Baiskeli: Usafiri unaotegemewa na wajawazito Kyela

Stella Mwaikusa

Wajawazito wa vijiji vya Masoko na Busoka vinavyopatikana kata ya Busale wilaya ya Kyela, wamekuwa wakitumia usafiri wa baiskeli wakati wa kwenda kupima maendeleo ya ujauzito katika zahanati ya Lema, ambayo iko umbali wa km sita kutoka vijiji  hivyo.

Zawadi Oscar (22) mkazi wa kijiji cha Masoko  anasema alipokuwa na ujauzito alikuwa akitumia usafiri wa baiskeli kwenda kliniki ,kutokana na zahanati ya Lema kuwa mbali na kijiji hicho.

“Nilikuwa na ujauzito wa miezi nane, ,lakini  niliendesha baiskeli kwenda kliniki, maana afadhali kwenda huko kwa baiskel kuliko kutembea kwa mguu, unachoka sana” anaeleza Zawadi.

kyela

Wanawake wa kijiji cha Masoko wakiwa wamekusanyika ili kuongea na mwandishi wa habari hii

Chistina Musa  mkazi wa kijiji cha Masoko anasema usafiri wa baiskeli kwa wajawazito katika kijiji hicho ni kitu kilichozoeleka, kwani hata yeye hutumia usafiri huo anapoenda kliniki katika zahanati ya Lema.

Anasema haoni tatizo kuendesha baiskeli, japo alikiri kwamba baada ya kutoka zahanati hujisikia kuchoka, lakini hana namna kwani katika kijiji anachoishi hakuna zahanati.

Mganga mkuu wa zahanati ya Lema, Mariam Ninde anasema ni kweli wajawazito kutoka vijiji vya Masoko na Busoka hutumia usafiri wa baiskeli na kuutaja usafiri huo kutokuwa na madhara kiafya kwa wajawazito.

“Mjamzito anapoendesha baiskeli ni moja kati ya mazoezi kwa hiyo hakuna ubaya,” anaeleza Ninde.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *