Miaka 50 ya uhuru Mwanza: RC awataka wananchi waendelee kuwa wavumilivu

Jamii Africa

nembo-miaka-50MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Evarist Ndikilo, amewataka wakazi wa mkoa huu waendelee kuwa wavumilivu; na hasa katika kipindi hiki ambacho licha ya kutimiza miaka 50  ya uhuru, alikiri kuwa bado WanaMwanza wanaendelea kukabiliwa na matatizo kadhaa  kimaisha na kisiasa .

Ndikilo alitoa rai hiyo Jijini hapa leo Desemba 9, kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Said Amanzi wakati akihutubia wananchi kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru.

“Taifa halijengwi mara moja, wala matatizo ya kimaisha hayamalizwi kwa kufumba na kufumbua. Matatizo yanayotukabili hivi sasa ni ya mpito. Wanamwanza tuunganishe nguvu kama Taifa tuone ni namna gani tutayakabili” alisema Ndikilo kupitia hotuba yake.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema suluhisho la mtatizo siyo wananchi kuleta fujo ama kutoelewana wao kwa wao, isipokuwa kwa kukaa pamoja na viongozi ama watendaji wa serikali kwa ajili ya kutafuta njia salama za kukabiliana nayo.

Kwa mujibu wa Ndikilo, mwananchi anayediriki kufanya hivyo anavunja sheria za sheria za nchi.

Aliyataja baadhi ya matatizo hayo kuwa ni uhaba wa walimu na vifaa vya kufundishia  na kujifunzia katika shule za msingi na sekondari pamoja na upungufu wa dawa za binadamu katika  zahanati, vituo vya afya na hospitali za serikali .

Ndikilo alilitaja tatizo jingine kuwa kuwepo kwa demokrasia changa ya mfumo wa vyama vingi vya sisasa ambapo baadhi ya wanasiasa wamediriki kupotosha ukweli kuhusu mchakato na uundwaji wa Katiba mpya.

“Toka mwaka 1992 nchi yetu imeingia katika demokrasia ya vyama vingi. Ni demokrasia changa sana. Tuutumie vizuri mfumo huu ili utuharakishie maendeleo ya nchi yetu” alisema.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa alisema mkoa wa Mwanza umepiga hatua mbalimbali za kimaendeleo tangu Taifa lipate uhuru.

“Miaka 50 iliyopita mkoa wa Mwanza haukuwa hivi: nyumba za bati zilikuwa za kuhesabu. Mkoa  mzima ulikuwa na kilomita 8.81 za barabara la lami; leo tunazo kilomita 424.14” alisema  na kuongeza kwamba

“Barabara za changarawe zilikuwa kilomita 125 tu, na leo tunazo kilomita 2593.42. Leo tunaweza kuwafikishia wananchi majisafi na salama kwa asilimia 64”

Alisema mwaka 1961, mkoa  wa Mwanza ulikuwa na vyanzo 50 tu vya maji inkilinganishwa na sasa ambapo kuna jumla ya vyanzo 3,326.

Aliendelea kufafanua hadi Desemba 9 mwaka 1961, mkoa wa Mwanza ulikuwa na sekondari nne pekee, ambazo hata hivyo hazikuwa za serikali.

Alizitaja shule hizo huku miaka wa kufunguliwa kwake ikiwa kwenye mabano kuwa ni Bwiru wavulana (1920), Bwiru wasichana(1952), Nsumba (1953) na Chopra (1959).

Katika hatua nyingine, Ndikilo alipuuza wanaobeza sekondari za Kata kwamba hazina maana kuanzishwa.

Alisema “Wapo wenzetu wanaozibeza shule hizi, ukweli unabaki palepale kuwa ni shule na zinaendelea kuboreshwa tena zipo zinazofanya vizuri sana; mfano, wa hivi karibuni pale Bungeni watoto sita miongoni mwa kumi waliofanya vizuri kitaifa walitoka shule hizi hizi”

Aliwataka wananchi wasiendelee kujenga shule za Kata, badala yake waziboreshe zilizopoa na kisha wajenge za kidato cha tano na sita.

Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru kimkoa yalifanyika kwenye uwanja wa Nyamagana, wilaya ya Nyamagana Jijini hapa na kuhudhuriwa na wananchi pamoja na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na serikali.

Habari hii imeandikwa na Juma Ng’oko, Mwanza

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *