Dodoma: Umwagiliaji wa nchi kavu wawanusuru wakulima na baa la njaa

Daniel Mbega

UHAKIKA na usalama wa chakula kwa jamii nyingi nchini Tanzania ni jambo linalopewa kipaumbele kwa ajili ya maendeleo ya uzalishaji na kuepukana na umaskini.

FikraPevu inatambua kwamba, katika kipindi ambacho Serikali ya Awamu ya Tano inalenga kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kutegemea malighafi za kilimo, suala la kilimo endelevu chenye kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni la muhimu hususan katika maeneo ambayo yana vyanzo vya kutosha vya maji.

Katika Kata ya Malolo, Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, wakulima wameongeza uzalishaji pamoja na uhakika wa usalama wa chakula kutokana na kilimo cha umwagiliaji wa nchi kavu, hivyo kuwanusuru wananchi na baa la njaa.

Malolo, ambayo ilimegwa katika Kata ya Ipera, inaundwa na vijiji vya Idodoma, Malolo yenyewe na Nzugilo na ina jumla ya wakazi 5,306, wakiwemo wanaume 2,592 na wanawake 2,714.

Unapoingia katika Kijiji cha Malolo ambacho ndiyo makao makuu ya Kata, umbali wa kilometa 155 kutoka makao makuu ya Wilaya ya Mpwapwa, unalakiwa na manzari nzuri ya nyumba bora za matofali ya kuchoma zilizoezekwa kwa bati, huku nyuma za tope zikiwa zinahesabika, hali inayoelezwa kwamba imetokana na mapato ya kilimo cha umwagiliaji.

Uchunguzi uliofanywa na FikraPevu umebaini kwamba, licha ya hali ya ukame kuyakumba maeneo mengi ya Tanzania na dunia kwa ujumla, hali iko tofauti katika Kata ya Malolo ambako wakulima wengi siyo tu wanaendelea na shughuli zao kama kawaida, bali wapo baadhi wanaotarajia kuanza kuonja mavuno mapya, hususan mahindi.

Wakati maeneo mengi ya Mkoa wa Dodoma ambao ni nusu jangwa yakiwa ndiyo kwanza yanaonja hali ya kijani kutokana na mvua zilizoanza kunyesha karibuni ili kupanda mazao mbalimbali ya chakula na biashara ambayo pia hulimwa katika Kijiji cha Malolo, hali kijijini hapo inaonyesha matumaini makubwa ya kuwepo kwa mavuno ya kutosha.

Katika kipindi cha masika, japokuwa mvua zimechelewa kunyesha, wakulima wa Malolo wanaonekana kuwa na pilika za kulima mahindi na mpunga, mazao ambayo yamemea pia kama yale yaliyopandwa wakati wa kiangazi katika umwagiliaji wa nchi kavu.

Awali ilikuwa ni rahisi kwa wakulima wa Kata ya Malolo kujikita katika kilimo cha umwagiliaji kwa sababu baadhi ya mazao yanahitaji mvua nyingi ambazo kwa sasa hazitabiriki.

Mchungaji Yeremia Lyakwasa, mkulima na mkazi wa Kijiji cha Malolo, anasema kilimo cha umwagiliaji kimewakomboa wengi kiuchumi na kikiendelezwa hata katika maeneo mengine nchini kinaweza kukuza mapato ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, anasema kuwa changamoto kubwa iliyopo ni ukosefu wa mbegu bora zinazoendana na mazingira, kwani wakulima walio wengi wanatumia mbegu za kienyeji.

Kwa upande wake, Everyne Lemabi, anasema amekuwa akitegemea kilimo cha umwagiliaji kwa kuwa ndicho ambacho kinampa uhakika wa chakula huku zao kuu analolitegemea likiwa mpunga.

“Lakini mbegu ndiyo tatizo, siku zote natumia mbegu za kienyeji – nikishavuna nahifadhi halafu msimu ukifika nachota nakuja kupanda,” anasema na kuongeza kwamba hajawahi kupata mbegu za ruzuku.

Zuberi Said Mlinji, Ofisa Ugani wa Kata ya Malolo, anasema kwamba wamejitahidi kuwahamasisha wakulima kutumia kilimo endelevu cha umwagiliaji katika maeneo ya nchi kavu pamoja na mabondeni, ambacho kimekuwa mkombozi mkubwa kiuchumi.

Mtaalam huyo wa kilimo anasema eneo la umwagiliaji kwa ujumla katika kijiji hicho ni hekta 500, huku hekta 100 kati ya hizo ni za umwagiliaji wa nchi kavu.

“Tunawashauri kupanda mazao ya chakula na biashara, hususan yale ambayo soko lake ni la uhakika kama mpunga, mahindi, nyanya, maharage na mbogamboga pamoja na matunda,” anasema.

Mlinji anasema kwamba, tangu mwaka 2016 ameanzisha zao za matikiti maji, ambapo shamba lake lenye ukubwa wa ekari moja limekuwa kama shamba darasa.

“Kabla ya hapo hakukuwa na kilimo cha matikiti maji, lakini tangu nilipoanzisha kilimo hiki msimu huu nimeshuhudia wakulima wengi wakihamasika,” anasema.

Anasema kilimo cha zao hilo, mbali ya mazao mengine, kinaweza kumtoa mkulima kwenye umaskini, kwani kama litatunzwa vizuri, mkulima anaweza kupata Shs. 8 milioni kwa ekari moja baada ya miezi mitatu wakati gharama zake ni chini ya Shs. 1.5 milioni.

Anaongeza: “Unapolima matikiti maji huhitaji kuyabeba kupeleka sokoni, malori yanakuja mpaka shambani na wanachuma wenyewe wakati wewe ukihesabiwa fedha zako.”

FikraPevu imearifiwa kwamba, mazao yanayolimwa wakati wa masika katika eneo la umwagiliaji ni mahindi na mpunga, na wakati wa kiangazi wakulima hao wanalima zaidi vitunguu, maharage, nyanya na mbogamboga.

Katika kufanikisha kilimo hicho hata wakati wa kiangazi, wananchi hao wanategemea mito miwili mikuu ya Chabi na Sazima, ambayo pia inatumiwa na wakulima wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro ambao wako ng’ambo ya pili ya Mto Chabi.

“Huku kuna mifereji miwili mikuu inayotumiwa kumwagilia mashamba yaliyoko nchi kavu, wenzetu wa upande wa Kilosa wana mifereji mitatu, lakini tumekubaliana kutumia mifereji miwili miwili kwa zamu – wao wanaamua ni mifereji gani itumike,” anasema na kuongeza kwamba, changamoto za matumizi ya maji hayo hutatuliwa kwa vikao vya pamoja baina ya pande hizo mbili.

Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, Bosco Paulo Mwaluga, anasema kwamba, kama mkazi yeyote wa Malolo ni maskini, basi umaskini ameutaka mwenyewe kwa kuwa zipo fursa nyingi za kiuchumi kupitia kilimo.

“Ukitaka kuwa maskini hapa Malolo basi umeamua mwenyewe, vinginevyo fursa ni nyingi na ardhi ipo ya kutosha yenye rutuba, hata kama huna shamba, yapo mashamba mengi ya kukodi,” anasema.

Hata hivyo, anabainisha kwamba, changamoto inayowakabili wakulima ni miundombinu mibovu ya barabara, ambapo wanategemea zaidi kusafirisha mazao yao kupeleka Iringa au Morogoro japokuwa wako ndani ya Mkoa wa Dodoma.

“Ni rahisi kufika barabara kuu ya Morogoro-Iringa ambao ni mwendo wa kilometa 20 tu kuliko kwenda Mpwapwa ambako barabara ni mbovu na hakuna magari yanayokuja,” anasema.

Kilimo endelevu hasa cha umwagiliaji ndicho kinachohimizwa na serikali kwa kuwa ni cha uhakika kuliko kutegemea mvua hasa katika kipindi hiki ambacho mabadiliko ya tabianchi yameathiri hata upatikanaji wa mvua za kutosha.

Aidha, kilimo hicho endapo kitatumiwa vyema, kinaweza kuwafanya wananchi wakafikia hali ya uchumi wa kati kama mipango mbalimbali ya maendeleo, hususan Mkukuta na Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea Mwaka 2025 pamoja na Malengo Endelevu ya Dunia (SDG), yanavyoelekeza.

<Mwisho/FP>

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *