Sera ya Maji ya mwaka 2002 inabainisha kuwa “Maji ni muhimu kwa viumbe vyote duniani, bila maji hakuna uhai. Aidha maji ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kiwango cha maendeleo ya jamii yoyote kinategemea kuwepo kwa maji ya kutosha na yenye ubora unaotakiwa. Katika hali yake ya asili, maji ni sehemu ya mazingira ambapo wingi na ubora wake ndio unaosaidia katika kuamua jinsi maji yatakavyotumika”.
Lakini hali imekuwa tofauti na matarajio ya sera hiyo, ambapo mahitaji ya maji yameongezeka nchini kutokana na ongezeko kubwa la watu na shughuli za kiuchumi na kijamii ambazo zinatumia maji kwa wingi.
Ripoti ya Benki ya Dunia (2017) juu ya Usimamizi Mzuri wa Maji inaeleza kuwa kwa miaka 25 iliyopita idadi ya watu waliopo Tanzania imeongezeka mara dufu, kiwango cha uchumi kimeongezeka zaidi ya mara tatu lakini upatikanaji wa maji hauendani na ongezeko hilo. Matokeo yake vyanzo vya maji vimepungua kwa zaidi ya mita za ujazo 1,700 ikiwa na maana kuwa Tanzania imeungana na nchi nyingine duniani zenye mahitaji makubwa ya maji.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa mahitaji ya maji duniani ni makubwa wakati wa kipindi cha ukame na maeneo ya nchi yanayokabiliwa na tatizo la ukame. Mvua nyingi zinanyesha miezi 2 hadi 3 kwa mwaka na baada ya kutathmini mtiririko wa mahitaji ya mazingira, Tanzania ina mahitaji ya maji yanayofikia asilimia 150 wakati wa kipindi ukame.
Upungufu huu unaathiri uzalishaji wa chakula na umeme na kusababisha uharibifu wa mazingira, hali inayoleta migogoro na ushindani wa kutumia maji miongoni mwa sekta mbalimbali za kijamii na zile za kiuchumi.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Greyson Lwenge wakati akisoma hotuba ya bajeti 2017/2018 alibainisha kuwa “usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji nchini unafuata taratibu za usimamizi shirikishi wa rasilimali za maji kupitia Bodi za Maji za Mabonde tisa yaliyopo nchini, ambapo mabonde saba kati ya hayo yanahusisha maji shirikishi kati ya nchi yetu na nchi jirani.
“Kutokana na rasilimali hizo za maji, takwimu zilizopo zinaonesha kuwa maji yanayofaa kwa matumizi mbalimbali ni kilomita za ujazo 96.27 na kila mwananchi ana uwezo wa kupata maji wastani wa mita za ujazo 1,800 kwa mwaka. Aidha, kiwango cha chini cha mahitaji ya maji kwa kila mtu kwa mwaka kinachokubalika kimataifa ni mita za ujazo 1,700. Iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa, kiwango hicho kitapungua hadi kufikia mita za ujazo 883 katika mwaka 2035”.
Upungufu huo wa maji unatishia ukuaji wa viwanda na majiji kama Dar es Salaam ambalo ni kitovu cha shughuli za kiuchumi na viwanda nchini. Kwa muda mrefu sasa Dar es Salaam imekuwa na tatizo la uhaba wa maji licha ya ahadi za kisiasa za kumaliza tatizo hilo ambalo limekuwa kikwazo katika ukuaji wa uchumi.
Inaelezwa kuwa katika majiji ya Tanzania usambazaji wa maji wa uhakika ni changamoto katika ukuaji wa viwanda hasa kipindi cha ukame. Benki ya Dunia inaeleza kuwa uzalishaji wa bia ni miongoni mwa viwanda vikubwa nchini na soko lake linakuwa. Lakini mwaka 2015 kwasababu ya uhaba wa maji ilizuia juhudi za Kampuni ya Bia kujitanua katika jiji la Mbeya. Kampuni hiyo ilisitisha mipango yake ya kujenga kiwanda hicho kwasababu ya kutokuwa na uhakika wa upatikanaji wa vyanzo vya maji.
Hata hivyo, viwanda vilivyopo Dar es Salaam vinatishia kupotea kwa vyanzo vya maji kutokana na mifumo mibovu ya majitaka na uharibifu wa mazingira hasa utiririshaji wa taka sumu na maji machafu kuelekezwa katika mito na vyanzo vya maji.
Katika ripoti ya Viwanda ya mwaka 2013, inaonyesha kuwa Tanzania ilikuwa na viwanda 49,243, ambapo asilimia 85.13 ni vidogo sana, 14.02% viwanda vidogo, 0.35% vya kati na 0.5% vikubwa. Serikali bado inaendelea kutengeneza mazingira ya kuanzisha viwanda vingi zaidi hasa katika miji mikubwa.
Sera ya viwanda ni muhimu ikajikita kuandaa mipango endelevu ya kutunza mazingira na kuhakikisha kunakuwa na mifumo imara ya kusimamia maji taka na kuyawekea utaratibu mzuri wa kutumika tena ili maji yanayozalishwa yatumike katika viwanda.
Uwekezaji katika miradi ya maji yanayotumika katika viwanda unapwa kuangaliwa upya ili kuenda sambamba na mahitaji ya viwanda vinavyojenga.