LICHA ya kutajwa kuwa mkombozi wa kiuchumi, lakini zao la tumbaku bado limeendelea kuwa hatari duniani kutokana na kusababisha vifo milioni 6.
Wanaopoteza maisha kutokana na mazao ya tumbaku, ni wale watumiaji na wasio watumiaji wa bidhaa za zao hilo kila mwaka.
Uchunguzi wa FikraPevu unaonesha kwamba, kila baada ya sekunde sita mtumiaji mmoja wa tumbaku hufariki dunia kwa madhara yatokanayo na zao hilo, yakiwemo saratani ya mapafu, numonia na maradhi mengine sugu.
Nchini Tanzania, kama ilivyo katika nchi nyingine za Afrika, serikali imekuwa ikihamasisha kilimo cha tumbaku hasa katika mikoa ya Ruvuma, Tabora, Mbeya, Morogoro na Iringa kwa nia ya kukuza uchumi na kuongeza pato la familia, hivyo kuondoa umaskini wa kaya.
Zao hilo, FikraPevu imeelezwa kwamba, linashika nafasi ya pili nyumba ya zao la pamba kati ya mazao ya biashara kwa kuchangia fedha za kigeni.
Wahamasishaji wa kilimo cha tumbaku wanasema zao hilo linastawi katika ardhi isiyo na rutuba ambayo haiwezi kutumia kwa kilimo cha mazao mengine, lakini kubwa zaidi ni kuongeza fedha za kigeni na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.
Aidha, si serikali au wadau wa tumbaku wanaotilia mkazo kueleza madhara yatokanayo na matumizi ya tumbaku.
Tumbaku na Pato la Taifa
Kulingana na taarifa za Benki Kuu ya Tanzania (BOT), mchango wa zao la tumbaku kwenye uchumi wa taifa ni mkubwa, ambapo inaelezwa kuwa kila mwaka zao hilo huchangia zaidi ya Dola za Kimarekani 150 milioni.
Wakulima wakubwa kwa wadogo wanalima tumbaku nchini na serikali inapata kodi kubwa, hivyo inakuwa vigumu kwa Bajeti ya Serikali kupangwa bila tumbaku kuguswa kama chanzo cha mapato.
FikraPevu inafahamu kwamba, mwaka 2014/2015 zao la tumbaku lilikuwa miongoni mwa mazao makuu ya asili ya biashara yaliyozalisha tani 937,060.2 ikilinganishwa na tani 897,028 zilizozalishwa katika mwaka 2013/2014.
Katika mwaka 2014/2015 tumbaku ilishika nafasi ya nne kwa kuzalisha tani 113,600 ikiwa nyuma ya sukari (tani 300,230), pamba (tani 203,313) na korosho (tani 200,000), wakati mazao ya chai ilikuwa tani 35,500, pareto (tani 7,600), mkonge (tani 40,000) na kahawa tani 40,759.2.
Vifo vinavyosababishwa na tumbaku
Haya ndiyo madhara yanayompata mtumiaji wa tumbaku na bidhaa zake.
Inaelezwa kwamba, zaidi ya watu bilioni moja ulimwenguni wanavuta tumbaku na takriban watu milioni 6 hufariki dunia kila mwaka kutokana na madhara yatokanayo na tumbaku, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Hii maana yake ni kwamba, kila baada ya sekunde sita mvutaji mmoja wa tumbaku hufariki dunia.
Zaidi ya vifo milioni 5 kati ya hivyo ni matokeo ya uvutaji wa moja kwa moja wakati zaidi ya vifo 600,000 ni vya watu wasiovuta ambao huathirika na moshi wa tumbaku.
Inaelezwa kwamba, karibu 80% ya wavutaji tumbaku wote duniani wanaishi katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.
Uvutaji wa tumbaku katika nchi zinazoendelea unakua kwa asilimia 3.4 kila mwaka huku mauzo ya sigara zenye vishungi ulimwenguni yakiwa sigara bilioni 15 kwa siku – hii ikimaanisha kwamba sigara milioni 10 huuzwa kila dakika duniani.
Hata hivyo, inaelezwa kwamba, Waingereza waliokufa kwa madhara ya tumbaku ni mara 12 ya vifo vilivyotokea wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Takwimu zinaonesha kwamba, nchini Marekani pekee, uvutaji wa tumbaku husababisha vifo vya watu zaidi ya 480,000 kila mwaka, vikiwemo vifo 42,000 vinavyotokana na kuvuta moshi ya tumbaku hata kama siyo wavutaji.
Hali hiyo inaonesha kwamba ni karibu kifo kimoja kwa kila vifo vitano kila mwaka, au vifo 1,300 kila siku, ambapo kwa wastani wavutaji wa tumbaku hufa miaka 10 kabla ya umri wao.
Taasisi ya Udhibiti wa Magonjwa nchini Marekani (CDC) inaeleza kwamba, wanawake wengi wanakufa kutokana na saratani ya mapafu kuliko saratani ya matiti.
Dkt. Noel Peter, wa Mbagala jijini Dar es Salaam, anasema kwamba athari za sigara ni kubwa na zinachangia vifo vingi kwa wavutaji na wasio wavutaji.
“Mvutaji anaathirika, lakini hata asiye mvutaji, akivuta moshi wa sigara unamuathiri kama unavyomuathiri yule anayevuta na madhara yake ni makubwa sana,” ameiambia FikraPevu.
Aidha, Dkt. Noel anasema, karibu 80% (au vifo 8 kati ya 10) ya vifo vyote vya magonjwa sugu ya mfumo wa upumuaji (chronic obstructive pulmonary disease – COPD) vinasababishwa na uvutaji wa tumbaku.
Mkazo wa kilimo
FikraPevu inatambua kwamba, Sera na mikakati mbalimbali ya kilimo imekuwa ikitazama tumbaku kama mkombozi kwa wakulima na serikali kwa ujumla.
Bidhaa za tumbaku, hasa sigara, ni biashara ya makampuni makubwa ya kimataifa yakiwa yametawanya mitandao yao katika mataifa mbalimbali ulimwenguni, ikiwemo nchini Tanzania.
Mwaka 2011, nchi tano za Afrika (Malawi, Tanzania, Zimbabwe, Zambia na Msumbiji) kwa pamoja zilizalisha zaidi ya tani 530,000 baada ya kuongeza uzalishaji kutoka tani 372,000 mwaka 2000 ambapo wakati huo ni Zimbabwe na Malawi zilizokuwa kwenye kundi la 20 bora.
FikraPevu inatambua kwamba, kumekuwepo na ongezeko la asilimia 47 katika uzalishaji wa tumbaku barani Afrika kuanzia mwaka 2000 hadi 2011.
Kwa mwaka huo, kumbukumbu zinaonyesha kwamba, usafirishaji wa majani ya tumbaku nje ya nchi kwa mataifa ya Malawi, Zimbabwe na Msumbiji ulishika namba moja kati ya mazao ya kilimo.
Tanzania yashika nafasi
Aidha, kwa Tanzania, tumbaku ilishika nafasi ya pili nyuma ya pamba na huko Zambia zao hilo lilishika nafasi ya tatu kati ya mazao ya kilimo yaliyosafirishwa nje.
Nchini Malawi, mojawapo ya nchi zinazotegemea zaidi uchumi wa tumbaku duniani, zao la tumbaku linaingiza asilimia 60 ya mapato ya taifa.
Taarifa ambazo FikraPevu inazo zinaonyesha kwamba, thamani ya fedha za kigeni zilizoingizwa na nchi hizo tano ilikuwa imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 70 kutoka Dola 960 milioni za Marekani mwaka 2000 hadi Dola 1.658 bilioni mwaka 2011.
Uzalishaji wa tumbaku umeendelea kukua tangu mwaka 2003 hadi kufikia asilimia 25 kutoka tani 6.03 milioni mwaka 2003 hadi tani 7.5 milioni mwaka 2012 ambapo nchi za Kiafrika zilizalisha tani 650,000, au asilimia 8.7 ya uzalishaji wote duniani.
Katika msimu wa 2015, mataifa 10 yaliyozalisha kwa wingi tumbaku na kiasi chake kwenye mabano yalikuwa; Bara China (tani 2,995,400), Brazil (862,400), India (720,730), Marekani (397,540), Indonesia (196,300), Pakistan (129,880), Malawi (126,350), Argentina (119,430), Zambia (112,050), na Msumbiji (97,080).
Athari za kimazingira
Moja ya majiko ya kienyeji yanayotumia kuni nyingi katika kukaushia tumbaku.
Licha ya tumbaku kuingiza fedha nyingi, lakini FikraPevu inaona kwamba, kilimo hicho kikitazamwa kwa darubini kali, faida yake haina maana sana kama madhara yatokanayo na matumizi yake kutokana na kuleta athari kubwa za kiafya kwa wananchi na uharibifu mkubwa wa mazingira kutokana na ukataji wa miti inayotumika kama kuni za kukaushia tumbaku.
Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Songea, Kaswam Maswaga, anasema hakuna juhudi za makusudi zinazofanywa na wakulima za kupanda miti kwa ajili ya kupata nishati ya kukaushia tumbaku na akatoa wito kwa wakulima kuhakikisha juhudi za kupanua mashamba mapya ya tumbaku zisilete athari za kukata miti kwa ajili ya kukaushia tumbaku.
Wanaharakati wasemaje?
Wafanyakazi kama hawa wanaochambua tumbaku nao wako hatarini kupata madhara kama ilivyo kwa wavutaji.
Frank Komba, mwanaharakati wa mazingira kutoka wilayani Namtumbo, anasema mashamba ya tumbaku yanasababisha uharibifu mkubwa wa misitu wilayani humo pamoja na mikoa mingine inayolima tumbaku kutokana na zao hilo kuhitaji kuni nyingi kwa ajili ya kuchomea tumbaku.
“Ukataji holela wa misitu ili kukaushia tumbaku umeleta athari kubwa ya mabadiliko ya tabia nchi katika kipindi cha miongo michache mkoani Tabora, na sasa mkoa umekuwa na ukame,” anasisitiza Komba.
Komba anasema jitihada za kushawishi wakulima kuacha kulima tumbaku na kuanza kuzalisha mazao mbadala zimekuwa ngumu kwa kuwa wakulima wanaamini zao hilo lina faida kubwa ukilinganisha na mazao mengine ya biashara.
“Ukataji miti ovyo unaoendelea kufanyika kila mwaka karibu wilaya nzima ya Namtumbo, umechangia sana uharibifu wa vyanzo vya maji wilayani Namtumbo, huku kiwango cha mvua kikiendelea kupungua mwaka hadi mwaka,” anasema John Nilahi mkazi wa Namtumbo.
Zao la tumbaku linateketeza maelfu ya tani za kuni kila mwaka zinazotumika kwa ajili ya kukaushia tumbaku kwa mfano inakadiriwa katika mkoa wa Tabora kila mwaka kuni zinazotumika ni zaidi ya meta za ujazo 124,389 za miti hukatwa.
Wakulima wengi hawajui madhara ya zao la tumbaku katika mazingira licha ya kwamba athari zinazotokana na ukataji miti ovyo kwa ajili ya kukaushia tumbaku zimeanza kujitokeza katika vijiji vingi.
Tishio la kuleta jangwa
FikraPevu inafahamu kwamba, utafiti uliochapishwa na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine ambao ulifanyika mkoani Tabora Machi 2012, unaonesha kuwa Tanzania inapoteza zaidi ya ekari 61,000 za misitu kila mwaka kutokana na zao la tumbaku hali ambayo inaliweka zao hilo shakani kwa kuwa linaweza kuleta jangwa.
Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 75 ya wakazi wa wilaya za Tabora ni wakulima wa tumbaku, wanalima wastani wa ekari 1.3 za tumbaku kwa mkulima kila msimu, zinazohitaji meta za ujazo 23 za kuni kukaushia majani ya tumbaku.
Mtafiti Mkuu katika utafiti huo, Mwita Mangora, anasema masalia ya misitu mkoani Tabora yaliopo sasa hayana uwezo wa kukidhi matumizi makubwa ya kuni za kuchomea majani ya tumbaku yanayoongezeka kila mwaka.
Marufuku ya kimataifa
FikraPevu inafahamu kwamba, mnamo mwaka 2003, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliridhia Azimio la Mfumo wa Kudhibiti Tumbaku (Framework Convention on Tobacco Control – FCTC), mkataba wa kimataifa uliolenga kupunguza mahitaji ya bidhaa za tumbaku na usambazaji wake.
Mbali ya mikakati ya kupunguza mahitaji, mkataba unaeleza kwamba nchi zilizoridhia, ikiwemo Tanzania, lazima ziangalia mbadala mwingine wa kiuchumi kwa wakulima wa tumbaku, kupunguza ukubwa wa ardhi ya kilimbo cha tumbaku, na kulinda mazingira pamoja na afya za wakulima.
Hali hiyo inatokana na madhara makubwa yatokanayo na kilimo cha tumbaku pamoja na matumizi yake, ambapo kwa Marekani pekee, inaelezwa kwamba zaidi ya watu milioni 16 wanaugua maradhi ambayo yamesababishwa na uvutaji wa tumbaku.
Gharama kubwa
FikraPevu inatambua kwamba, sekta ya tumbaku inatumia mabilioni ya fedha kila mwaka kwa ajili ya matangazo na promosheni.
Taarifa zinasema, kwa mwaka 2014, zaidi ya Dola 9 bilioni zilitumika kwa matangazo ya tumbakuna bidhaa zake nchini Marekani pekee kutangaza sigara – sawa na takriban dola 25 milioni kila siku, na dola milioni moja kila saa.