Katibu Mwenezi wa Taifa wa Chama cha Mapinduzi Bw. Nape Nnauye ametajwa kama mlengwa wa waraka wa siri ambao unakituhumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa mpango wake wa kupinga posho za vikao za wabunge na watumishi wengine una malengo yenye maslahi ya kifedha.
Waraka huo ambao Fikra Pevu imeuona umeficha jina la mwandishi wake lakini imejaa alama mbalimbali kuonesha kuwa umetungwa na mmoja wa makada maarufu wa CCM au shabiki wa CCM mwenye lengo la kupunguza makali ya hoja za Chadem haijawezekana kuuthibitisha kama ni wa kweli au wa kufoji kwa ajili ya propaganda. Kinyume na baadhi ya vyombo vya habari vilivyoripoti kuwa Nape anatuhumiwa kuwa mwandishi wa waraka, waraka huo Fikra Pevu imedokezwa umeandikwa na kada mmoja mashuhuri wa CCM ukielekezwa kwa Nape Nnauye.
Waraka huo unafunua kwa kiasi msingi wa madai ambayo yalitolewa na baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali ambao walidai kuwa maandamano ya Chadema ambayo yamekuwa yakifanyika mara kwa mara yamefadhiliwa na wafadhili ili kuleta vurugu nchini. Mapema mwezi wa tatu Waziri wa Maendeleo ya Wanawake na Watoto Bi. Sofia Simba alikuwa Waziri wa kwanza wa serikali ya Kikwete kudai hadharani kuwa Chadema kilikuwa kinapokea fedha kutoka nje ya nchi. Akizungumza na Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) Bi. Simba alidai kuwa Chadema kinafadhiliwa kutoka na nchi za Ulaya.
Madai hayo yalirudiwa pia na mmoja wa mawaziri waandamizi wa serikali ya awamu hii ya nne Bw. Bernard Membe ambaye naye alinukuliwa kukituhumu mojawapo ya vyama vya siasa (bila kukitaja jina) kuwa kinafadhiliwa na mataifa ya nje. Hata hivyo kauli hiyo ilipewa changamoto na baadhi ya mabalozi kitu kilichomfanya Membe (kupitia Wizara yake) kutoa tamko kuwa alichokisema kilinukuliwa vibaya. Matamshi ya Membe na Simba yalilazimisha CHADEMA kutaka viongozi hao kutaja nchi hizo au wafadhili hao kitu ambacho hakijafanywa hadi hivi sasa licha ya kuwa vyombo vyote vya intelligensia na usalama vinasimamia na serikali ya chama chao.
Waraka huo umedai kuwa kulikuwa na vikao mbalimbali kabla na baada ya uchaguzi juu ya kufadhili Chama cha Demokrasia na Maendeleo, “Kuna kikao kilifanyika mara baada ya uchaguzi au kabla ya kuapishwa Rais JK pale Novemba 6, 2010 jijini Nairobi!” umedai waraka huo bila kuelezea ni kina nani waliohudhuria kikao hicho kwani tangu baada ya uchaguzi hadi kuapishwa kwa Rais Kikwete viongozi wa juu wa Chadema aidha walikuwa kwenye majimbo yao kujaribu kuzuia uchakachuaji wa kura au walikuwa Dar-es-Salaam.
Waraka huo ukaendelea hapo hapo na kudai kuwa “Katika kikao hiki ndipo Uongozi wa juu wa Chadema ulikabidhiwa jumla ya Shilingi Bilioni 3.7 za Kitanzania, kimchanganuo : takriban theluthi 2 za fedha zilitoka kutoka Wafadhili wa ndani ya Tanzania na theluthi moja ilichangwa na taasisi mashuhuri ya kidini duniani pamoja na Wapenzi wa Chadema waishio nchi za nje!”. Kama ilivyokuwa katika kushindwa kutaja jina la nchi wafadhili au mataifa wafadhili waraka huo umeshindwa pia kutaja “taasisi mashuhuri ya kidini duniani” japo katika mwendelezo wa ajenda ya udini ni wazi kuwa kinachoashiriwa ni Kanisa Katoliki kwani katika uchaguzi uliopita lilituhumiwa na baadhi ya wanasiasa na mashabiki wa wanasiasa hao kupendelea CHADEMA. Waraka umeshindwa kusema fedha hizo zilizotolewa na taasisi hiyo “mashuhuri” ya kidini zilitolewa na kiongozi gani.
Waraka huo ambao unaonekana kuandikwa kiufundi kwa kutumia lugha ya kushawishi lakini ukiwa na makosa ya kimantiki na kihoja ulikejelewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Dr. Willibrod Slaa alipozungumza na waandishi wa habari juzi. Kiini cha madai ya waraka huo ni kuwa Chama cha Demokrasia kilipewa shilingi bilioni 3.7 na “wafadhili” hao huko Kenya, hata hivyo waraka hausomi kama hizo zilikuwa ni fedha taslimu, hundi, au ahadi. “Fedha hizi zilikabidhiwa Uongozi wa Chadema jijini Nairobi na zimeingizwa nchini kama fedha za ufadhili wa kampeni na shughuli za kisiasa” umesema waraka huko na katika kuonesha kutokuwa na ufahamu au hata uhakika wa kile inachodai ukaendelea kusema kuwa “Huenda zimehifadhiwa katika akaunti tofauti zozote binafsi maalum katika benki za hapa nchini”. Waraka umedai pia kuwa “kimchanganuo : takriban theluthi 2 za fedha zilitoka kutoka Wafadhili wa ndani ya Tanzania na theluthi moja ilichangwa na taasisi mashuhuri ya kidini duniani pamoja na Wapenzi wa Chadema waishio nchi za nje!”
Hata hivyo waraka huo wenye kurasa tatu umedai kuwa lengo hasa la fedha hizo lilikuwa kuwalipa mishahara wabunge wa Chadema endapo wangefungiwa na Bunge baada ya tukio la kutoka kwenye ukumbi wa bunge kupinga hotuba ya Rais Kikwete baada ya uchaguzi kwenye kikao cha Novemba 18, 2010. “Huenda zimehifadhiwa katika akaunti tofauti zozote binafsi maalum katika benki za hapa nchini” umedai waraka huo.
Katika kuashiria ajenda ya ukabila haijifichi waraka huo umejaribu kutengeneza mgogoro baina ya viongozi wa chama hicho kwa kudai kwamba mpango wa fedha hizo ulikuwa ukijulikana na watu wachache. Haishangazi kuwa waraka unadai kwamba “ni asilimia 60 ya Wabunge walijua kuna fedha za wafadhili kuwakimu endapo kibano kitawafika hata hivyo lakini ukweli ni viongozi wajuu wanne tu wa Chadema ndio walijua kuwepo kwa fedha hizo na wafadhili wake.” Waraka unawataja viongozi hao kuwa “Mwenyekiti wa Chadema Taifa Freeman Mbowe Mwenyekiti Muasisi wa Chadema Mzee Edwin Mtei, Mbunge wa Chadema Moshi Mjini Philemon Ndesamburo na Katibu Mkuu wa Chadema Dkt Wilbrod Slaa.” Viongozi wote hao wanne wanatoka maeneo ya Kaskazini mwa Tanzania huku watatu kati yao wakiwa ni Wachagga.
Waraka umeonesha kujichanganya kidogo na hivyo kupoteza kuaminiwa kwake kwa kudai kuwa “Masharti ya fedha hizi ni kutumika katika hatua na harakati zozote za kuitia misukosuko, na ikiwezekana kuidhalilisha Serikali ya awamu ya 4 mbele ya Watanzania na jumuiya ya Kimataifa.” Masharti haya yanaonekana ni kinyume na madai ya awali kwenye waraka huo kwamba fedha hizo kama zilikuwepo kweli zilikuwa kwa ajili ya kuwalipa mishahara wabunge wa CHADEMA endapo wangefukuzwa na Bunge. Waraka hausemi masharti hayo mapya yalitolewa lini, wapi na nani.
Katika kuonesha kujua waliofanya ufadhili huo waraka huo umedai kuwa “Hawa Wafadhili ambao baadhi yao ni wale watuhumiwa wa Ufisadi ndani ya CCM wamekuwa wanawaendesha puta Viongozi wa Kitaifa wa Chadema!” Kwa maneno mengine waraka huo umedai kuwa baadhi ya wana CCM ndio wanafadhili upinzani bila kugundua kuwa kwa kufanya hivyo wanatuhumu usaliti ndani ya Chama cha Mapinduzi na kukiri kushindwa kuukabili usaliti huo na kukionesha CCM katika mwanga wa udhaifu zaidi. Waraka unamtaja mmoja wa watu wanaodaiwa kufadhili mpango huo kuwa ni gazeti moja lilimtaja “kiongozi Mstaafu wa ngazi ya juu katika awamu zilizopita kuwa yumo katika orodha ya Mafisadi wapya, kwa Mastaajabu makubwa Katibu Mkuu wa Chadema Dk Slaa alijitokeza hadharani na kukanusha kuwa hakumtaja kiongozi huyo! Hii si hulka ya Dk Slaa siku zote akisoma tuhuma hadharani inakuwa imetoka na hutoa rai kwa muhusika kuwa kama anahisi ameonewa aende mahakamani lakini kwa huyu Kiongozi kwa vile wanamuelewa ni mmoja wa wafadhili wao, Dk Slaa bila ya kimeme alitoa kauli ya kukanusha haraka haraka kuwa yeye katika mkutano wa kutangaza watuhumiwa wapya wa ufisadi hakumtaja!”
Kumbukumbu zote zinaonesha kuwa kiongozi pekee mwenye kutimiza sifa ya tukio hilo ni Waziri Mkuu Mstaafu na mwanachama wa muda mrefu wa CCM Bw. Fredrick Tsumaye. Hata hivyo katika maelezo yake juzi kwa waandishi wa habari Dr. Slaa amesema kuwa “Lakini Sumaye hayuko katika ufisadi mkubwa huu tunaouzungumzia unaolitafuna taifa. Kama mtu ana vielelezo vya ufisadi wake, ambavyo sijui, atuletee. Sisi tunapozungumzia ufisadi mkubwa hatumwoni Sumaye miongoni mwao, lakini haina maana kwamba tunalinda mafisadi.” Dr. Slaa alikumbushia kuwa ni yeye ndiye aliyemtuhumu Sumaye Bungeni kuhusu kashfa ya shamba la kule Kibaigwa, Morogoro. Ilikuwa ni mwaka 2004 kwenye kikao cha Bajeti Bungeni ambapo Dr. Slaa alimtuhumu Sumaye kuwa alimiliki shamba pasipo halali na kumtaka ajiuzulu hivyo hata madai ya ushirikiano wa watu hawa wawili sasa hivi ni magumu kuyaona kama waraka unavyodai.
Waraka huo umeenda mbele zaidi na kudai kuwa fedha hizo ambazo Chadema “walipatiwa” bado zipo na hazijatumika kiasi cha kutosha. “hizi fedha hata theluthi moja hazijatumika bado zimebaki nyingi zaidi ya theluthi 2 na ushei na kwa vile watuhumiwa wa ufisadi wameungana na Chadema zimeshatumbukizwa fedha za kutosha kuwalipa posho Wabunge wa Chadema wakati watakapo amua kugomea kuchukua posho ya Bajeti rasmi ya Serikali!” Kwa maneno mengine waraka umetoa sababu ya tatu ya hizo fedha kuwa ni kulipa posho za vikao zile ambacho CHADEMA wametaka ziondolewe kwa Wabunge. “kinyemela Wabunge wa Chadema watakuwa wanapokea posho zile zile kutoka mfuko huu wa kifisadi ! Kwa hiyo tishio la Wabunge kugomea posho zao binafsi za vikao vya bajeti ni kweli na linatekelezeka bila ya maumivu yeyote”
Waraka huo hata hivyo unaionesha serikali katika mwanga mbaya hasa kufuatia kashfa za uingizaji na utoroshwaji wa fedha nchini katika sakata la EPA na MEREMETA kuwa haijajifunza wala kuwa na uwezo wa kusimamia fedha haramu nchini au hata kujua ni kiasi gani kinaingia na kutoka. Waraka huo unasema “Kinachotakiwa ili wananchi wasihadiwe na uzalendo bandia na wakati huohuo kudhalilishwa Serikali na Bunge ni kuwashushua mara moja , kwa kueleza kuwepo mfuko wa fedha za kifisadi ulioanza kwa mtaji wa Bilioni 3.7 na hatujui huenda sasa ni zaidi bilioni 10 au zaidi”. Kitu kinachoshangaza hata hivyo katika waraka mzima ambao Fikra Pevu imeupitia kwa makini ni kushindwa hata mara moja kujaribu kuvihusisha vyombo vya usalama au vya usimamizi wa sheria katika kuwaumbua Chadema hasa kwa kukamata, na kuzuia fedha hizo ambazo kama ni kweli zitakuwa zinavunja sheria ya uchaguzi ya 2010 pamoja na Sheria ya kuzuia Fedha haramu nchini.
Hata hivyo, waraka huo unaonekana hasa kujaribu kuzuia kuvuja damu kwa CCM hasa kwenye sakata la posho ambapo ukimya wa Rais Kikwete na utetezi wa viongozi wa CCM umewafanya waonekane kwa mwanga mbaya. Waraka huo unaakisi hisia za baadhi ya wana CCM kuwa hoja ya posho kama ambavyo imekuwa ikisukumwa na Chadema ambao wamekuwa wakitekeleza walichoahidi katika ilani yao kunafanya serikali ya Kikwete ionekane vibaya. “sasa inaelekea baada ya kuona Serikali haikukana mpango wake wa kuondokana na kulipa posho zisizo za lazima Chadema wanakuja na siasa za uchonganishi na hivyo kuliingiza jina la JK katika malumbano na hili bila ya shaka linatokana na kuhakikisha uchonganishi wa ukoleze na baadae watoe hukumu kuwa midhali JK hatotoa waraka wa kufuta posho mara moja basi anaunga mkono ‘ufisadi’” unasema waraka huo.
Hofu ya mwandishi wa waraka huo inadhihirika kuhusiana na Rais Kikwete kushindwa kuchukua msimamo kwenye suala la posho kwa kusema kuwa “Hawa jamaa wakiongozwa na Kinara wao wanakuwa na vikao vya mara kwa mara bila ya shaka kurejea jinsi ‘media’ na hisia za Wananchi zilivyo kuhusu kadhia hii ya posho! Hawa ‘plotters’ wanajua JK akifuta posho Wabunge wote watakosana naye na wakati huohuo Chadema watakuwa wamepanda chati nchini.! Wanajua jambo wanalomtaka JK alifanye haliwezekani na kama kawaida wataendelea na ajenda yao ya maandamano kuhakikisha Tanzania haitawaliki!”
Waraka huo katika kuelekea hitimisho lake umeonekana kutuhumu taasisi za usalama wa taifa kuwa yumkini zina watu ambao ni mawakala wa Chadema au mafisadi na wamekuwa wakipenyesha taarifa nyeti mbalimbali kwenda kwa wapinzani. “kwa uhakika kabisa ‘Mafisadi’ na kinara wao wana mtandao ambao unapata taarifa nyeti sambamba anazopata JK na kwa uhakika wana ushawishi mkubwa ndani ya ‘System’ ya kuhakikisha JK hapati habari ambazo zitawakaanga au zitamfanya JK mambo yake yawe mazuri!” umedai waraka huo huku ikidai kuwa ni taarifa hizo ndizo zimewezesha CHADEMA kuanzisha “tafrani hii”
Maelekezo ya waraka huo ni kumtaka Nape ambaye ni Katibu Mwenezi kutumia muda wake kuwaeleza wananchi juu ya ukweli wa uwepo wa fedha hizi na kuwa awe tayari kukana kujua chanzo cha waraka huo. “Lazima wananchi waelezwe kinaga ubaga zile posho wanaolipwa kwa kushiriki maandano zinatoka katika mfuko wa ‘Mafisadi’ na kwamba wanachezwa shere tu na Viongozi wa Kitaifa hasa Mbowe na Slaa” waraka umetoa wito. Pamoja na kuwataja viongozi wengine wa Chadema waraka huo umemtilia shaka Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara) Bw. Zitto Kabwe kuwa “inasikitisha Zitto anatumika bila ya kujua (labda awe naye kwa sasa tayari Mafisadi wameshamteka.)” Waraka unawasiwasi kuwa endapo suala la posho zitagomewa na wabunge wa Chadema basi “itakuwa imehalalisha matumizi ya fedha hizo!”
Katika hitimisho lake waraka huo umemtaka Nape kutowahusisha watu wowote na taarifa hizo na asimwamini mtu yeyote iwe wa upinzani au CCM au mkongwe na hivyo kufanya hali ya kisiasa nchini ionekane ya kutokuaminiana kupita kiasi hasa ndani ya CCM. “Asije mtu akajichekesha awe wa Chadema au CCM ngazi ya juu akataka umwambie source yako abadan! Mtu ambaye unaweza ku-confide ni JK tu ikiwa ni lazima!)” umemalizia waraka huo.
Na. Mwandishi Wetu