Uchaguzi wa Igunga na juhudi za kukandamiza upigaji kura

Jamii Africa

Uchaguzi mdogo wa ubunge huko Igunga utaamuliwa kwa namba. Utaamuliwa kwa idadi ya watu watakaojitokeza kupiga kura na siyo watu wanaojitokeza leo hii kwenye mikutano ya kampeni. Utaamuliwa na watu ambao wataamua kuacha shughuli zao siku hiyo na kwenda kutumbukiza karatasi moja kwenye sanduku la kura. Kuanzia mwanzoni mwa wiki hii inayoisha nimekuwa nikujiulzia ni kitu gani kitawapa wapinzani ushindi na ni kitu gani kitawarudishia CCM ushindi. Jibu ni lile lile – namba.

Nimejiuliza mwanzoni mwa wiki kwanini CCM imejikuta ikidaiwa kufanya vitu vile vile tulivyovisikia huko nyuma – kuulizia ni nani kajiandikisha kupiga kura. Kwa watu wengi hili linaonekana kama njia ya “kuiba kura” lakini kwa mtu yeyote anayetengeneza mikakati ya ushindi ya uchaguzi ni muhimu sana kujua nani kajiandikisha kupiga kura. Kuna maswali muhimu ambayo mpanga mikakati yeyote ya uchaguzi (political strategist) anajiuliza mapema.

a. Watu wangapi wamejiandikisha kupiga kura kwenye jimbo au eneo linalogombewa?
b. Kati ya waliojiandikisha ni wangapi wanachama wa chama chako?
c. Kati ya wanachama wako waliojiandikisha ni wangapi wanapanga kupiga kura siku ya uchaguzi?
d. Ni wangapi wanapanga kumpigia kura mgombea wa chama chako?

Maswali haya manne ni muhimu sana kwa uchaguzi wowote wenye kuhusisha chama zaidi ya kimoja au zaidi ya mgombea mmoja. Lengo la kutaka majibu kwenye maswali haya ni kutaka hasa kujua mwelekeo wa wapiga kura siku ya uchaguzi ukoje kwa kadiri chama chako kinahusiska. Kwa mfano, kama watu wengi sana wamejiandikisha kupiga kura na kati yao wengi wanapanga kupiga kura siku hiyo ya uchaguzi basi mwanamkakati wetu atatakiwa kufanya juhudi kubwa sana ya kutaka kujua kati ya hao ni wangapi ambao ni wanachama wa chama chake. Hivyo, juhudi kubwa itawekwa kwenye kuhamasisha wanachama kujitokeza zaidi kupiga kura – kama wamejiandikisha kwa wingi.

Kwa mfano, kwenye uchaguzi ambapo watu 100,000 wamejiandikisha kupiga kura, utafiti unaonesha kuwa karibu 60,000 ni wanachama wa chama kimoja. Sasa Chama kinahitaji kujua kati ya hao 60,000 ambao ni sawa na asilimia 60 waliojiandikisha kupiga kura ni wangapi kati yao wanapanga kupiga kura siku hiyo. Lengo ni kujaribu kuhamasisha kwa kadiri inavyowezekana wanachama kujitokeza kupiga kura. kama asilimia hamsini tu watajitokeza kupiga kura ina maana ya kuwa vyama vingine vitagawana kura zilizobakia.

Lakini kuna lengo la pili vile vile la kutaka kujua idadi hizi. Lengo pia huwa katika kile kinachojulikana kama voters suppresion – yaani kugandamiza upigaji kura. Kama chama chenye nguvu/tawala kinaona kuwa kinaweza kikapoteza kura endapo wapiga kura wengi watajitokeza basi mbinu hutafutwa za kugandamiza upigaji kura. Katika uchaguzi wa mwaka jana nilikuwa miongoni mwa watu wachache tulioweza kuonesha kuwa CCM ingeweza kushinda uchaguzi endapo kungekuwa na ugandamizaji kura. Siyo kusudio langu hasa kuanisha mbinu mbalimbali zinazotumika duniani kugandamiza kupiga kura. Lakini ni muhimu kutambua kuwa mbinu kubwa iliyotumika ni kuhakikisha kuwa wengi waliojiandikisha kupiga kura hawajitokezi kupiga kura.

Mbinu kama vitisho (umwagikaji damu, jeshi, n.k) zinatumika kuwafanya watu wahofie kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi. Mbinu za kutisha watu zilifanikiwa sana kuhakikisha kuwa katika historia ya Tanzania mwaka jana ndio watu wachache zaidi walijitokea kupiga kura. Tangu uhuru hatujawahi kuwa na chini ya asilimia 69 (wastani ni asilimia 70) ya waliojiandikisha kupiga kura kupiga kura. Mwaka jana ilikuwa chini ya asilimia 45. Niliandika wakati ule kuwa kama upigaji kura utakuwa chini ya asilimia 70 CCM itashinda.

Lakini kwa vyama vya siasa pia ni muhimu kupata picha ya kundi la wapiga kura ili kujua ni ujumbe gani unataka kuufikisha wakati wa kampeni. Kama katika kufanya utafiti chama kinagundua kuwa wapiga kura wake wengi wako mjini, ni wanaume, na wana kazi rasmi ujumbe wao ni lazima utakuwa ni tofauti zaidi wa kuwahamasisha. Huwezi kwenda kuwahubiria wafanyakazi wa maofisini sera za kilimo! Hawa watapenda kujua kuhusu haki za kazi, pensheni, usalama kazini, mafao mbalimbali n.k Lakini vile vile unapoenda kuhutubia kwenye maeneo ya vijijini ambako wafanyakazi wake wengi ni wenye ajira binafsi au wakulima wa kujishikiza ujumbe wako kwao utakuwa tofauti vile vile. Hawa labda watahitaji kujua zaidi mipango mbalimbali ya kuboresha kilimo, afya ya msingi, elimu n.k

Hivyo basi utaona kuwa japo kwa baadhi ya watu wanaweza kushtuka kuona chama kinafuatilia kujua nani kajiandikisha kupiga kura na nani mwanachama – mbinu ambazo binafsi ninaamini zinakubalika kisiasa kama hazihusishi wizi, vitisho au geresha ya aina fulani – ukweli ni kuwa hii ni mbinu ya kisiasa ya uchaguzi na wakati umefika kwa vyama vya upinzani navyo kujua mapema namna ya kuzitumia. CCM inafanya kile ambacho hakikatazwi kisheria – kwa kadiri nijuavyo. Upinzani unahitaji kujua jinsi ya kuhamasisha kujiandikisha; kujua idadi ya wanachama wake waliojiandikisha, na vile vile kuweza kufahamu ni kiasi gani kati yao wana uwezekano wa kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi.

Bila kupata majibu ya maswali haya na hasa kwenye mfumo wetu ambapo wapiga kura wote watakaopiga kura kwenye uchaguzi huu mdogo ni wale tu waliojiandikisha mwaka jana basi kazi ya kushinda uchaguzi kwa chama kama CDM, CUF au NCCR haviwezi kuwa rahisi kama inavyodhaniwa. Vyama hivi vya upinzani vina kazi kubwa kubwa ya kuweza kupata kura za wanaCCM hasa ukizingatia kuwa kwenye uchaguzi wa mwaka jana CCM ilipata kura 35,674 wakati CUF ilipata kura 11,321. 

Kwa upinzani kushinda Igunda ni lazima igeuze hizo namba zilizokwenda CCM wakati kwa upande wa CCM inahitaji kura kidogo kutoka upinzani kuweza kuziba jaribio lolote la kuangushwa. Kama ilivyotokea kwenye uchaguzi wa Rais ni ishara kuna uwezekano mkubwa wa kura nyingi za CUF zikaenda kumpa nguvu kura za CCM na hivyo kupunguza athari yoyote ya kura za CCM kupungua kutokana na hasira za kuondoka kwa Rostam.

Lakini namba hizi mbili hazina maana kubwa bila kujua idadi ya waliojiandikisha kura Igunga. Ni idadi hiyo kwa kweli ndio itakayoamua ni nani atakuwa mshindi kwani kama wanachama wengi walioiunga mkono CHADEMA mwaka jana hawakupata nafasi ya kupiga kura (kwa sababu hakukuwa na mgombea wa CDM) basi watu hawa wanaweza kujitokeza zaidi safari hii kwani mgombea “wao” amepatikana. Swali kubwa ni kiasi gani cha waliopigia kura CCM na CUF mwaka jana watahama na kwenda kuipigia kura CDM?

Idadi hiyo ni ipi?

Kwa mujibu wa vyanzo vyangu vya kuaminika watu waliojiandikisha kupiga kura mwaka jana huko Igunga ni 170,586. Hii ni idadi kubwa sana. Lakini kwa kuiangalia idadi hii na kulinganisha na watu waliojitokeza kupiga kura mwaka jana ni rahisi kwa namna fulani kuweza kutabiri mwelekeo wa uchaguzi mdogo wa Igunga kwa kuangalia namba. Kama mwanamkakati wa kisiasa  kuna vitu naweza kuvisema kwa uhakika kuhusu nani ataelekea kushinda. Lakini hebu tuangalia hizi namba kwa ukaribu kidogo.

– Waliojiandikisha kupiga kura mwaka jana = 170, 586
– Walioipigia kura CCM = 35,674
– Walioipigia kura CUF =  11, 321
– Kura zilizoharibika = 2018
– Jumla ya kura zilizopigwa = 49,013.

Hivyo: Waliopiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana kwenye kura za wabunge ni asilimia 28.73 ya wale waliojiandikisha kupiga kura. Kwa maneno mengine asilimia 71 ya waliojiandikisha kupiga kura hawakujitokeza kupiga kura (hii ni karibu kabisa na theluthi mbili ya wapiga kura waliojiandikisha).

Kwa kulinganisha kidogo tunaweza kuona kuwa kura za Urais za Igunga kati ya wagombea 7 ambao majina yao yalikuwepo kwenye karatasi ya kura mgombea wa CCM alipata kura: 24,945, wa CUF= 7,355, CHADEMA =6,815 na wagombea wengine 521. Jumla ya kura zote pamoja na zilizoharibika zilikuwa 40,412. Hivyo, waliojitokeza kupiga kura za urais ni sawa na asilimia 23.69 ya wale waliojiandikisha kupiga kura.

Namba hizi zinatuonesha vitu kadhaa:

1. Karibu watu 10,000 walioenda kupiga kura za wabunge hawakupiga kura za Rais.
2. Mgombea wa Urais wa CCM alipoteza kura 10,729 kulinganisha na kura alizopata mgombea wa Ubunge wa CCM
3. Mgombea wa Urais wa CUF alipoteza kura 3966 kulinganisha na kura alizopata mgombea wa Ubunge wa CUF
4. Mgombea wa Urais wa CHADEMA alipata kura 6,815

Swali hapa la msingi ni kukosekana kwa mgombea wa Ubunge wa CHADEMA kule Igunga kuliathiri kwa kiasi gani kura za mgombea wa Urais hasa tukiangalia jinsi ambavyo matokeo ya ubunge ya CCM na CUF yanavyoonekana kuwa juu ya yale ya Rais? Je yawezekana kama mwelekeo huo ungeendelea yawezekana mgombea Ubunge wa CDM angepata kura zaidi ya zile za Rais? Je kura alizopata Dr. Slaa ni sehemu ya kura ambazo Kikwete na LIpumba walinyimwa au zilikuwa ni kura za wale ambao walikuwa ni nje ya hao wapiga kura wa CCM na CUF? Kama ni hilo la pili, ni kwanini karibu watu elfu 13 ambao walipiga kura za Ubunge kwa vyama vyao hawakupigia kura urais wa vyama vyao?

Siri itakuwepo kwenye kuzuia watu kujitokeza kupiga kura
Ni wazi kabisa – angalau inapaswa kuwa wazi – kuweza kuona kuwa matokeo ya uchaguzi mdogo yatategemea sana upigaji kura. Hadi hivi sasa mojawapo ya taarifa ninazozisikia kutoka Igunga ni kuwa vituo vya kupigia kura viko mbalimbali sana kiasi kwamba inataka moyo kwa mtu kwenda kupiga kura. Hii yaweza kuwa ni mbinu ya “kijiografia” ya kugandamiza upigaji kura. Ni kitu gani kitamfanya mzee atembee maili moja au mbili au zaidi kwenda kupiga kura?

Katika hili vyama ni lazima vijipange kuhamasisha wanachama wake na mashibiki wake kujitokeza kupiga kura na kujitolea usafiri wa kupelekana kwenda kupiga kura na kurudi. Sheria ya Uchaguzi (ambayo niliibeza tangu ilipoanza kufikiria na kuja kupitishwa) inakataza watu kukodisha magari kwa ajili ya kupeleka watu na kuwarudisha kutoka vituo vya kupigia kura (Ibara 23:3,4). Lakini sheria hiyo hiyo (ibara ya 23:5) inaruhusu wapiga kura wenyewe kwa kutumia gharama zao wenyewe (joint cost) kusaidia kupelekana kwenye vituo vya kupigia kura na kurudisha. Lakini vile vile sheria hiyo inatoa jukumu kwa serikali kuhakikisha kuwa usafiri unakuwepo kwa wale wote (bila kujali vyama au siasa) wanaotaka kufika mahali pa kupigia kura endapo kutokana na sababu mbalimbali vituo vya kupigia kura viko mbali na makazi yao.

Hii ina maana ya kwamba, hoja ya kuwa watu hawakuweza kufika kwenye maeneo ya kupigia kura kwa sababu ya umbali, mto au daraka haina nguvu kwani vyama vinatakiwa vipange na sreikali na kuhamasisha wanachama wao kujipatia usafiri wao kwenda vituo vya kupigia kura. Kwa vile haki ya kupiga kura ni haki ya msingi ni muhimu wananchi watambue kuwa serikali inaweza kukodi au kuhakikisha kuwa mabasi na vyombo vya usafiri vinakuwepo kwa watu wanaotaka kupiga kura.

Kwa ufupi ni kuwa matokeo ya uchaguzi mdogo wa Igunga yatategemea sana hisabati na jinsi namba zinavyoweza kutumika. Tuangalie wiki moja iliyobakia kuweza kuona ni kwa kiasi gani kura zinagandamizwa na ni kwa kiasi gani watu wanajipanga kujitokeza kupiga kura au kusaidiwa kujitokeza kupiga kura ili watu wasiwe na udhuru. Upinzani utafanya vizuri endapo watu wengi watajitokeza kupiga kura na CCM itafanya vizuri kama watu wachache watajitokeza kupiga kura.

Imeandikwa na M. M. Mwanakijiji

3 Comments
  • Kwa mtu yeyote aliyekomaa kiakili akisoma habari zenye uchambuzi wa kitakwimu kama huu, lazima akupe sifa ndg yangu Mwanakijiji. Huwa nafarijika sana na kupata habari za uhakika nikisoma makara zako siku zote. Hongera kwa uwezo wa kipekee wa kifikra.

  • Haiwezekani watu 10,000 wakampigia kura mbunge halafu wakasahau au wakakataa au wakaharibu kura za rais na ukizingatia kuwa vyama vyenye wagombea ubunge waliopata kura nyingi walikuwa na mgombea rais. Lazima huu ulikuwa ni mkakati. Ama walikubaliana wasimpigie kura rais (I really doubt this) au ni kura za kupikwa.

    Lakini lingine ni kwamba kulikuwa pia kuna kura za madiwani. Diwani wa Igunga kwenye wapiga kura 22,000 ni wa CHADEMA. Hivyo ni vizuri your analysis to take into account kura za udiwani ili kupata picha kamili. Hao waliomchagua diwani wa CHADEMA walimpigia kura nani? CUF au CCM? Je Diwani wa CHADEMA alipata kura nyingi kuliko mgombea ubunge wa CUF??????

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *