BARABARA za lami zenye urefu wa kilometa 689.9 ambazo zimegharimu jumla ya Shs. 781.132 bilioni zinafunguliwa na kuzinduliwa na Rais Dkt. John Magufuli kuanzia Julai 19, 2017 huku Mkoa wa Kigoma ukiunganishwa kwa mtandao wa barabara za lami.
FikraPevu inafahamu kwamba, miradi tisa kati ya 10 ya ujenzi wa barabara hizo zinazozinduliwa mwezi Julai 2017 imejengwa na makandnarasi kutoka China.
Ujenzi wa kipande cha kilometa 6 katika barabara ya Tabora-Nyahua
Uchunguzi wa FikraPevu unaonyesha kwamba, barabara ya Kigoma – Biharamulo – Lusahunga yenye urefu wa kilometa 154 ambayo inatarajiwa kufunguliwa na Rais Magufuli Julai 19, 2017 imejengwa kwa ubia baina ya kampuni mbili za China ambazo ni China Henan International Cooperation Group Co. Ltd. (CHICO) na China Railway Seventh Group.
Barabara hiyo, ambayo iligharimu Shs. 191.454 bilioni, imeweza kuunganisha Mkoa wa Kigoma na mikoa ya Kagera na Geita na kurahisisha mawasiliano ambayo awali yalikuwa ya shida.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Nyakanazi – Kibondo yenye urefu wa kilometa 50 unatarajiwa kufanyika Kakonko, Kigoma Julai 21, 2017.
Hiyo ndiyo barabara pekee katika Ukanda wa Magharibi (Western Corridor) ambayo inajengwa na kampuni ya kizalendo ya Nyanza Road Works, ambapo itagharimu Shs. 45.985 bilioni.
Taarifa kutoka Ikulu zinaeleza kwamba, siku hiyo hiyo ya Julai 21, 2017 Rais Magufuli atazindua ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Kidahwe – Kasulu yenye urefu wa kilometa 63.
Barabara hiyo inajengwa na kampuni ya China Railways 50 Group kutoka China kwa gharama ya Shs. 41.88 bilioni na tayari Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, ameipa kampuni hiyo hadi mwezi Mei 2018 badala ya Novemba 2018 kukamilisha ujenzi huo ili kuharakisha mkakati wa Serikali wa kuufungua mkoa wa Kigoma kwa barabara za lami.
Taarifa za Ikulu zinaeleza kwamba, Julai 23, 2017 Rais Magufuli a atafungua barabara ya Kaliua – Kazilambwa yenye urefu wa kilometa 56 huko Kaliua.
Taarifa kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) zinasema, barabara hiyo imejengwa na kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co. Ltd. (CHICO) kwa gharama ya Shs. 58.563 bilioni.
FikraPevu inafahamu kwamba, kampuni ya CHICO kutoka Jimbo la Henan nchini China ambayo iliwahi kupata mkataba wa Dola za Marekani 206 milioni wa ujenzi wa barabara kutoka Wakala wa Maendeleo ya Barabara nchini Zambia ili kujenga barabara ya Mansa-Luwingu nchini humo, ndiyo iliyopewa mikataba mingi ya ujenzi nchini Tanzania.
Hadi kufikia mwaka 2014 CHICO ilikuwa na mikataba 13 nchini Tanzania ya barabara zenye urefu wa 705.2km yenye thamani ya Dola za Marekani 490.26 milioni kwa wakati huo.
Mikataba hiyo ni pamoja na barabara ya 34km ya Singida-Iguguno awamu ya kwanza, 42km za barabara hiyo ya Singida-Iguguno awamu ya pili, 33km za barabara ya Sekenke-Shelui awamu ya tatu, 60km za barabara ya Mwandiga-Manyovu, 35.7km za barabara ya Kigoma-Kidahwe, 19.20km za barabara ya Bonga-Babati, 42km za barabara ya Tabora-Urambo, 59.1km za barabara ya Kyaka-Bugene, 84.6km za barabara ya Dareda-Minjingu, 76.6km za barabara ya Kidahwe-Uvinza-Ilunde, 132km za barabara ya Isaka-Ushirombo, 1.5km ya upanuzi wa Barabara ya Kilwa awamu ya tatu, 85.5km za barabara ya Nyanguse-Musoma, na 154km za barabara ya Kigoma-Lusahunga.
FikraPevu imearifiwa pia kwamba, siku hiyo ya Julai 23, 2017 Rais Magufuli atafungua barabara ya Urambo – Ndono – Tabora yenye urefu wa jumla ya 94km, ufunguzi ambao utafanyika mjini Urambo.
Barabara hiyo imejengwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza ya 42km kutoka Tabora hadi Ndono imejengwa na kampuni ya CHICO kwa gharama ya Shs. 51.346 bilioni, na awamu ya pili yenye urefu wa 52km kutoka Ndono hadi Urambo imejengwa na China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kwa gharama ya Shs. 59.764 bilioni.
Mnamo Julai 24, 2017, taarifa zinasema, Rais Magufuli atafungua barabara ya Tabora – Puge – Nzega yenye urefu wa kilometa 114.9, uzinduzi ambao utafanyika Tabora mjini.
Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara hiyo kutoka Nzega-Puge (58.8km) imejengwa na kampuni ya China Communications Construction Company (CCCC) kwa gharama ya Shs. 66.358 bilioni, wakati awamu ya pili (56.1km) kutoka Puge hadi Tabora imejengwa na kampuni ya umma ya China, Sinohydro, kwa gharama ya Shs. 62.737 bilioni.
FikraPevu inafahamu kwamba, Sinohydro ndiyo “sura ya upanuzi wa China ulimwenguni” kwani ina mikataba katika nchi 55 duniani kuanzia Bara Asia, Afrika, Ulaya (kutoka makao makuu ya Umoja wa Ulaya huko Belgrade, Serbia), Amerika Kaskazini na Amerika Kusini, ambapo nchini Tanzania ilishinda mikataba 12 ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa 779.95km.
Kulingana na ratiba hiyo, kabla ya kufungua Uwanja wa Ndege wa Tabora siku hiyo ya Julai 24, 2017 Rais Magufuli atafungua barabara ya Tabora – Nyahua yenye urefu wa kilometa 85 mjini Tabora ambayo imejengwa na kampuni ya China Chongqing International Construction Corporation (CICO) kwa gharama ya Shs. 93.402 bilioni.
Hata hivyo, kilometa sita za barabara hiyo bado hazijakamilika na mkandarasi huyo amepewa hadi kufikia Oktoba 2017 awe amekamilisha ujenzi.
Aidha, Julai 25, 2017 Rais Magufuli atafungua barabara ya Manyoni – Itigi – Chaya yenye urefu wa kilometa 89.3, ufunguzi utakaofanyika mjini Itigi.
Ujenzi wa barabara hiyo umefanywa na kampuni ya Sinohydro kwa gharama ya Shs. 109.643 bilioni.