Mlima Kilimanjaro umeshinda tuzo ya Kivutio Bora cha Utalii Afrika mwaka 2017 na ushindi huo ni wa nne tangu mwaka 2013.
Ushindi huo ulitangazwa katika hafla ya Tuzo ya Maeneo yanayotembelewa zaidi duniani (World Travel Awards-WTA) zilizofanyika katika jiji la Kigali nchini Rwanda, ambapo Tanzania ilipata tuzo 3 kikiwemo kisiwa cha Thanda na nyumba ya kulala wageni ya Four Seasons iliyopo katika hifadhi ya Serengeti.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa (TANAPA), Allan Kijazi ambaye aliiwakilisha nchi na kupokea tuzo ya Mlima Kilimanjaro ambao ni miongoni mwa hifadhi za taifa 16 zilizo chini ya TANAPA.
Mlima Kilimanjaro ambao una urefu mita 5,895 umetangazwa kama eneo muhimu ambalo linaongoza kwa kuvutia watalii wengi kutokana na upekee ulionao wa kuwa mlima mrefu kuliko yote Afrika. Mlima huo umeendelea kutetea tuzo kwa mara ya tatu mfululizo tangu uliposhinda mwaka 2015 na 2016. Kwa mara ya kwanza ulishinda mwaka 2013.
Kulingana na taarifa ya WTA inaeleza kuwa Tanzania pia imepata umaarufu kwa kupata tuzo nyingine ya Nyumba bora ya kulala wageni ambapo Four Seasons iliyopo katika hifadhi ya Serengeti imeshinda tuzo hiyo. Pia Kisiwa cha Tanda kilichopo ndani ya kisiwa cha Shungimbili katika Wilaya ya Mafia kilishinda taji la kisiwa cha anasa barani Afrika.
Mlima Kilimanjaro ulishindanishwa na vivutio vingine vilivyomo Afrika ikiwemo Hifadhi ya Ngorongoro Crater, Kasri la Giza (Misri), Kisiwa cha Robben (Afrika Kusini), Mlima Table (Afrika Kusini) na Maporomoko ya maji ya V&A Waterfront (Afrika Kusini).
Ushindi wa Mlima Kilimanjaro ni matokeo ya kushinda tuzo mara mbili mfululizo, kupigiwa kura na watu wengi na kufikia vigezo ambavyo viliwekwa na watoaji wa tuzo hizo WTA.
Tuzo ya Mlima Kilimanjaro iliyotolewa na WTA
Tuzo zingine ambazo Tanzania imejipatia ni tuzo ya mbuga ya wanyama bora ambapo mbuga ya wanyama ya Singita iliyopo katika hifadhi ya Serengeti imeibuka mshindi wa kwanza. Tuzo ya Afrika ya Kisiwa Huru cha Watalii imeenda kwa ‘And Beyond Mnemba Island Lodge’ iliyopo Zanzibar. Pia imepata tuzo ya Kampuni Bora ya Utalii ambayo imeenda kwa kampuni ya Abercrombie and Kent iliyopo Arusha.
Sekta ya utalii ina umuhimu kwa maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii ya Tanzania. Sekta inahusika katika uzalishaji wa ajira, mapato ya serikali, utunzaji wa mazingira na viumbe hai.
Akisoma Hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii bungeni mwaka huu, Waziri Prof. Jumanne Maghembe alisema sekta ya utalii kwa kipindi cha mwaka 2016 na 2017 imeajiri watu laki tano na wengine milioni moja walijiajiri wenyewe. Sekta hiyo ilichangia asilimia 17.5 ya pato la taifa na kulipatia taifa asilimia 25 ya fedha zote za kigeni.
Hali ya Utalii Tanzania
Kulingana na Wizara ya Maliasili na Utalii inasema Tanzania ni moja ya nchi yenye vivutio vingi vya utalii ambavyo bado havijajulikana na watu wengi. Ni nchi yenye maajabu mengi ikiwa imezungukwa na uoto wa asili.
Mlima Kilimanjaro, mlima mrefu kuliko yote Afrika uliozungukwa na barafu, Kisiwa cha Zanzibar, hifadhi ya wanyama ya Serengeti, Ziwa Manyara, Ngorongoro Crater, Ruaha, Selous na hifadhi ya bahari katika kisiwa cha Mafia ni miongoni mwa vivutio vingi vya Tanzania.
Taarifa ya wizara hiyo inaendelea kusema kuwa muonekano mzuri wa mandhari ya nchi na watu wakalimu wanaifanya Tanzania kuwa sehemu bora ya kutembelewa na watu kutoka duniani kote.
Tanzania ina Hifadhi za Taifa 16, mbuga za wanyama 17, hifadhi ya kihistoria 1, hifadhi za bahari, fukwe ukanda wa maziwa na nyanda za juu ambazo huakisi utajiri wa asili uliopo nchini.
Hifadhi za Taifa
Hifadhi za Taifa zilizopo zinatumika kama njia mojawapo ya utunzaji wa mazingira kwa vizazi vijavyo. Hifadhi zilizopo ni:
- Hifadhi ya Taifa ya Arusha
- Hifadhi ya Gombe
- Hifadhi ya Katavi
- Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro
- Hifadhi ya Kitulo
- Hifadhi ya Ziwa Manyara
- Hifadhi ya Mikumi
- Hifadhi ya Mkomazi
- Hifadhi ya Ruaha
- Hifadhi ya Kisiwa cha Rubondo
- Hifadhi ya Saadani
- Hifadhi ya Serengeti
- Hifadhi ya Tarangire
- Hifadhi ya Odzungwa
- Hifadhi ya Saanane
- Hifadhi ya Milima Mahale
Licha ya kuwa na vivutio vingi katika maeneo mbalimbali nchini, sekta ya utalii imejikita zaidi katika mkoa wa Arusha na Zanzibar ambapo inakadiriwa kuwa asilimia 90 ya watalii toka nje wanatumia muda wao mwingi katika maeneo hayo mawili.