Ukatili wa kijinsia ni matendo yote yanayolenga kuvunja haki za binadamu ikiwemo kudhalilisha utu wa mtu. Ukatili huo hutokea kwa wanawake na wanaume lakini wanaoathirika zaidi ni wanawake, hii ni kwa sababu mila na desturi, mifumo ya kisheria na sera inampa sauti na nguvu zaidi mwanaume.
Ukatili wa kijinsia uko wa aina mbalimbali: kutumia nguvu, saikolojia, kiuchumi, udhalilishaji wa kingono, mauaji na udhalilishaji wa watoto. Vitendo vya ukatili huambatana na vipigo, kuchomwa moto, ubakaji, ukeketaji wanawake, mimba na ndoa za utotoni, mauaji ya wazee, kunyimwa mahitaji na kumiliki mali.
Mahusiano ya binadamu katika eneo katika shughuli za kiuchumi, kijamii, kisiasa au kitamaduni huuwa na matokeo chanya na hasi kwa wanaume na wanawake. Kama hakuna usawa uwezekano wa haki za binadamu katika eneo husika kufunjwa ni mkubwa.
Shule za msingi ni eneo mojawapo ambapo vitendo vya ukatili hutokea ambapo huathiri mwenendo wa elimu ya wanafunzi. Watu ambao wanatakiwa kuwalinda watoto na kuhakikisha wanapata elimu bora, wakati mwingine huwageukia wanafunzi hao na kuwafanyia ukatili.
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inatamka wajibu wa jamii katika kumlinda na kutunza haki za mtoto ili kuhakikisha analelewa na kuwa ustawi mzuri katika maisha yake. Lakini bado haki za mtoto zinavunja.
Utafiti wa Shirika la Watoto Duniani (UNICEF-2011) unaeleza kuwa msichana mmoja kati ya watatu na mvulana mmoja kati ya saba ameshawahi kufanyiwa ukatili wa kijinsia. Pia zaidi ya asilimia 70 ya wavulana na wasichana wameshawahi kufanyiwa ukatili wa namna fulani kwenye miili yao kabla ya kutimiza miaka 18.
Vitendo hivyo hufanyika kwa siri, na huchukua muda mrefu mpaka vikajulikana kwa watu kwa sababu wanafunzi wanaofanyiwa hasemi kwa kuhofia wale waliowafanyia kuwadhuru. Ukatili wa kijinsia ni uvunjaji wa haki za binadamu kwa sababu huathiri utu wa mtu na maisha yake.
Mkurugenzi wa Kituo cha Jinsia Chuo Kikuu Cha Dar es salaam, Dkt. Eugenia Kafanabo anasema mwaka 2015 walifanya utafiti kubaini Ukatili wa Kijinsia katika shule za msingi zilizopo katika Wilaya za Ilala na Temeke ambapo walikutana na ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto ambapo ukatili unafanywa na watu walio karibu na watoto wakiwemo wazazi, walimu na wafanyakazi wengine wa shule.
“ Ukatili wa kijinsia unatokea hata katika shule za msingi na inaonekana ni mateso ya kisaikolijia yanayofanyika sirini kwa wanafunzi wengi hasa wa kike ambapo huathiri maendeleo ya masomo na wengine hulazimika kuacha shule” anasema Dkt. Kafanabo.
Ukatili ambao unawakumba wanafunzi hao ni kunyimwa chakula, kupigwa bila sababu, kudhalilishwa kingono, kubakwa na kulawitiwa, kunyimwa pesa ya matumizi, kufanyishwa kazi ngumu na kupewa majina ya kudhalilisha.
“Tuliwahoji wanafunzi 4000 na kati ya hao wanafunzi 1,268 walisema hawapewi chakula nyumbani na hata wakifika shuleni hawapati chakula na hukaa na njaa. Lakini wanaopigwa bila sababu walikuwa 663 na 553 walidhalilishwa kingono”, anafanunua Dkt. Kafanabo.
Anaeleza kuwa wanafunzi wengi wa shule za msingi nchini hawako salama na wanahitaji uangalizi wa karibu ili kuwaepusha na matendo hayo ambayo hutendwa na watu wa karibu na wanafunzi, ambapo hukatazwa na wahusika kuwaambia watu wengine kwa yale wanayotendewa.
Walimu Wakuu, waalimu walezi (patrons), wafanyakazi katika shule na wanafunzi wenye umri mkubwa wanatajwa na utafiti huo kuongoza kuwadhalilisha wanafunzi hasa wa kike, jambo linalowaathiri kisaikolojia na kuwalazimu baadhi ya wanafunzi kuacha shule na kujiingiza katika kazi hatarishi.
“Wanafunzi 1343 walisema Walimu Wakuu katika shule za msingi walidhalilisha na walimu walezi (992) wakifuatiwa na wanafunzi wenye umri mkubwa (240). Wanafunzi hawana mahali pa kusemea yanayowakuta wanabaki kimya kwa sababu wanatishiwa kuuwawa”, anasema Dkt. Kafanabo.
Mwalimu akiwa darasani anafundisha wanafunzi
Kulingana na Utafiti huo, Wasichana wanatajwa kuathirika sana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambapo wasichana 1,822 walitendea ukatili ikilinganishwa na wavulana 1,513.
Changamoto kubwa ni ukosefu wa takwimu sahihi kuhusu tatizo hilo, kwani vitendo hivyo huwa haviripotiwi na wanaovitekeleza hawachukuliwi hatua za kisheria kutokana na ukosefu wa ushaidi au rushwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya PiepPoint Limited, June Warioba anasema yeye ni mmoja wa waathirika wa vitendo vya ukatili na anawataka waliotendewa wasikae kimya bali watoe taarifa ili wapate msaada. Anasema ukatili wa kijinsia unaweza kumpata mtu yoyote pasipo kujali hadhi aliyonayo.
Licha ya wanafunzi hao kunyimwa haki zao shuleni, pia wakirudi nyumbani nako hukutana na ukatili ambao hufanyiwa na madereva wa bodaboda, majirani na ndugu wa karibu wakiwemo wazazi wa kiume.
Serikali na wanaharakati wameshauriwa kutoa elimu na kutengeneza mfumo rasmi katika shule utakaosaidia wanafunzi kusikilizwa na kubaini changamoto wanazokabiliana nazo, kwa sababu huduma hiyo haipatikani katika shule nyingi. Hata wanaotakiwa kuwalinda wanafunzi ndio vinara wanaowadhalilisha wanafunzi.
“Ukatili wa kijinsia ni tatizo ambalo limekita mizizi katika jamii zetu lakini tuendelee kutoa elimu kwa watu ili wabadilike” anasema Dkt. Kafanabo.
Ili kutokomeza ukatili wa kijinsia, Mshauri wa Mambo ya Jamii kutoka Shirika la ICI Consults, Lawrence Kilimwiko anasema mabadiliko ya kisera na sheria zinazosimamia mila na desturi na jamii zinatakiwa zipitiwe na zile zinazomkandamiza mwanamke na mtoto ziboreshwe ili kujenga usawa katika matumizi ya rasilimali za nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Wanawake Wanahabari Tanzania (TAMWA), Edda Sanga amesema ukatili wa kijinsia kwa watoto bado ni tatizo kubwa ambalo linafanyika kwa siri, na juhudi za vyombo vya habari zinahitajika ili kuibua matukio hayo na kutoa elimu kwa jamii kumlinda mtoto na kumuhakikishia haki ya kuishi na kupata elimu.