UMEPITA mwaka mmoja na miezi mitatu tangu tumefanya uchaguzi mkuu na sasa tumesalia na miaka mitatu na miezi saba mpaka uchaguzi mwingine mwaka 2020.
Wakati wa kampeni za mwaka 2015 wabunge walipata fursa ya kuweka sera na ahadi zao hadharani ili kutushawishi tuwapigie kura watuongoze katika nchi ya ahadi.
Mgombea Ubunge jimbo la Mwibara, Kangi Ligora, akionyesha machejo ya furaha, baada ya kuomba kura wananchi katika mkutano wa kampeni wa Mama Samia Suluhu Hassan mwaka 2015.
Ni imani yangu ili sera na ahadi za wabunge hawa ziweze kufanikiwa, ni dhahiri washirikiane na wananchi.
Wabunge wako wapi?
Swali la msingi baada ya kuwapa kura wabunge, leo hii wako wapi? Mbona hatuwaoni majimboni kwetu?
Nikiri kuwa siyo wabunge wote ambao hawaonekani majimboni kwao, kuna baadhi ya wabunge wako majimboni wakitenda kazi na jamii zao, ila pia kuna wabunge ambao huenda majimboni mwao wakati wa misiba, majanga; kama mafuriko ama wakisikia ujio wa waziri Fulani, ndo wao hutokea majimboni.
Wajibu wa wabunge
Kwani wabunge kazi yao ni nini hasa? Je, wabunge hupaswa kwenda bungeni kwa niaba yetu na kuwasilisha shida zilizopo majimboni na kusubiri serikali kutenda ama wanapaswa kutenda zaidi ya hapo?
Kwa mtizamo wangu, nadhani yapo majukumu zaidi ya wabunge kwenda kwenye vikao vya bunge, kwani wabunge wametokana na sisi wananchi, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanafanya kazi na wananchi wao na sio kwa niaba ya wananchi wao.
Ni vyema kuelewa kuna tofauti ya wabunge kufanya kazi kwa niaba ya wananchi na kufanya kazi na wananchi.
Ni ukweli kwamba kwa muda mrefu wabunge wamekuwa wakitenda kazi zao kwa niaba ya wananchi na sio kufanya kazi na wananchi wao.
Ili maendeleo endelevu na imara yaweze kuonekana ni vyema wafanye kazi na sisi wananchi na sio kwa niaba yao, kwani sisi wananchi tunamajukumu ya kushiriki kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo yetu wenyewe.
Ikumbukwe kuwa wabunge ni ‘kiunganishi’ baina ya wananchi na serikali na ni muhimu kwa wabunge kutushirikisha kila hatua wanayofanya kuleta maendeleo kama walivyoadhidi wakati wa kampeni.
Mantiki ya makala haya ni kueleza yale ambayo wabunge wanapaswa kufanya ili kuleta maendeleo endelevu na sio kubaki kuwa wawakilishi na kutenda kwa niaba ya wananchi.
Ni ukweli kuwa wabunge wengi hurudi katika majimbo yao mara kadhaa, ila wananchi wanaweza wasitambue ya kuwa wamerudi majimboni mwao na wengine huishia kuwaona wabunge wao wakati wa uchaguzi tu.
Ieleweke kuwa wabunge wametokana na wananchi ambao tuliwapa ridhaa, ni wazi wanapaswa kuishi katika majimbo yao.
Haileti mantiki yeyote kama tunamchagua mbunge asiyeishi jimboni mwake na kuwa anaishi sehemu zingine.
Kuwa na wabunge wanaoishi maeneo tofauti na majimbo yao, ni sawa na kuwa na baba asiyeishi na familia yake, ambaye anaishi kwa jirani, anachokifanya ni kuja kuwasalimia watoto wake pale anapojisikia.
Wasikae ofisini
Kwa upande mwingine, wabunge wanapokuwa majimboni muda wote, kazi yao kubwa sio kukaa ofisini, kwani hatukuwachagua ili wakae ofisini, bali ofisi zao ni katika mitaa, vijiji ama mijini katika majimbo yao.
Hapa ningependa kusisitiza kuwa kazi kubwa ya wabunge ni kufanya vikao na wananchi wao ama makundi mbalimbali ya wataalamu katika majimbo yao, ili kujua changamoto na maoni ya wananchi kuhusu maendeleo.
Wabunge wanapaswa kukaa na wananchi katika sehemu mbalimbali za majimbo yao na kutoa mrejesho wa kila hatua wanayopitia katika kuhakikisha sera walizoahidi zinatimia.
Fedha za serikali
Ni wazi ya kuwa mara nyingi sera zinazoahidiwa na wabunge hutegemea fedha za serikali ili kuona zinatimia, hivyo serikali ikishindwa kutoa fedha, ni wazi kuwa ahadi za wabunge hazitatimia.
Hapa ndo maana nasisitiza kuwa maendeleo ya majimbo yanachangiwa na wananchi na sio kuwaachia wabunge watende kwa niaba yetu.
Wabunge wanapaswa kuwa chachu ya maendeleo kwa kuwashirikisha wananchi katika jitihada wanazofanya na kuweka bayana changamoto, ili kuchangia mawazo ya kuzitatua.
Shida Tarime
Ni vyema nikatoa mfano katika hili, mimi naishi wilayani Tarime, mkoani Mara, kwa sasa, ambako shida kubwa ya wilaya yetu ni maji safi na salama, kwani bado asilimia kubwa ya wakazi wa wilaya hiii wanategemea maji ya visima vya asili ama vile vya kuchimbwa kwa mikono. Ni watu wachache sana wenye uwezo wa kupata maji ya bomba.
Lakini kitu cha ajabu, wilaya hii imezungukwa na mto mkubwa, Mto Mara na pia kwa upande mwingine imezungukwa na Ziwa Victoria, ila vyanzo hivi havitumiki kuleta maji safi na salama kwa wananchi wake.
Kutotumika kwa maji ya vyanzo hivyo kunatokana na kile kinachoelezwa kuwa kukosekana kwa fedha za kuyavuta maji hao, kwa kuwa serikali haijatenga fedha.
Hapa tukisubiri serikali itenge fedha kwa ajili ya kuleta haya maji, tutasubiri sana.
Tunapopaswa kuona jitihada za mbunge ambapo anapaswa kukaa na wananchi na kuzungumza na wananchi wake na kutoa mapendekezo ya pamoja kuona nini tunaweza kufanya ili kupata maji kutoka vyanzo hivyo.
Ni muhimu wabunge kushirikisha wananchi na watalaamu katika kutatua changamoto zinazokabili majimbo yao, na siyo kusubiri tu michango kutoka serikalini.
Uwepo wa wabunge majimboni sio kushiriki misiba na sherehe tu, bali ni kuwa chachu ya maendeleo majimboni.