JANUARI 3, 2017 majira ya saa 3:00 usiku katika Kitongoji cha Songambele, Kijiji cha Mumba, Kata ya Masoko katika Wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya, wakati wananchi wengine wakiwa wameanza kupitiwa na usingizi, kundi la watu watano lilikuwa makaburini.
Hawakuwa wakizika maiti, bali walikuwa na kazi kubwa ya kuchimbua kaburi alimozikwa Bi. Sisala Simwali, dada aliyekuwa na ulemavu wa ngozi (albino).
FikraPevu inafahamu kwamba, marehemu Sisala alifariki dunia Februari 28, 2008 baada ya kuugua na kuzikwa Februari 29, 2008 katika makaburi ya familia.
Mtuhumiwa mmoja aliyeuawa na wananchi wenye hasira baada ya kukutwa akichimbua kaburi la marehemu Sisala Simwali huko Mbeya.
Kishindo cha kuchimbua kaburi kikawaamsha wananchi, ambao licha ya kupiga simu polisi katika Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi, walianza kupambana na watu hao na wakafanikiwa kuwakamata wawili huku mmoja akiuawa na wananchi wenye hasira na wengine kukimbia.
Lengo la watu hao, kwa mujibu wa mahojiano ya awali kati ya polisi na watuhumiwa, lilikuwa kupata mifupa ya albino ambayo walikuwa wameelekezwa na mganga wa jadi kwamba wakiipeleka basi watatengenezewa dawa ya utajiri.
FikraPevu inatambua kwamba, tukio hilo ndilo la kwanza kwa mwaka 2017 likihusisha matukio ya albino ambayo kwa miaka kadhaa sasa yametamalaki nchini Tanzania na kuwafanya watu wenye albinism kuishi kwa mashaka katika nchi yao wenyewe.
Na linaleta hofu kubwa kwa jamii kuona kwamba badala ya kuwateka, kuwakata viungo na hata kuwaua albino, sasa majahili wameanza kuyasaka makaburi walimozikwa albino na kuyafukua ili wachukue mifupa na kupeleka kwa waganga kwa imani za kishirikina.
FikraPevu inajua kuwa, mpaka sasa mtoto Pendo Emmanuel Nundi (6) wa Kijiji cha Ndamhi wilayani Kwimba mkoani Mwanza hajapatikana tangu alipotekwa nyara Desemba 27, 2014.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, CP Valentino Longino Mlowola, akionyesha picha ya mtoto Pendo Emmanuel ambaye mpaka sasa hajapatikana.
Mauaji kila mahali
Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, matukio ya kushambuliwa, kutekwa na kuuawa kwa albino kwa sasa yametamalaki nchini kote, ingawa zamani yalikuwa yakiripotiwa zaidi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Itakumbukwa kwamba, tangu Januari 31, 2017 mpaka sasa, Said Abdallah (47) mwenye ualbino, mkazi wa Kijiji cha Mbezi Mlungwana wilayani Mkuranga katika Mkoa wa Pwani, hajapatikana tangu alipotoweka katika mazingira ya kutatanisha.
Taarifa za uchunguzi zilieleza kwamba, mara ya mwisho kabla hajatoweka, Abdallah aliwaaga wenzake anaoishi nao kuwa anakwenda kuuza mboga za majani katika Kijiji cha Mtipule ambacho kipo kati ya Kijiji cha Nyakenge na Kitongoji cha Kaloleni ambapo ilielezwa kuwa siku hiyo alionekana katika kilabu inayouza pombe za kienyeji huko Mkuranga.
Ikaelezwa pia kwamba, siku hiyo ya Janauri 31, 2017 Abdallah aligombana na wenzake aliokuwa akinywa nao pombe majira ya saa 1:30 usiku na kisha aliondoka kilabuni hapo na kuelekea kusikojulikana. Hajapatikana mpaka leo.
FikraPevu inafahamu kuwa, ndugu wa Abdallah waliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Kimanzichana, Mkuranga na kupewa RB namba KIM/RB/50/2016 na kama hiyo haitoshi pia waliamua kupeleka taarifa katika Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Mkuranga na kupewa RB namba MKU/PE/05/2016.
Mpaka sasa hakuna taarifa zozote zilizotolewa hadharani kuhisiana na kutoweka kwa Abdallah, na kama zipo za siri pengine Polisi ndio wanaojua zaidi.
Matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino yanapnekana kurudi kwa kasi kubwa baada ya kudhibitiwa, kwani wakati Abdallah hajulikani aliko mpaka sasa, tukio jingine la kutekwa nyara mtoto mdogo wa kiume mwenye ualbino, Tito Nkuryu (3) huko Itilima mkoani Simiyu lilitokea usiku wa kuamkia Februari Mosi, kabla ya mtoto huyo kuokolewa na kupelekwa kituo cha kulelea watoto, Lamadi.
Watu Wawili Wakamatwa Na Mifupa Ya Albino, Walikuwa Wanaenda FikraPevu inafahamu pia kwamba, Aprili 29, 2017 watu wawili walikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Kagera wakiwa na viungo mbalimbali vya mwili ikiwemo mifupa mitatu inayodhaniwa kuwa ya mtu mwenye ualbino.
Mifupa iliyokamatwa Muleba ambayo inadhaniwa kwamba ni ya marehemu Zeulia ambaye alikuwa na ualbino.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, ACPHenry Mwaibambe, alinukuliwa akisema kuwa tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Kyota, Kata ya Kimwani wilayani Muleba baada ya jeshi hilo kuweka mtego kwa watuhumiwa hao ambao walikuwa wanatafuta wateja wa viungo hivyo.
Watuhumiwa waliotiwa mbaroni ni James Rutozi (66) mkazi wa Kimwani ambaye ndiye aliyekuwa anahifadhi viungo hivyo na Emanueli Kaloli (50) ambaye pia ni mkazi wa Kimwani aliyekuwa anatafuta mteja wa viungo hivyo.
Kama ilivyotokea kule Mbeya, watuhumiwa waliokamatwa huko Muleba walifukua kaburi la marehemu Zeulia Jestus aliyekuwa na ualbino ambaye alifariki mwaka 2006 na kuzikwa katika Kijiji cha Rushwa, Kata ya Mushabago wilayani Muleba.
Taarifa ambazo FikraPevu inazo zinaeleza kwamba, marehemu Zeulia ambaye wakati huo alikuwa na miaka 24, alifariki dunia muda mfupi baada ya kujifungua na ndipo watuhumiwa hao walifukua kaburi hilo mwaka 2008 kwa maelekezo ya mganga wa jadi.
Jeshi la Polisi mkoani Kagera, baada ya kuomba kibali mahakamani, lilikwenda kufukua kaburi hilo Machi 23, 2017 na kugundua kuwa viungo hivyo walivyokamatwa navyo watuhumiwa vimetolewa katika mwili wa marehemu huyo.
Uchunguzi wa FikraPevu unaonyesha kwamba, tatizo la usalama wa albino nchini Tanzania ni sugu na limeibuka tena baada ya kupoa kwa muda na sasa linatishia hata usalama wa nchi.
Siku tatu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015, Mohammed Said (35), mkazi wa Mkuranga, alivamiwa na watu wasiojulikana na kushambuliwa kwa kumkata panga kichwani.
Operesheni nyingi
Hali ya kuongezeka kwa matukio hayo ndiyo inawafanya wananchi wahoji kwamba zile jitihada zilizoonyeshwa na Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya usalama kwa kipindi cha takriban miezi nane mwaka 2015 zimepotelea wapi?
Taarifa ambazo FikraPevu inazo zinaonyesha kwamba, serikali iliongeza kasi ya kuwasaka wauaji wa albino mara baada ya kutoweka kwa Pendo Emmanuel, kasi ambayo siyo tu ilifanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa wengi, lakini iliambatana na operesheni kabambe ya kuwasaka na kuwatia mbaroni waganga takriban 200 nchi nzima waliokuwa wakijihusisha kupiga ramli chonganishi.
FikraPevu inafahamu matukio takriban manne ya mfano yanayohusisha albino, ambapo polisi wakishirikiana na vyombo vingine vya usalama, walifanikiwa kupambana na kuwatia mbaroni baadhi ya watuhumiwa, huku pia wakikamata viungo vya albino.
Bi. Ester Jonas, mama wa marehemu Yohana Bahati, akiwa hajitambui katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza baada ya kukatwa mapanga na kunyang'anywa mtoto wake.
Tukio la mtoto Yohana Bahati (1) wa Kitongoji cha Ilyamchele, Buseresere wilayani Chato lililotokea Februari 2015 lilivuta hisia za watu wengi, ikiwemo jumuiya ya kimataifa, baada ya majahili kuvamia nyumbani kwa Bahati Misalaba na kumkata mapanga mama wa mtoto kabla ya kumnyang’anya na kutoweka naye.
Jitihada za vyombo vya usalama zikasaidia kupatikana kwa kiwiliwili cha mtoto huyo kikiwa kimefukiwa shambani, lakini tayari majahili hao wakiwa wameondoka na mikono na miguu, viungo ambavyo mpaka leo bado havijapatikana ingawa baadhi ya watuhumiwa wametiwa mbaroni.
Mara baada ya tukio hilo, likafuata tukio la mtoto Baraka Cosmas (4) wa Kijiji cha Kikonde wilayani Sumbawanga ambaye alikatwa kitanga cha mkono wa kulia, lakini jitihada za wanausalama zikafanikisha, siyo tu kuwakamata watuhumiwa wote akiwemo tajiri aliyetoa tenda, bali hata kiganja chenyewe ambacho inaelezwa kwamba tajiri huyo alikihifadhi nyumbani kwake.
Baraka Cosmas akiwa amelazwa Hospitali ya Rufaa Mbeya baada ya kukatwa kitanga cha mkono wa kulia.
Mtuhumiwa Sajenti Kalinga Malonji aliyekamatwa na kiganja cha Baraka.
Hiki ndicho kiganja cha Baraka ambacho mtuhumiwa Sajenti Kalinga Malonji alikamatwa nacho.
Aidha, FikraPevu inajua kwamba, tukio la kukamatwa kwa Mwalimu wa shule ya msingi huko Kahama mkoani Shinyanga, akiwa na mifupa inayodhaniwa kuwa ya binadamu akiambatana na waganga wa jadi nalo lilivuta hisia kubwa na likafanikiwa kufichua mambo mengi ikiwemo mitandao ya mauaji dhidi ya watu wenye ualbino.
Taarifa zinaeleza kwamba, kazi kubwa ambayo inastahili pongezi kwa jeshi hilo ni ile ya kuubomoa ‘mnada’ wa albino mkoani Tabora hasa baada ya kumkamata mtu mmoja akiwa katika harakati za kumuuza binti mwenye ualbino wilayani Nzega.
Kukamatwa kwa Masanja Mwinamila (44), mkazi wa Kitongoji cha Kona Nne, Kijiji cha Ugembe II, Kata ya Mwakashanhala, Tarafa ya Puge wilayani Nzega katika Mkoa wa Tabora akitaka kumuuza hai Margreth Hamisi (6) binti wa dada yake kwa mamilioni ya fedha kunadhihirisha kwamba matukio mengi ya kuuawa au kujeruhiwa kwa watu wenye ualbino yanapangwa na kufanikishwa na wanandugu wenyewe kwa sababu ya mawazo potofu ya kutafuta utajiri kwa njia za mkato.
Masanja Mwinamila siku alipokamatwa akitaka kumuuza hai mtoto Margret Hamisi, ambaye ni binti wa dada yake.
Mwandishi wa FikraPevu, Daniel Mbega akiwa na manusura Margreth Hamisi (kushoto) na kaka yake Tano baada ya kuokolewa kwa binti huyo huko Nzega
FikraPevu inafahamu kwamba, Masanja alikwishahukumiwa kifungo cha miaka 10 jela tangu Juni 19, 2015 baada ya kukiri kutenda kosa la kuteka nyara mtoto mwenye albinism kwa lengo la kutaka kwenda kumuuza.
Kesi zisizo na watuhumiwa
FikraPevu inafahamu kwamba, tangu mwaka 2006 hadi Mei 2017 kumekuwepo na matukio mbalimbali ya mauaji, kujeruhi na kuteka nyara watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Katika kipindi hicho takriban walemavu wa ngozi (albino) 39 waliuawa, 11 walijeruhiwa na wanne walitekwa nyara ambapo kati ya waliotekwa nyara, ni wawili tu waliokolewa – Margreth Hamisi wa Nzega na Tito Nkuryu wa Itilima mkoani Simiyu.
FikraPevu inaripoti bila shaka kwamba, kuna kesi takriban nne za mauaji ambazo hazina mtuhumiwa hata mmoja tangu matukio yatokee mwaka 2006 hadi 2009.
Mfano wa kesi hizo ambazo ziko mahakamani na upelelezi unatakiwa kufanyika ni Shauri lenye Namba. KAH/IR/92/2006, la mauaji ya Arip Amon wa Kahama; Shauri Namba. MIS/IR/2010/2007, la mauaji ya Sitakelewa Shitobelwa wa Misungwi; Shauri Namba. KDO/IR/1334/2008, la mauaji ya Safina Meshaki (miezi mitano) wa Mgalama – Kibondo; na Shauri Namba. GER/IR/2056/2009 la mauaji ya Gasper Elikana (10), aliyekuwa Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nyawilimirwa, Geita.
Mashauri mengine kadhaa yako mahakamani lakini kuna watuhumiwa ambao hawajapatikana, lakini kama serikali ingeongeza nguvu katika misako yake ingeweza kuwapata watuhumiwa.
Kama jeshi hilo lilifanikiwa walau kufuatilia na kukamata watuhumiwa katika kadhia hizo zilizotajwa, ni wakati sasa wa kuhoji nini kilichotokea hata ikawa wameshindwa kupambana na matukio hayo.
Yawezekana wako kazini, lakini kazi yenyewe ina ufanisi kiasi gani ikiwa kila siku kuna matukio mapya? Ni ufinyu wa bajeti au kujisahau? Ni kupuuza janga hilo ama kusubiri matukio yatokee ndipo waanze kukimbizana?
FikraPevu inaona kuna kila sababu, tena ya msingi kabisa, ya kuhakikisha serikali kupitia vyombo vyake vya usalama, inashughulikia masuala ya mauaji ya albino, ambayo yanakwenda sambamba na mauaji ya vikongwe, ili kurudisha amani ya wananchi badala ya kuzidi hofu na mashaka.
Kama serikali iliona iko salama, basi ni wakati wa kuongeza fungu katika kazi maalum kama hizi, ikibidi kuwashirikisha na albino wenyewe katika mapambano hayo katika msingi wa kujenga uwazi na uwajibikaji.