Tripoli yaanguka; Mwisho wa Gaddafi?

Mwanakijiji

Ndani ya masaa 72 Jiji la Tripoli nchini Libya limeanguka mikononi mwa waasi ambao walikuwa wanaendesha kampeni ya kumuondoa rais wa nchi hiyo Dikteta Muammar Gaddafi. Kuanguka kwa jiji la Tripoli kunaashiria kuhitimishwa kwa kampeni hiyo iliyozidi kwa miezi sita kamili sasa na ambayo imegharimu maisha ya mamia ya wananchi wa Libya ambao wamekuwa chini ya utawala wa Gaddafi na familia yake kwa zaidi ya miaka 40 sasa.

Mwishoni mwa juma waasi wa Libya walikuwa wanalizunguka jiji hilo la Afrika ya Kaskazini kama fundo la kamba na pole pole waliteka maeneo mbalimbali na kuzima majaribio yoyote ya utetezi wa wapiganaji wa Gaddafi. Kusika siku ya Jumamosi jioni kuamkia Jumapili waasi walikuwa kilomita chache kutoka Viwanja vya Kijani ambapo wiki kadha wa kadha mashabiki wa Gaddafi walikuwa wakikutana kutiana shime.

Maelfu ya wananchi wa Libya wakipepea bendera ya waasi – ambayo ni bendera ya zamani ya Mfalme wa Libya – walianza kujitokeza barabarani kuwapokea waasi hao na usiku wa kuamkia Jumatatu hii maelfu zaidi wamejitokeza katika mitaa na viunga vya Jiji la Tripoli kuwakaribisha waasi hao ambao wanapigana chini ya uongozi wa Baraza la Mpito la Libya ambalo linawakilisha serikali mbadala ya ile ya Gaddafi. Hadi hivi sasa nchi 32 zimetambua baraza hilo kuwa mwakilishi halali wa wananchi wa Libya. Tanzania siyo mojawapo.

Kuanguka kwa jiji hilo kuliharakishwa usiku wa Jumamosi ambapo katika hali inayoonekana kupangwa mapema misikiti ya Jiji la Tripoli ilianza kurusha matangazo ya kuwataka wananchi wa Libya kujitokeza kupigana kumuondoa Gaddafi. Wito huo unasadikiwa kuwa ulikuwa ishara kwa vikosi vya waasi wa Libya ambavyo vilikuwa vimeshaingia jijini hapo na kujipanga na silaha na kujificha kusubiri muda muafaka. Vikosi hivyo vilibadilisha mwelekeo wa vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya kwani kabla majeshi ya Libya hayajua ni wapi pa kuwazuia waasi wasiingie Libya ilijikuta tayari ina waasi katikati yake.

Pamoja na jitihada za kukatisha tamaa wapiganaji na watu wengi kwa kuwahikikishia kuwa hali ni “shwari” uongozi wa Libya ulijikuta unazidiwa. Kufika Jumapili usiku watoto watatu wa kiume wa Kanali Gaddafi walikuwa wamekamatwa na kushikiliwa mikononi na vikosi vya waasi hao.

Miongoni mwa watoto hao ni pamoja na ambaye alionekana kama msemaji mkuu wa familia Bw. Seif Gaddafi pamoja na ndugu yake Al-Saad Gaddafi. Kukamatwa kwa vijana hao ambao hawakuweza kutoa upinzani wowote kunaashiria tu kuwa walikuwa tayari kuona watu wengine wanapigania maisha yao huku wao wenyewe wakishindwa kunyanyua bunduki zao. Kukamatwa kwa watoto hao wa kiongozi huo kwaweza kuwa funzo kwa watoto wa marais wengine duniani ambao wamekuwa wakijiingiza katika utendaji kazi wa wazazi wao na kujijengea wingu la ujiko na utisho.

Mtiririko wa matukio yaliyochangia kuanguka kwa utawala wa Gaddafi tangu kuanza kwa kampeni hiyo uko hivi:

 Januari 14, 2011 – Rais wa Tunisia Ben Ali anang’olewa kufuatia maandamano ambayo yamejulikana kama Machipuo ya Waarabu na kuanzisha wimbi la maandamano katika nchi kadha wa kadha za Waarabu.

 Februari 11, 2011 – Rais Hosni Mubarak wa Misri naye analazimishwa kujiuzulu kufuatia maandamano na mgomo mkubwa wa wananchi kwenye viwanja wa Tahrir jijini Cairo.

 Februari 15, 2011 – Wananchi wa jiji la Benghazi Mashariki ya Libya waanza maandamano ya kumpinga Gaddafi. Muda si mrefu baadaye uasi wa kijeshi unaanza na jiji la Bengazi linaangukia mikononi mwa waasi kwa urahisi, Mji wa Mistrata nao waangukia mikononi mwa waasi muda si mrefu baadaye.

 Machi 15, 2011 – Vikosi vya serikali ya Libya vinafanikiwa kurudisha nyuma vikosi vya waasi na kukomboa miji karibu yote isipokuwa Mistrata na Benghazi.

 Machi 17, 2011 – Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatoa ruhusa kwa nchi wanachama kutoa msaada kuzuia mauaji ya wananchi pamoja na kuzuia ndege za Libya kuruka. “Ukanda wa Kutokuruka Ndege” watangazwa juu ya nchi ya Libya. UM unaagiza kuwa “njia zozote” zitumike kuhakikisha azimio hilo la UM linatekelezwa.

 Machi 30, 2011 – Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Libya Bw. Musa Kusa anaenda Uingereza na huko anaomba hifadhi ya kisiasa na kukataa kuwa mwakilishi wa Gaddafi.

 Aprili 14, 2011 – Viongozi wa mataifa ya Magharibi Barack Obama, David Cameron na Nicolas Sarkozy wanasema wazi “Gaddafi lazima aondoke, aondoke moja kwa moja”.

 Aprili 19, 2011 – Baada ya waasi kufanya vibaya katika kampeni yao ya kwanza kuelekea Tripoli, maafisa wa Kijeshi toka Uingereza wanaingia Bengazi na kutoa ushauri wa kijeshi kwa waasi.

 Mei 28, 2011 – Vikosi vya NATO vinashambulia makazi ya Gaddafi pamoja na makao makuu ya Kamandi yake ya Kijeshi. Gaddafi ananusurika.

 Juni 27, 2011 – Mahakama ya Kimataifa ya The Hague, yatoa hati za kuwakamata Gaddafi na watoto wake pamoja na viongozi wengine wa juu kwa mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu na makosa ya kivita.

 Julai 20, 2011 – Marekani yatambua rasmi Baraza la Mpito la Libya kuwa mwakilishi halali wa wananchi wa Libya.

 Julai 27, 2011 Uingereza yatambua rasmi Baraza la Taifa la Mpito kuwa ni serikali halali ya Libya.

 Julai 28, 2011 – Kamanda Mkuu wa vikosi vya waasi wa Libya Abdel Fattah Yunus anauawa katika mazingira yaliyojaa utata. Msaidizi wake ateuliwa kuongozi waasi.

 Agosti 15, 2011 – Waasi waanza kampeni kutoka pande zote kuelekea Tripoli. Miji ya Zawiya na Ghariyan yaangukia mikononi mwa waasi.

 Agosti 20, 2011 – Risasi zinaanza kusikika jiji la Tripoli baada ya vikosi vya waasi vilivyokuwa vimeshatangulia na kujificha (sleeper cells) vilipoanza kujitokeza.

 Agosti 21, 2011 – Waasi waingia katikati ya jiji la Tripoli, watoto wawili wa Gaddafi watekwa na mmoja (Mohammed) ajisalimisha mwenyewe.

Hata hivyo, kuanguka kwa Tripoli hakujakamilika hadi kijarida hiki kinatoka. Rais wa Libya haijulikani alipo japo kuna tetesi kuwa ametoka nchi lakini kuna uwezekano yeye naye anaweza kuangukia kwenye mikono ya waasi. Kuanguka kwa Tripoli hata hivyo hakumaanishi kuwa mgogoro wa kisiasa utakuwa umefikia kikomo. Kama kilichotokea Misri ni mfano, basi Libya inakazi kubwa ya kuanza kujenga taasisi za kiutawala.

Wakati huohuo Rais wa Syria Bw. Bashar Al Assad amehakikishia wananchi wake kuwa serikali yake haiko katika hatari ya kuanguka kufuatia maandamano ambayo kama yale ya Libya yalianzishwa na matukio ya Tunisia miezi karibu saba nyuma. Hata kama Gaddafi, Assad aliamua naye kuzima uasi kwa kutumia vikosi vya jeshi lakini pamoja na matumizi makali ya nguvu dhidi ya wananchi wake bado wananchi wa Syria wameendelea kujitokeza kupinga utawala wake.

Wananchi wa Libya wanasubiria kwa hamu kusikia hatima ya Kanali Gaddafi.

9 Comments
  • Nimesikitishwa sana na kimbelembele cha nchi za magharibi juu ya hali tete na mgogoro wa Libya kwa Ujumla. Swali, je nini hatima na uhuru wa Afrika juu ya ubepari na ukoloni hai wa nchi tajiri? Lini Waafrika watakaa, kupanga na kuamua mambo yao yenye tija na mstakabali wa nchi zao na maisha yao kwa ujumla? Mwenzako akinyolewa, zako tia maji!

    • @Chris ..Hiyo haiwezekani ,kama marais wetu hawawezi kutatua shida za nchi zao wataweza kukaa na kutatua ya bara zima ??

      Tusidanganyane, africa tutaendelea kutatuliwa shida zetu na nchi za magharibi mpaka tutakapoelewa kwamba ukiwa mdarakani si kutatua matatizo ya familia yako bali ya taifa lako

      • @ Julie jibu lako ulilompa Chris ni lenye hekma kubwa. Viobgozi wa nchi mbalimbali hususan Tanzania walitazame hilo.

  • Sifurahii anguko la Gadaff hasa kwa namna ama njia ilyotumika kwani imeangamiza maisha ya wasio na hatia ingawa siamini kama kweli mtawala huyo alistahili zawadi hiyo kwa mazuri aliyoyafanya katika nchi hiyo.

    • Kwa nini akae madarakani kwa miaka zaidi ya arobaini? Ina maana katika Libya nzima hakuna mtu mwingine anayeweza kuwa rais? Hapo demkrasia iko wapi?

  • Nampongeza simba wa Afrika Robert Mugabe kwa kumfukuza balozi wa Libya anaye jifanya kuwatambua waasi,nivizuri afukuzwe tena afunguliwe mashitaka kusifia uuwaji mkubwa wa waasi na NATO na mataifa ya magharibi yenye uchu na Afrika yetu nzuri na tajiri.
    Jamani kuanguaka kwa Ghaddafi ni tiketi ya Afrika kuridishwa utumwani pitia ukoloni mamboleo,ambao Nkwame Nkuruma&Nyerere7Ghaddafi&Mugabe waliweza kuupinga na kuto usaidia kwa moyo mmoja.
    Ghaddafi yeye hanashida ametaka saidia watu watu wamekataa kwA ujinga na tamaa zao. lAKINI wenye shida ni hao walio msaliti Simba wa Afrika. basi wacha wa ng’atwe na wazungu wanyonyaji mabepari,tutaona mwisho wa hiyo libya huria.
    Afrika tunaizd didimia na hao mashushushu viongozi wa AU niwaafrika wazungu.
    Mzungu alituletea dini na kutupeleka utumwani na kutupora na kubaka na kutesa ngugu zetu eti leo ni mhisani?Hata hapo hatujifunzi na historia cc tu wajinga japo c wote.Mapinduzi yapo tu na yanaendelea.

  • Hata kama alifanya mengi mazuri kwa watu wake kwa nini ashikilie madaraka zaidi ya miaka arobaini? Ina maana katika nchi nzima ya Libya hakuna mtu mwingine anayeweza kuwa rais? Hapo demokrasia iko wapi?

  • Chenye mwanzo hakikosi mwisho kutolewa kwa Ghadaf madarakani kuwe na manufaa kwa walibya na si kwa watu wachache kwani ndani ya utawala wa Ghadaf wananchi walinufaika kutokana huduma mbalimbali za kijamii

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *