MMEM yaongeza idadi ya wanafunzi shuleni,  yasahau kujenga vyoo

Jamii Africa

“Tunahitaji kutetea mfumo wa elimu unaokidhi mahitaji na kufanya mabadiliko  ili kuleta elimu bora kwa watoto wetu na taifa la kesho kwa ujumla”. Hii ni nukuu ya aliyekuwa Waziri wa elimu, Magreth Sitta aliyoitoa mwaka 2006 katika kuonyesha umuhimu wa elimu nchini.

Elimu ya msingi iko katika mfumo maalumu ambao huongoza utendaji  na uendeshaji wa shule za msingi ambazo ni muhimu kwa kila raia wa watanzania kupitia aina hii ya elimu kwa sababu humjengea msingi wa kuendelea kusoma elimu ya sekondari na chuo. Lakini elimu ya msingi imepitia vipindi mbalimbali vya uendeshaji na kuifikisha hapa ilipo.

Wakati Tanzania inaingia katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 ililazimika kuwa na mfumo huru wa elimu   ambao unatoa fursa kwa shule binafsi na jukumu la serikali kubeba gharama zote za shule likapungua ambapo wazazi ambao ndio walezi wa wanafunzi walikuwa na sehemu ya kuchangia katika maendeleo ya shule.

Mfumo huo wa kuchangia elimu ya msingi ulikuwa na athari kwa watoto ambao walitakiwa kulipiwa gharama za masomo ndipo waruhusiwe kujiunga na shule. Watoto wengi walibaki nyumbani na kulazimika kuajiriwa, wengine waliandikishwa wakiwa na umri mkubwa.  

Elimu hii ya msingi ilionekana kama ya kibaguzi kwa sababu watu waliokuwa na uwezo mzuri wa kiuchumi ndio waliweza kumudu gharama  za kuwasomesha watoto na familia zenye kipato kidogo ziliendelea kutaabika katika ujinga na umaskini.

Serikali ya awamu ya tatu chini ya rais Benjamin Mkapa ilifanya tathmini na kutambua idadi kubwa ya watoto walikuwa hawapati haki ya kwenda shule. Mabadiliko makubwa ya mfumo yalifanyika ili kutoa nafasi zaidi kwa watoto wa Tanzania kupata elimu ya msingi ambayo itawaandaa kujitegemea katika nyanja mbalimbali za maisha. 

Mabadiliko haya yaliambatana na kuifanya elimu ya msingi iwe bure ambapo serikali ilibeba jukumu tena la kuratibu na kulipa gharama zote za wanafunzi wanapokuwa shuleni. Mabadiliko haya ambayo yalikuja mwaka 2001 yalipokelewa kwa hisia tofauti na wananchi.

Mageuzi hayo yaliambatana na mfumo mpya uliojulikana kama Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi Awamu ya kwanza (MMEM I) ambao ulilenga zaidi kuboresha elimu ya msingi. Jitihada zilizofanyika ni kujenga na kuboresha madarasa katika shule mbalimbali ili kupokea idadi kubwa ya wanafunzi ambao walikuwa nyumbani.  

 Takwmui zinaonyesha kuwa tangu serikali ianzishe mfumo wa kutoa elimu bure mwaka 2001 idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa imeongezeka kutoka milioni 4.9 mwaka 2001 mpaka wanafunzi milioni 8.3 mwaka 2010.

Awamu ya kwanza ya MMEM I ilionyesha mafanikio makubwa na mipango zaidi ikafanyika kuandaa mpango mwingine wa MMEM II ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2007 hadi mwaka 2011.

Ikitoa hotuba bungeni Waziri wa Elimu na Mafunzo Stadi wa wakati huo, Shukuru Kawambwa  wakati wa makadirio ya bajeti ya wizara ya elimu ya mwaka 2012/2013, alisema Serikali iliendelea kutekeleza Awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM II) kwa kutoa Ruzuku ya Uendeshaji wa Shule, ambapo wastani wa Shilingi 6,025 zilitolewa kulinganisha na lengo la Shilingi 10,000 kwa kila mwanafunzi wa Elimu ya Msingi.

MMEM II umefanyiwa mapitio ili kuwezesha maandalizi ya MMEM III. Katika utekelezaji wa mpango huu, idadi ya wanafunzi walioandikishwa katika Darasa la Kwanza iliongezeka kutoka 1,356,574 mwaka 2010 hadi 1,404,998 mwaka 2012 na idadi hiyo inaongezeka.

Aidha, watoto wa jinsi zote wanapata fursa ya kuandikishwa katika Elimu ya Msingi; idadi ya Shule za Msingi nchini imeongezeka kutoka 15,816 mwaka 2010 hadi 17,379 mwaka 2017.  Mafanikio ya MMEM yamesaidia kuongeza wanafunzi katika shule na ufaulu lakini changamoto inayobaki ni ubora wa elimu  kukosa stadi muhimu ambazo nwanafunzi anapaswa azipate.

 Licha ya mafanikio yaliyopatikana kwenye Mpango wa MMEM bado changamoto imebaki kwenye uejnzi wa vyoo. Nguvu kubwa imewekezwa kuongeza idadi ya madarasa lakini vyoo vimesahaurika. Mathalani shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko iliyopo wilaya ya Tunduru ina wanafunzi 1,367 ambao wanatumia matundu 10 vyoo ambapo kwa wastani tundu moja linatumiwa na wanafunzi 100.

Kulingana na mwongozo wa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inazitaka shule kuwa na uwiano mzuri wa vyoo ambapo tundu 1 kwa wasichana 20 (1:20) na kwa wavulana ni (1:25). Lakini kwa shule nyingi hali tofauti na matarajio ya wizara iliyo na jukumu la kuboresha miundombinu ya shule.
Taarifa za shirika la Haki Elimu zinaonyesha kuwa katika utekelezaji wa MMEM II mwaka 2008/2009 vyoo 29,328 vilitajwa kujengwa lakini bajeti yote kwa mwaka huu ilikuwa ni bilioni 7 ambayo ingeweza kujenga vyoo 14,285 tu na miradi mengine ingetakiwa kusimama. Pia katika mwaka wa 2009/2010 bajeti ilikuwa bilioni 7 ambayo ingejenga vyoo 29,328 ambavyo vilipangwa kujengwa mwaka 2009, bajeti hii ni uthibitisho kuwa fedha zinazoelekezwa katika mpango huo hazikidhi mahitaji ya miradi yote inayotakiwa kutekelezwa.

Serikali inahitaji umakini zaidi katika kutenga bajeti za maendeleo ya shule ili kuepuka matatizo yanayotokana na kushuka kwa kiwango cha elimu nchini ambacho huatarisha mstakabali wa wanafunzi ambao taifa linawategemea kutumia rasilimali zilizopo kuleta mabadiliko katika jamii.
 Mpango huu tangu unaanzishwa mwaka 2001 ulionyesha kuwa mkombozi wa shule za msingi lakini kadri unavyoboreshwa katika awamu tofauti unakabiliwa na changamoto nyingi za utendaji hivyo kuathiri maendeleo ya elimu nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *