ACFTA: Pambazuko jipya la Afrika ‘ Tuitakayo’

Jamii Africa

Mnamo tarehe 21 mwezi wa tatu mwaka huu Afrika iliweka historia kwa viongozi wa Afrika kutia sahihi ya kuwa na soko huru la Afrika. Viongozi kutoka nchi 44 na zaidi walikutana Kigali Rwanda kutia sahihi na makubaliano ya kuwa na soko huru la Afrika litakaloruhusu uhuru wa mzunguko wa bidhaa na uhuru wa watu kufanya biashara.

Nchi takribani 10 barani Afrika hazikutia sahihi makubaliano hayo ikiwamo Nigeria na Afrika Kusini. Nchi hizi bado zinasema zinaendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali juu ya uamuzi huu kabla ya kufika makubaliano ya kujiunga ama la.

The African Continent Free Trade Area (ACFTA) kama inavyojulikana katika lugha ya kigeni inatarajiwa kuanza kazi ndani ya miezi sita kuanzia sasa. Lengo kubwa la soko huru hili la Afrika ni pamoja na kuondoa vikwazo vya kufanya biashara kama ushuru na kuagiza bidhaa kwa upendeleo. Hii itaruhusu nchi wanachama kupitisha bidhaa na huduma kwa uhuru.

Hatua hii kwa maoni yangu ni hatua ya kupongezwa kwani inaashiria mwanzo mzuri kwa bara la Afrika katika kufanya maamuzi yenye tija.  Hatua hii kwa maoni ya watu wengine inaonekana haitofanikiwa kwa kuwa Afrika bado ina chanamoto nyingi ikiwemo vita, uchumi dhaifu, viwanda vichache na uuzaji wa bidhaa ghafi katika nchi za magharibi.

Kwa muda mrefu Afrika imekuwa msitu wa uvunaji wa mabepari (nchi za Magharibi) ambao hutajirika kwa rasilimali za bara hilo. Hii yote imewezekana kwa kuwekewa vikwazo na masharti mengi ambayo yalipewa jina la soko la dunia ambalo lilihodhiwa na mabepari hao.

Afrika ina watu takribani bilioni 1.2 ambao wana uwezo mzuri wa kuliendeleza bara lao. Kasumba imejengwa kuwa maendeleo ya Afrika hayawezi kupatikana bila kuwa na wawekezaji kutoka nchi za magharibi ambao wana ujuzi na mitaji.

Hatua hii ya kuanzisha soko huru la Afrika ni dhahiri sasa tutapata fursa ya kufanya biashara baina ya nchi wanachama na pia kupata wawekezaji wa Afrika wenye ujuzi na teknolijia ambao watasaidia kuinua uchumi na maisha ya wananchi wa nchi moja moja.

Jambo la kusikitisha ni kwamba, takwimu za Jukwaa la Uchumi la Dunia (Word Economic Forum) zinaonyesha  kuwa ndani ya Afrika mzunguko wa biashara ni asilimia 16 tu wakati nchi za Asia (71%) na Umoja wa Ulaya (52%).

Hii inaonesha dhairi kuwa Afrika inasafirisha zaidi malighafi kwenda nje ya bara hilo kuliko inavyojiuzia yenyewe na kutengeneza bidhaa zilizokamilika ambapo ni changamoto katika ukuaji wa uchumi.

Wasiwasi wa baadhi ya watu ni kwamba soko huru la Afrika litafanikiwa ili hali kuna changamoto nyingi ambazo bado hazijatatuliwa kama vile ukosefu wa miundombinu, umeme wa uhakika, ujuzi, elimu bora na teknolijia ya kisasa.

Watu wengine wanahoji ni baada ya muda gani hasa utekelezaji halisi utaaanza? Kama Nigeria ambayo ina watu wengi na uchumi imara bado haijaridhia makubaliano hayo, kweli soko huru litafanikiwa?

Nadhani ni muhimu kutambua ya kuwa ni vyema kuwa na dhamira sahihi na kuanza kujikwamua kama bara kwani hakuna wa kutusaidia kama sio waafrika wenyewe kuamua kusimama kidete kupigania uhuru wetu wa kiuchumi na kifikra.

Mathalani, Umoja wa Ulaya (EU) ambao ulianza mwaka 1957. Waasisi wa Jumuiya ya Ulaya walikuwa sita tu ambao ni Ubelgiji, Ufaransa, Italia, Luxembourg, Netherlands na Ujerumani Magharibi. Soko huru rasmi lilifanikiwa miaka takribani 37 baadae ambapo mwaka 1993 ndipo lilianza rasmi na ndipo walipoongeza wanachama wengine 15.

Nia thabiti ndio jambo muhimu katika kupata uhuru wa uchumi haijalishi itachukua miaka mingapi kufanikiwa ila kuna ramani tayari inayotoa mwanga katika kile ambacho Afrika inataka kukifikia.

Ni ukweli ulio wazi ya kuwa, soko huru la Afrika litapitia vikwazo na misukosuko mingi kutoka kwa nchi zilizoendelea ambazo kwa muda mrefu zinatawala soko la bidhaa duniani.   

Kwa kuhitimisha, kwenye kitabu cha How the West Was Lost kilichoandikwa na Dambisa Moyo kimeeleza wazi ya kuwa mwisho wa karne hii nchi nyingi duniani zitakuwa zimepiga hatua kubwa ya maendeleo hivyo nchi za Magharibi hazitakuwa na uwezo tena kutawala uchumi wa dunia.

Soko huru la Afrika litaipatia nguvu Afrika kiuchumi ya kuamua itakacho na pia bara halitahitaji tena misaada kutoka nchi za Magharibi kwaajili ya maendeleo. Hapa ndio utakuwa mwisho wa udhalimu, vitisho, vikwazo na mikopo yenye masharti magumu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *