Watu 16 wamefariki dunia na wengine kujeruhiwa katika ajali ya basi mkoani Geita wakati mabasi ya Sheratoni na Bunda yalipogongana. Basi la Sheratoni lilikuwa likitoka Biharamulo kwenda Bukombe wakati lile la Bunda lilikuwa likitoka Musoma kwenda Bukoba; ajali imetokea eneo la Kibingo kata ya Nyamigota mkoani Geita. Idadi ya waliokufa inaweza kuongezeka wakati wowote.
Maiti chache tayari zimeshatambuliwa huku baadhi ya majeruhi wakiwa wameruhusiwa kutoka hospitali.
Hii ni ajali nyingine ndani ya siku chache ambayo inalishtua taifa baada ya ajali mbaya iliyotokea huko Kimara mwishoni mwa Juma lililopita ambapo watu watatu walikufa hapo hapo akiwemo mmoja wa watunzi na waigizaji wa filamu mbalimbali nchini. Mlolongo wa ajali za vyombo vya usafiri nchini umekuwa ukitokea mara kwa mara ikiwa ni ishara ya serikali kushindwa kulipatia utatuzi wa kudumu vyanzo vya ajali hizo ambazo zimekuwa kama “kawaida” katika sehemu mbalimbali nchini.