China taifa lililo Mashariki ya mbali lenye uchumi unaokuwa kwa kasi na kuwa miongoni mwa mataifa duniani yenye ushawishi mkubwa katika diplomasia ya kimataifa.
Mafanikio ya kiuchumi ya Jamuhuri ya China ni uongozi thabiti wa nchi hiyo ambao umejengwa kusimamia kikamilifu sera na rasilimali za taifa hilo ili kuwaletea maendeleo wananchi. Taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu ambao wanazidi bilioni moja, limeendelea kijiimalisha katika nchi nyingi na hata kutishia maslai ya nchi kubwa kama Marekani yenye nguvu kubwa ya kiuchumi na kisiasa “Super Power”.
Licha ya China ya kuwa na viongozi thabiti ambao wameitoa China katika moja ya nchi zilizokuwa maskini katika miaka ya 60, waliasisi Mapinduzi ya Kijani ‘Green Revolution’ ambayo yalichochea ukuaji wa kilimo na uanzishwaji wa viwanda vikubwa vya nguo na bidhaa mbalimbali ambazo zinauzwa katika nchi nyingi duniani. Kipato kinachopatikana kimeendelea kutumika kuboresha maisha ya wananchi na kuanzisha miradi ya kijamii.
Kutokana na nchi hiyo kuwa na watu wengi ardhi imekuwa changamoto kubwa kiasi cha kukosa maeneo ya kujenga makazi na kuwalazimu kujenga maghorofa. Wingi wa viwanda pia umechangia changamoto hiyo, kutokana na ukweli kuwa China ina soko kubwa la bidhaa duniani hivyo inalazimika kufungua viwanda vingi kukidhi mahitaji ya wanunuzi.
Hali hiyo imeifanya nchi hiyo kutandaa katika mataifa mengine duniani hasa yale ya Afrika kutafuta ardhi kujenga viwanda na miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Kuna sababu ya sisi kuamini kuwa ushirikiano na uwekezaji kati ya China na Tanzania utaendelea katika maeneo mengine. Tanzania ina uhakika wa kufurahia faida za uwekezaji wa China katika maendeleo ya kiuchumi na kupunguza umaskini”, – Balozi wa China nchini Tanzania Dkt. Lu Yuquing ambaye amemaliza muda wake.
Mpango huo wa China kutandaa katika nchi za Afrika umetajwa kama ni ukoloni mamboleo wa taifa hilo kwa nchi masikini ikidai kuwa inaendeleza sera za ujamaa ambazo msingi wake mkubwa ni kusaidiana katika nyanja za kiuchumi na kisiasa.
Lakini wachambuzi wa diplomasia za kimataifa wanautilia shaka uwekezaji unaofanywa na China katika mataifa ya Afrika, kuwa haulengi kulinufaisha bara hilo zaidi ya kuchukua rasilimali muhimu ili kujiimarisha kiuchumi na kuwa taifa lenye nguvu duniani.
Kwa hoja hiyo, Afrika kwa sehemu inanufaika na misaada ya China lakini si kwa kiwango kinachotakiwa, ikilinganishwa na rasilimali zinazochukuliwa na taifa hilo.Katika kuendeleza kile kinachoitwa kuzikwamua nchi za Afrika, taifa hilo limeimarisha nguvu zake katika nchi yetu Tanzania ambayo imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za gesi, mafuta, madini, ardhi yenye rutuba, mbuga za wanyama na rasilimali watu.
Ushirikiano wa China na Tanzania ulianza mwaka 1965 wakati huo nchi yetu ilikuwa inafuata siasa ya ujamaa na kujitegemea. Wakati huu ushirikiano baina ya nchi hizi mbili uliimarika zaidi kutokana na uwekezaji na misaada iliyotolewa na China, ambapo sasa ushirikiano huo umefika katika nyanja za afya, elimu, usambazaji wa maji, nishati, madini, huduma za serikali, rasilimali watu, biashara, viwanda, miundombinu na usafiri.
Mwaka 1970, wakati serikali ya China ikiwa katika umaskini mkubwa, iliisaidia Tanzania na Zambia kujenga reli ya TAZARA ambayo inaunganisha mataifa hayo mawili. Zaidi ya wahandisi na wataalamu 50,000 kutoka China walitumwa kutengeneza reli hiyo na wafanyakazi 69 walikufa na kuzikwa katika makaburi ya kumbukumbu ya China jijini Dar es salaam.
Pamoja na changamoto hizo, ushirikiano huo ulizidi kuimarika hasa katika awamu ya nne ya uongozi wa rais Jakaya Kikwete, ambapo mwaka 2013 rais wa China, Xi Jinping alifanya ziara ya kiserikali kuendeleza ushirikiano uliopo na kuzindua mpango mkakati wa ‘win-win result’ ambao ulilenga kuyavutia makampuni ya China kuwekeza nchini ili kuendeleza rasilimali zilizopo katika maeneo mbalimbali ya nchi.
China imefanikiwa kujenga Kituo cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNIC), Uwanja wa Taifa, Mradi wa usambazaji maji wa Charinze, Kituo cha kutibu magonjwa ya moyo na mafunzo katika hospitali ya Muhimbili, Shule nne za msingi (4 Sino-Africa Friendship Primary schoool). Pia wamefanikiwa kutengeneza umeme na taa za barabarani zinazotumia nishati ya jua.
Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere uliojengwa kwa msaada wa serikali ya China
Serikali ya China iliikopesha serikali ya Tanzania Dola za Kimarekani bilioni 2 kutekeleza miradi mbalimbali ukiwemo Ujenzi wa Mkongo wa Taifa ambao utaboresha sekta ya mawasiliano katika nchi za Afrika Mashariki; bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es salaam; ujenzi wa nyumba za Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Anasema tangu mradi wa kujenga Mkongo wa Taifa uanze mwaka 2009, mradi umetengeneza faida ya Dola za Kimarekani milioni 40 na kuajiri wafanyakazi 800 and kuwaandaa wataalamu 200 katika teknolojia ya mawasiliano (ICT) kusimamia shughuli za mokongo huo.
Pia China ilitoa Dola za Kimarekani milioni 412.5 kufanikisha ujenzi wa Bandari Kavu eneo la Kurasini katika Wilaya ya Temeke ili kupunguza mlundikano wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam.
Mwaka 2013 pekee China imewekeza zaidi ya Dola bilioni 2.17 katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania ikiwemo sekta za uzalishaji, uchukuzi, nishati, madini, usafiri, mawasiliano na utalii.
Miradi ambayo inatekelezwa kwa ushirikiano wanchi hizo mbili ni pamoja na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, Kituo cha uzalishaji umeme wa gesi cha Kinyerezi ambacho kiko katika hatua ya III na IV na kinagharimu Dola bilioni 1.
Pia mahusiano ya kibiashara pia yameimarika hasa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ambapo mwaka 2011 na 2012 biashara ilikuwa ni Dola bilioni 2.1 na bilioni 2.5, na inakisiwa biashara baina ya mataifa hayo mawili itaongezeka zaidi miaka ijayo.
Katika soko la ujenzi,zaidi ya asilimia 70 ya miradi ya barabara na madaraja imejengwa na makampuni ya China. Ni teknolojia yao iliyotukuka na bei nzuri inayolingana na mahitaji ya Watanzania ndio inayofanya makampuni kupata zabuni nchini. Kutokana na hali hiyo kampuni hizo zimeisaidia Tanzania kuokoa zaidi ya asilimia 20 ya miradi yote ya uwekezaji.
Ni dhahiri kuwa China imejiimarisha katika nchi yetu, na wasiwasi wangu ni mikopo tuliyochukua ili kukamilisha miradi ya maendeleo, je tunauwezo wa kuilipa kwa wakati ikizingatiwa kuwa deni la nje nalo linakuwa kwa kasi ambapo kati ya Julai 2016 hadi Julai 2017 limeongezeka mpaka Dola bilioni 1.5 na deni la ndani ni bilioni 2.
Misaada tunayoipata kutoka China sio kitu kibaya lakini kama taifa hatuna budi kufanya tathmini ya kina ya rasilimali zetu tukilinganisha na mafanikio ya kiuchumi tunayayopata na hali ya raia mmoja mmoja, kuliko kuiweka nchi rehani kwa kukabidhi rasilimali muhimu kwa wageni.
Mafanikio ya kweli katika taifa yatapatikana ikiwa tutambua nafasi tuliyonayo katika kuendeleza rasilimali zetu na kukuza teknolojia yetu, na sio kama ilivyo sasa ya kukabidhi kila kitu kwa wawekezaji hata shughuli ndogo ndogo ambazo zinaweza kufanywa na raia wa wakaida.
Tunahitaji programu ya kitaifa ya kutufunza jinsi ya kuziendeleza rasilimali zetu na kujitegemea kwani ni kama tumejisahau sana hata viongozi wetu hawana dira ya kutuongoza kufika kule tuendako.