Utashi wa kisiasa kuinusuru Dar es Salaam dhidi ya uharibifu wa mazingira

Jamii Africa
Taarifa iliyotolewa na Benki Kuu imeonesha mikopo iliyotolewa kwa sekta binafsi imeongezeka kwa 1% tu mwaka wa fedha ulioisha Julai 2017 ikilinganishwa na 15.2% kwa mwaka wa fedha ulioishia Julai 2016. Pia sekta ya kilimo imeporomoka kwa -9.4% baada ya kuporomoka kwa -0.2% mwaka uliopita.

November 30 hadi Disemba 2, 2016 kule Mexico ulifanyika mkutano wa mwaka wa viongozi wa majiji makubwa duniani ujulikanao kama ‘C40 Mayor’s Summit’. Mkutano huo uliwakutanisha Mameya na viongozi kutoka katika majiji mbalimbali duniani yanayokuwa kwa kasi kiuchumi.

Mameya hao walikusanyika katika jiji la Mexico City katika mkutano wa 6 unaofanyika kila mwaka ambao ulilenga kujadili njia ambazo viongozi wa majiji hayo wanaweza kuzitumia kutatua viashiria na athari za mabadiliko ya tabia nchi katika nchi zao.

Mkutano huu uliwakutanisha viongozi wa serikali kutoka katika majiji 91, wakiwakilisha wananchi wa majiji hayo duniani kote kubadilishana uzoefu wa jinsi gani wanaweza kupunguza hewa ukaa itokanayo na ukuaji wa viwanda ili kulinda afya, ustawi wa watu waishio katika maeneo ya mijini. Pia mkutano huo uliangazia njia mbadala za kutunza mazingira ili kufikia Malengo ya  Maendeleo Endelevu (SDG’s)– 2030.

Kulingana ripoti ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (2017) inaonyesha kuwa katika mwaka 2015 pekee watu bilioni 4 ambao ni sawa asilimia 54 ya watu wote duniani walikuwa wanaishi katika maeneo ya mjini na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia watu bilioni 5 ifikapo 2030.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa ukuaji wa miji umeleta changamoto mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa makazi duni na holela, uchafuzi wa hewa, uhaba wa huduma za msingi na miundombinu ambapo inaiweka miji hiyo katika hatari ya kukumbwa na majanga.

Majiji hayo yanatoa asilimia 55 ya hewa ukaa yote inayotolewa na nchi zote duniani, na yanachangia asilimia 25 ya pato la dunia yaani GDP ambapo mtu 1 kati ya 12 anaishi katika majiji hayo.

Kundi la C40 lilianzishwa mwaka 2005 na sasa linajumuisha majiji 11 ya Afrika yanakuwa kwa kasi: Johannesburg, Cape Town, Dar es salaam, Addis Ababa, Nairobi, Cairo na Lagos, Dakar, Durban, Tshwane na Accra.

Mkutano huo ulishuhudia kutolewa kwa ripoti mpya ya Mkataba wa Paris juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa ambayo umejengwa katika tafiti zilizofanywa mwaka 2011 katika Mkutano wa C40 uliofanyika Sao Paulo Brazil.

Ripoti hiyo yenye kurasa 400 inatoa taarifa kwa viongozi wa serikali kujitathmini jinsi wanavyoendesha majiji yao, kwa kulinganisha na uzoefu wa majiji mengine yaliyofanikiwa ili kuwasaidia kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa.

“Wakati mazungumzo ya kimataifa yakiendelea kutafuta njia mbadala, majiji ya C40 yanaendelea mbele” alisema Meya wa zamani wa jiji la New York Michael Bloomberg ambaye pia ni Mwenyekiti wa bodi ya C40. “ Sisi kama wavumbuzi na wataalamu, majiji yetu yanahusika zaidi na suala hili ikiwa ni changamoto kubwa wakati huu”.

“C40’s inasisitiza katika vipimo na ripoti za kitaalamu zitakazosaidia majiji kutumia rasilimali na kutafuta njia inayofaa na ripoti hii inaonyesha kuwa juhudi zetu zinaleta matokeo ya kuridhisha” alisema Bloomberg akirejea ripoti ya utafiti uliofanywa 2011 na C40,

“Kwa kutumia taarifa hii jinsi inavyofanya kazi – na kipi kinawezekana, majiji yanaweza kuendesha mjadala wa kimataifa juu ya mabadiliko ya tabia nchi na hali joto na kuchangia katika kufikia malengo ya taifa katika kupunguza utoaji wa hewa ukaa”.

Mkutano huo ulikuwa ni muhimu kwani ni muendelezo wa juhudi za kimataifa za kupunguza athari za tabia nchi ambazo zinatishiwa na ongezeko kubwa la viwanda ambavyo hujengwa katika majiji makubwa, na kutoa hewa chafu ambayo huathiri mwenendo wa mvua, joto na afya za watu waishio katika maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Lakini jambo nyingine lilijitokeza katika mkutano huo, ni tathmini iliyofanywa na kugundua kuwa majiji ya Dar es salaam na Nairobi nchini Kenya ni moja ya majiji barani Afrika ambayo yanakuwa kwa kasi kiviwanda na kuwa na ongezeko kubwa la watu.

Majiji hayo mawili yanafuata nyuma ya majiji ya Lagos, Cape Town, Addis Ababa, Johannesburg na Cairo ambayo yanatajwa na mkutano huo kuwa ni majiji makubwa Afrika ambayo pia yanakabiliwa na changamoto nyingi za mabadiliko ya tabia nchi.

Jiji la Dar es salaam linakuwa kwa kasi na kuwa kitovu muhimu cha uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki ambapo idadi kubwa ya viwanda, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi zinaratibiwa na kuendeshwa katika jiji hilo.

Muonekano wa jiji la Dar es salaam

Changamoto kubwa ya jiji hilo ni ongezeko kubwa la watu ambalo haliendani na miundombinu iliyopo kwa maana ya barabara, maji, umeme, mpangilio wa makazi na huduma muhimu za kijamii.

Kutokana na ofisi nyingi za serikali kujengwa katika jiji hilo watu wengi hukimbia kutoka mikoa mingine na kuingia  Dar es salaam kila siku kufuata huduma muhimu ambazo hazipatikani katika mikoa yao.

Hali hiyo imesababisha kuwepo kwa makazi mengi yasiyo na mpangilio mzuri, adha ya usafiri na foleni kubwa za magari, ambayo husababishwa na kasi ndogo ya utanuzi wa barabara kuu na za pembezoni mwa jiji.

Kutokana na ukweli kuwa usafiri ni tatizo, ajali nyingi hutokea hasa za magari na bodaboda na kuchangia zaidi ya vifo 400 vinavyotokana na ajali kila mwaka.

Kwa mujibu wa takwimu za Kikosi Cha Usalama Barabarani nchini zinaeleza kuwa kuanzia Januari hadi Julai 2016, watu 1,580 wamekufa kutokana na ajali za barabarani, wengine 4,659 walijeruliwa katika ajali 5,152 zilizotokea nchi nzima. Kwa upande wa pikipiki waliokufa walikuwa 430,, waliojeruliwa 1,147 katika ajali 1,356.

Muonekano wa jiji hilo sio wa kuvutia hasa katika utunzaji wa mazingira, maeneo mengi ni machafu yakiwa na miundombinu mibovu ya maji taka, makazi duni, kuzagaa kwa chupa na mifuko ya plastiki katika mitaa.

 Takwimu za mtandao wa SoapBoxies (2016) unaoangazia utunzaji wa mazingira duniani, unaliweka jiji la Dar es salaam katika nafasi ya 12 miongoni mwa majiji 25 ambayo yanaongoza kwa uchafu duniani huku mipango mibovu ya usimamizi wa taka ikitajwa kama sababu inayosababisha hali hiyo. 

Inaelezwa kuwa ipo mipango mizuri ya kuboresha jiji hilo lakini inakwamishwa na mgongano wa maslahi ambao unasababishwa na utofauti wa kisiasa wa viongozi ikizingatiwa jiji hilo linaongozwa na Meya kutoka upinzani.

Isaya  Mwita, Meya wa jiji la Dar es salaam katika ripoti ya 2016 iliyowekwa kwenye tovuti ya C40 inaeleza mipango kutatua changamoto zilipo hasa mabadiliko ya hali hewa ambayo ni matokeo ya uwepo wa viwanda vingi vinatoa hewa ya ukaa. 

‘’Ili jiji letu liwe safi na kuwa sehemu nzuri ya kuishi, tutaimarisha juhudi za ukusanyaji taka, usafiri na kujenga vituo na maeneo ya kuhifadhi uchafu. Tutashirikiana na wadau, ili taka zitumike kuzalisha umeme wa gesi utakaotokana na taka zilizofukiwa chini ya ardhi. Mabadiliko hayo yataongeza mapato kutoka katika usimamizi wa taka na kuwa na uwezo wa kutengeneza mbolea kutokana na taka” inaeleza ripoti hiyo.

Lakini anasema suala hilo halizuii kutengeneza sera na miradi mbalimbali inayolenga kuliweka jiji hilo katika sura mpya. Katika kutatua changamoto ya usafiri, serikali inaendelea kutekeleza mradi mkubwa wa barabara za mabasi yaendayo kasi ambao unaratibiwa na Mabasi yaendayo haraka Dar Rapid Transit Agency (DART)” kwa udhamini wa Benki ya Dunia. Mradi huo umesaidia kupunguza foleni hasa kwa magari yanayotoka Kimara kuelekea katikati ya mji. 

Mradi wa mabasi yaendayo haraka (DART) ni miongoni mwa mikakati ya kupunguza foleni Dar es salaam

Ujenzi wa  barabara za pembezoni mwa jiji ambazo zitakuwa mbadala wa kupunguza foleni zisizokuwa za lazima. Pia mradi anuani za makazi ili kuwa na mpangilio mzuri wa jiji na utambulisho wa makazi unaendelea.

Sambamba na hilo ni kufunga kamera za video katika maeneo muhimu ya majengo na barabara kuu, ili kuchunguza mwenendo wa watu na shughuli za kiuchumi na kijamii kuhakikisha jiji linakuwa na usalama wakati wote.

Suala la usafi pia linapewa kipaumbele kuhakikisha jiji linavutia hasa kwa wageni ambapo mradi wa kukusanya taka ngumu na kuzibadilisha kuwa mbolea itakayotumiwa na wakulima na kutengenezea umeme kutoa nishati kwa wananchi uko katika mchakato muhimu.

Ofisi ya jiji inaendelea kutenga maeneo ambayo yatatumiwa kujenga miji ya mifano kama walivyofanya kwa mji wa Kigamboni ambao umeanza kujengwa na ukikamilika utalipatia jiji mapato kwasababu utakuwa kivutio kikubwa kwa watalii.

Kulibadilisha jiji la Dar es salaam katika muonekano wa aina yake kama yalivyo majiji mengine duniani inawezekana, kinachohitajika ni uwajibikaji na uwazi wa viongozi wakishirikiana na wananchi katika maamuzi muhimu ya kuliendeleza jiji hilo linalokuwa kwa kasi barani Afrika.

Licha ya changamoto hizo bado jiji hilo limeendelea kujipatia sifa mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa kuwa na bandari inayohudumia mataifa ya Afrika Mashariki na kuwa kiungo muhimu cha biashara za kimataifa ambazo hufanywa Kusini mwa jangwa la Sahara.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *