TANROADS Kagera yakiri kutolipa fidia kwa wananchi

Jamii Africa

WAKALA wa barabara mkoani Kagera (TANROADS) imekiri kudaiwa mamilioni ya shilingi na wananchi walioathiriwa na upanuzi wa barabara ya Mutukula Muhutwe uliofanyika zaidi ya miaka kumi na tano iliyopita.

Hayo yamebainika wiki hii baada ya baraza la madiwani wa wilaya ya Bukoba kuwabana viongozi wa TANROADS juu ya utekelezaji wa sheria mpya ya hifadhi ya barabara ilihali bado kuna wananchi wanaodai fidia.

Diwani wa kata ya Katoma Silvand Kempanju alihoji hatima ya wananchi ambao hawakulipwa mita tano kama walivyohaidiwa,na badala yake kutangazwa kwa sheria mpya itakayofanya wananchi wasilipwe haki yao.

Wakati wa upanuzi wa barabara ya Mutukula-Muhutwe  mwaka 1992 iliyojengwa kwa kiwango cha lami wananchi walilipwa mita 17.5 badala ya 22.5 na kupewa ahadi ya kulipwa kiasi kilichobaki hapo baadaye.

Sheria ya sasa imeongeza urefu wa hifadhi ya barabara kutoka mita 22.5 kila upande hadi mita 30 hali inayoyafanya maeneo mengi ya wananchi kuangukia katika hifadhi ya barabara.

Akijibu hoja za madiwani mwakilishi wa Tanroads mhandisi Jackson Lwerengera alikiri wananchi kulipwa mita pungufu wakati wa upanuzi wa barabara na kuwataka waendelee kuvuta subira wakingoja uamuzi wa serikali.

Akiwa ameongozana na Phares Nsindaji pia mtaalamu kutoka Tanroads, Lwerengera alieleza kuwa wapo wananchi watakaolipwa ambao mali zao zipo nje ya mita 22.5 ambapo sheria ya sasa imeongeza mita hizo kufikia 30.

“Hili ni suala la kitaifa serikali iliona umuhimu wa kuwa na barabara kubwa wananchi hawaruhusiwi kufanya maendeleo mapya, kama kuna mali hiyo italipwa” alisema Lwerengera.

Katika kikao hicho mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bukoba Sadru Nyangashe alisema sheria mpya iliyoambatana na bomoa bomoa kabla ya kusitishwa iliwachonganisha wananchi na serikali baada ya kutoelimishwa kwanza.

Pia alitaka elimu ya kutosha itolewe kwanza kwa wananchi kuhusu sheria mpya ya hifadhi ya barabara na wananchi wanaostahili kulipwa wapewe haki yao.

Habari hii ni kwa mujibu wa mwandishi wa Fikra Pevu – Phinias Bashaya aliyeko mjini Bukoba, Kagera

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *