HIVI karibuni, Rais John Pombe Magufuli alitoa agizo kwamba hakuna mwanafunzi aliyepata ujauzito atarudi shule kuendelea kwa masomo kwa kuwa serikali haiwezi kusomesha wazazi.
Ingawa wito huo wa Rais unaweza kuwa sehemu ya suluhisho la mimba kwa wanafunzi wa kike lakini siyo suluhisho bora kwa ustawi wa mtoto wa kike katika nyanja ya elimu.
Kwa maoni yangu, ni vyema tukajikita kutazama mzizi wa tatizo na kuweza kuuondoa ili lisiendelee kujirudia badala ya kuangalia matokeo ambayo ni mimba yenyewe na kumhukumu mwanafunzi huyo kwa kumnyima elimu.
Natambua kuwa watu wengi wanadhani kupata mimba ni suala la mwanafunzi husika kuwa mhuni tu ama tabia ya wanafunzi wa kike kupenda ngono.
Aina ya mawazo haya yanatokana na dhana za kibepari ambazo huaminisha watu kuwa tatizo kama hilo ni lake mwenyewe na siyo tatizo la mfumo husika. Hapa ndipo utasikia ya kuwa mtu yule ni maskini kwa kuwa hajasoma, hajajiajiri, amelogwa, siyo mchapa kazi na mengine mengi.
Aina hii ya mawazo tunayasikia kila siku kwa kuwa ubepari unaamini katika dhana ya ubinafsi na siyo dhana nzima ya jamii na hali hii ndiyo inayotukumba katika suala la mimba za wanafunzi kwa kuwa tunafikiri hili ni tatizo la watoto wa kike kwa kuwa hawajieshimu, hawapendi masomo, wana tamaa ya ngono, pesa, wakaidi, hawana maadili na mengine mengi.
Kama lingalikuwa tatizo la mimba za wanafunzi ni lao moja kwa moja ama sababu kama hizo nilizotaja hapo juu zenye mrengo wa kibepari basi kuwafukuza shule lingalikuwa suluhisho.
Kwa mtazamo wangu, mimba kwa wanafunzi siyo tatizo binafsi tu bali ni tatizo la kimfumo linalochangiwa kwa asilimia kubwa sana na mazingira.
Natambua dhana ya mazingira ni pana hivyo nitatumia nadharia ya Human Ecology kueleza maana ya mazingira katika muktadha huu.
Nadharia ya Human Ecology inasisitiza ya kuwa mazingira ya asili ama yale ya kutengenezwa na binadamu huchangia mabadiliko ya tabia ya mtu husika.
Kwa mantiki hiyo, mazingira yanaweza kuwa yale yaliyotengenezwa na binadamu, mazingira ya asili na mazingira ya kijamii na kwa utamaduni ambao mtu husika hupatikana.
Nadharia hii inatuonyesha wazi kwamba tabia ya mtu yeyote huchangiwa na mwingiliano alionao na mazingira yake. Kwa kusisitiza zaidi vile tunavyoona tabia za watu leo hii ndio mwingiliano alionao na mazingira yake ya asili ama yale ya kutengenezwa na mwanadamu mwenyewe.
Kwa mfano, leo hii urembo na utanashati unatafsiri tofauti kutokana na mazingira ya sasa. Kwa wanawake ili waonekane warembo lazima watinde nyusi, wapake vipodozi, waweke nywele bandia na kuvaa mavazi tunayodhani ndiyo ya kisasa.
Kwa wanaume, lazima wavae suruali za kubana mithili ya zile za kike, wengine washushe suruali nusu makalio, unyoe kiduku, kujichubua kidogo, kuvaa viatu bila soksi na kadhalika.
Hiyo mifano hapo juu inatoa taswira ya namna mazingira yetu yanavyoweza kuwa na nguvu kubwa ya ushawishi kiasi cha kukufanya utende bila kutumia utashi kwani usipofanya utaonekana wa kale na ili kuendana na mazingira binadamu aliyoyatengeneza lazima ufanye kama wao ili ufanane nao.
Suala la mimba za wanafunzi ni tunda la mazingira, ambalo linawakumba wanafunzi wetu hawa. Kama tunataka kutatua tatizo hili ni vyema tuanze na kurekebisha mazingira yale ambayo siyo rafiki kwa watoto wa kike ili kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la mimba kwa wanafunzi.
Kama nilivyosema hapo awali, wanafunzi hawa wa kike huishi katika mazingira aidha yaliyo rafiki au siyo rafiki kwao.
Hapa nitapenda kuangalia mambo kama umbali kutoka nyumbani hadi shuleni, aina ya elimu inayotolewa, adhabu zitolewazo, mahitaji muhimu ya wanafunzi, hali ya uchumi, kukosa mlo wawapo shuleni, ukosefu wa vyumba vya kulala kwa wanafunzi watokao mbali hasa wa sekondari, malezi hafifu, talaka kwa wazai, malezi kutokuwa ya jamii nzima, ombwe la maadili, elimu kutokuwa na mvuto, elimu isiyoleta matumaini ya ajira, tamaduni, siasa, ufisadi na mengine mengi.
Haya yote ni mazingira ya asili au yale ya kutengenezwa na mwanadamu ambayo yanaweza kuchangia yote kwa pamoja kwa asilimia nyingi mwanafunzi kupata mimba.
Tunapoamua kuwahukumu kwa kuwanyima fursa ya kusoma ni kana kwamba tunasema wanafunzi hawa wanaishi katika ulimwengu wao peke yao, na kwamba ni kosa lao binafsi na siyo kosa la mfumo wala mazingira.
Suluhisho la kweli katika vita dhidi ya mimba za wanafunzi ni kupambana na mazingira yanayowakumba watoto wa kike badala ya kuendelea kuwakandamiza kwa kuwanyima haki ya kukosa elimu.
Endapo watoto waliojifungua watakosa elimu ni dhahiri ya kuwa mzunguko wa umaskini utaendelea na kuongeza idadi kuwa ya watoto wa kike kutopata elimu na kuruhusu mgawanyiko baina ya wanawake na wanaume kuwa kubwa.
Kwa ujumla, makatazo pekee siyo suluhisho muhimu katika vita dhidi ya mimba za wanafunzi, bali ni vyema kuyarekebisha mazingira yote yanayosababisha kuwepo kwa mimba hizo.
Ni vyema Wizara ya Elimu na idara zake husika ikafanya utafiti wa kina kugundua changamoto za kimazingira, binafsi na za kisaikolojia ili kuja na mbinu mbadala itakayokuwa na tija zaidi kwa watoto wa kike ili mapambano yawe ya kisayansi zaidi.
Mwandishi wa hii makala amechambua vizuri na amefirikia kwa mapana. Kama jamii kwa kiasi kikubwa ingekuwa na mtizamo na fikra kama hizi pengine mimba mashuleni zingetokomezwa na mtoto wa kike angepata elimu bila kikwazo cha mimba shuleni.