Katavi: Vyeti feki vyaathiri huduma Duka la MSD. Watumishi watatu wakumbwa na fagio

Jamii Africa

NDOTO za wananchi wa Manispaa ya Mpanda na Mkoa wa Katavi kwa ujumla za Jumanne ya Januari 17, 2017 kuhusu kutatuliwa kwa changamoto ya upatikanaji wa dawa zimeyeyuka baada ya wafamasia watatu wa duka la serikali linalomilikiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kukumbwa na operesheni ya vyeti feki.

Wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipozindua duka hilo Januari 17, 2017 kulikuwa na matumaini makubwa kwamba walau kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa dawa ingeweza kupatiwa ufumbuzi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (katikati), akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Duka la Dawa la Bohari ya Dawa (MSD), Mpanda mkoani Katavi.

Hata hivyo, FikraPevu inafahamu kwamba, licha ya duka hilo kutofanya kazi kwa saa 24 tangu kufunguliwa, lakini kuondoka kwa watumishi hao watatu kumeongeza ukubwa wa tatizo.

“Duka limekuwa likifungwa usiku kutokana na uhaba wa watumishi, wagonjwa wanapata shida kutafuta dawa na sasa hili la operesheni ya vyeti feki ndilo limeongeza ugumu,” walisema baadhi ya wagonjwa waliokutwa hospitalini hapo.

Aidha, wananchi mbalimbali wanalalamika kwamba, licha ya kuwepo kwa duka hilo, lakini vifaa tiba na dawa muhimu zimekuwa zikikosekana, hali inayowalazimu kutafuta huduma katika sehemu nyingine za binafsi, jambo ambalo wanasema limekuwa likiwaathiri kwani gharama katika maduka ya binafsi ni kubwa kuliko kwenye duka hilo la serikali.

FikraPevu inatambua kwamba, Serikali ya Awamu ya Tano kwa nia njema kabisa, inaendelea na ukaguzi na ufuatiliaji wa vyeti vya kitaaluma kwa wafanyakazi wake kwenye sekta mbalimbali, ikiwemo pia sekta nyeti ya afya.

“Hii ni hospitali kubwa mkoani Katavi; ndiyo kimbilio letu na haistahili kukosa dawa na vifaa tiba hata vile vya msingi kabisa, lakini bahati mbaya hata bada ya kuwapo kwa dula la MSD, bado tunalazimika kununua dawa kwa wafanyabiashara,” anasema Said Juma, Mkazi wa Kawajense mjini hapa.

Juma ameiambia FikraPevu kuwa, Duka la MSD lina matatizo yale yale yaliyopo hospitalini hapo, kwani halina dawa muhimu kwa magonjwa ya kawaida kabisa kwa wakazi wa Mpanda na mkoani Katavi kwa ujumla.

Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkurugenzi wa MSD, Laurean Bwanakunu wakati wa uzinduzi wa Duka la Dawa Mkoani Katavi.

“Shida inakuwa kubwa zaidi nyakati za usiku kwani maduka mengi ya dawa huwa yamefungwa. Kimbilio letu huwa ni duka la dawa la Mkasu lililo jirani na hospitali. Hapo kila alfajiri utakuta watu walikuwa wakihitaji huduma tangu usiku wa manane, wakisubiri lifunguliwe,” anasema na kuongeza kuwa aghalabu nalo huwa halina baadhi ya dawa walizoandikiwa wagonjwa wengi.

Kukosekana kwa dawa jirani na hospitali, kwa upande mwingine, ni neema kwa waendesha bodaboda wenye kijiwe karibu na Hospitali ya Mkoa na mmoja wao anasema:

“Watu wengi huwa na haraka ya kununua dawa mbali na hospitali, maeneo ya mjini. Hawa lazima wakodi bodaboda. Hii ndiyo huduma yetu kwa wananchi na kwetu sisi ni kazi pia.”

 

Alichosema Waziri Mkuu

FikraPevu inafahamu kwamba, wakati wa uzinduzi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema kwamba, duka hilo lingeweza kumaliza matatizo ya upungufu wa dawa katika hospitali hiyo na kuleta unafuu kwa wananchi ambao wamekuwa na kero hiyo kwa miaka mingi.

“Duka hili litamaliza tatizo la upungufu wa dawa katika hospitali hii, vituo vya afya na zahanati za Mkoa wa Katavi. Serikali ina mikakati ya kufungua maduka ya dawa kupitia MSD kwenye kila mkoa hapa nchini ili kuondoa tatizo la vifaa tiba na dawa na kuwapunguzia wananchi gharama za matibabu,” alisema Majaliwa.

Wananchi waliohudhuria hafla hiyo waliifurahia hatua hiyo kutokana na ukweli kwamba mbali na uhaba wa dawa na vifaa tiba kwa mikoa iliyopo pembezoni mwa Tanzania, Katavi ikiwa mmojawapo, tatizo jingine ni ukubwa wa bei za dawa.

“Hili duka la serikali litatuuzia dawa kwa bei tunayoimudu wengi tofauti na maduka ya wafanyabiashara wengine,” alisikika akisema kwa matumaini makubwa mmoja wa wananchi waliokuwapo siku hiyo.

Wakati wa uzinduzi huo, iliahidiwa kuwa lingefanya kazi saa 24 likiwahudumia wakazi wa Mpanda na maeneo mengine mkoani humo.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurent Bwanakunu, alisema wakati wa uzinduzi huo kwamba, lengo la kufungua maduka katika mikoa saba nchini ni kusogeza huduma karibu na wananchi waweze kupata dawa bora na kwa bei nafuu, lakini inaonekana ahadi hizo hazijaweza kutimia.

FikraPevu inatambua kwamba, sekta hiyo muhimu katika maendeleo ya taifa, kwa miaka mingi imekuwa ikikumbana na changamoto kadhaa karibu kila kona ya Tanzania, kubwa ikiwa ni upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *