lishe, hii itasaidia kuwa na uhakika wa chakula,” Livingstone Mganga, mkazi wa Nansio, aliieleza FikraPevu kwa njia ya simu.

Mganga alisema kwamba, wakazi wa Ukerewe wamekuwa na kawaida ya kulima mazao mengi yakiwemo yanayostahimili ukame kama viazi na mihogo, lakini hamasa ya kilimo cha viazi lishe imekuwa kubwa baada ya kuambiwa umuhimu wa zao hilo hasa linapoongezewa thamani kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali.

Mwalimu Leocadia Vedasto wa Shule ya Sekondari Bukongo, Nansio, anasema kwamba, tangu mwaka 2016 yeye na akinamama wenzake walipoanza kilimo cha viazi lishe wameweza kunufaika kutokana na kuliongezea thamani.

“Baada ya kuvuna tunavikausha vizuri baada ya kuvimenya, halafu tunasaka unga ambao tunatengeneza bidhaa zaidi ya hamsini zikiwemo pilau la viazi, maandazi, kaukau (chips), chapatti, tambi, sambusa. biskuti, keki, na bidhaa nyinginezo ambazo mapato yake ni makubwa kuliko kuuza vibichi,” aliiambia FikraPevu.

Leocadia, ambaye pamoja na wanawake wengine 15 walikwenda Madrid, Hispania kupatiwa mafunzo mbalimbali ya ujasirimali kupitia Mradi wa Green Voices, anasema viazi lishe siyo tu vinaweza kuongeza akiba ya chakula, bali vinaweza kuongeza kipato cha familia kwani ekari moja iliyotunzwa na kustawi vizuri inaweza kutoa tani 7 (kilogramu 7,000).

Mradi wa akinamama

Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, Maria Tereza Fernandez (katikati mwenye miwani), wakati alipozindua mradi wa kilimo cha viazi lishe wilayani Ukerewe Julai 12, 2016. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Estomih Chang'a, na kushoto kwa Mama Tereza ni Balozi Getrude Mongela. (Picha na Daniel Mbega).

Julai 12, 2016 FikraPevu ilihudhuria uzinduzi wa mradi wa kilimo cha viazi lishe wa kikundi cha wanawake wa Green Voices Bukongo kinachoongozwa na Mwalimu Leocadia, ambapo walishuhudia bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa kwa viazi lishe.

Mradi huo ulizinduliwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, Maria Tereza Fernandez de la Vega, ambaye ni Rais wa taasisi ya Women for Africa Foundation inayofadhili miradi ya Green Voices Tanzania.

Katika uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Estomih Chang’a, alisema kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na uharibifu wa mazingira, ni vizuri wananchi kugeukia kilimo cha viazi lishe ambavyo vinastahimili ukame, lakini pia vina tija kubwa kwa kuongeza pato la familia.

“Ninashauri wananchi wote wa Ukerewe kulima viazi lishe kwa sababu mbali ya kuongeza akiba ya chakula, lakini vinaongeza pato la familia na taifa hasa vikichakatwa ili kutoa bidhaa mbalimbali,” alisema.

Balozi Mongela ahimiza

Shamba la viazi lililomea.

FikraPevu ilizungumza na Balozi wa Mfuko wa Wanawake Afrika, Getrude Mongella, ambaye alisema kilimo cha viazi lishe kikihimizwa kinaweza kuwa mkombozi kwa taifa kuhusu suala la uhakika wa chakula.

Alisema kwamba, kuanzishwa kwa kilimo hicho wilayani humo siyo tu kutawakwamua wanawake na wananchi wote, lakini pia kunaifanya Ukerewe kuwa kiini cha usambazaji wa zao hilo katika maeneo mengine ya Mkoa wa Mwanza.

“Ninawaomba watendaji wa serikali ya wilaya hamasisheni zao hili lilimwe katika visiwa vyote na kama ilivyokuwa zamani ambapo mbegu zote za pamba zilitoka Ukerewe, basi tengenezeni na zalisheni mbegu za kutosha msambaze katika wilaya nyingine za Mkoa wa Mwanza.

“Naamini mkoa wote ukilima zao hili njaa haitakuwepo na wanawake wanaweza kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo wakiziuza zitawakwamua kiuchumi,” alisema.

Hali ya kilimo Mwanza

Mwanza ni miongoni mwa mikoa michache nchini inayopata mvua mara mbili kwa mwaka katika misimu ya vuli na masika kwa wastani wa 720mm hadi 1,200mm, hali inayowawezesha wakulima kulima mara mbili.

Taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza inaeleza kwamba, mvua za vuli hunyesha kati ya mwezi Septemba na Januari, wakati zile za masika hunyesha kati ya mwezi Machi na Mei kila mwaka.

FikraPevu ambayo imetembelea mikoa ya Kanda ya Ziwa ukiwemo Mwanza, imebaini kwamba, mazao yanayopendekezwa kulimwa wakati wa vuli ni yale ya muda mfupi hususan viazi vitamu hasa mbegu zisizolikishwa (Non-Orange Fortified Varieties) aina ya Polista na Ukerewe, “Kishiga Mdege” na matembele, pamoja na mbegu zilizolikishwa (Orange Fortified) kama Ejumla, Karotoda na Kabode.

Aidha, mazao mengine ni mahindi hasa katika ukanda wa mazao (agro-ecological zone) unaopata mvua za wastani wa 1,100mm hadi 1,200mm kwa mwaka au zaidi ukanda ambao unajumuisha Tarafa za Ukara na Ilangala katika Wilaya ya Ukerewe na Tarafa za Kahunda na Buchosa katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, mbegu za mahindi zinazopendekezwa ni pamoja na mahindi chotara (hybrid) kama SeedCo yenye alama ya pundamilia (SC 513), Pannar inayokomaa kwa muda mfupi (PAN 4M-19) na kati (PAN 15), na Delkab (DKC 8053).

Aina ya mbegu za mahindi yasiyo chotara (ya chavua huria – OPV) ni pamoja na Kilima, Stuka, TAN 600H, Kitale na TMV 1.

Kuhusu zao la mpunga, FikraPevu imeelezwa kwamba, mbegu zinazofaa ni aina ya SARO 5 (TXD 306) na Supa inayolimwa mabondeni (low land rice), na NERICA 2 na 4 zinazolimwa nchi kavu.

Inaelezwa kwamba, msimu wa masika mazao yanayostawishwa ni mahindi, mpunga, dengu pamoja na mazao ya biashara, hususan pamba.

FikraPevu imebaini kwamba, Mkoa wa Mwanza wenye wakazi 2,772,509 unahitaji wastani wa tani 708,376 za chakula aina ya wanga kwa mwaka mzima, kiwango ambacho hata hivyo huwa hakifikiwi katika uzalishaji.

Kwa mujibu wa uchunguzi, katika msimu wa kilimo wa 2014/2015 mkoa huo ulizalisha tani 495,863.2 za chakula aina ya wanga ambacho ni asilimia 70 ya mahitaji, hivyo kuwa na upungufu wa asilimia 30, kiasi ambacho kinaweza kufikiwa ikiwa kilimo kitahusisha mazao mbalimbali ya chakula, hasa yenye kustahimili ukame kama viazi lishe.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *