Aliyebuni mashambulizi ya Balozi za Marekani 1998 auawa

Jamii Africa

Mhusika mkuu wa kupanga ulipuaji wa balozi za Marekani huko Nairobi Kenya  na Dar-es-Salaam, Tanzania imeripotiwa ameuawa huko Somalia Jumatano iliyopita. Fazul Abdullah Mohammed ndiye mtu aliyekuwa anatafutwa sana Afrika baada ya milipuko ile ya Augusti 8, 1998 ambayo ilisababisha vifo vya watu 220 na mamia wengine kujeruhiwa wakati magari yaliyojaa mabomu yalipolipuliwa katika malango ya balozi hizo.

Tukio hilo lilikuja baadaye kuhusishwa na kikundi cha kighaidi cha Al-Qaida  na lilikuwa ni tukio kubwa la mashambulizi dhidi ya maslahi ya Marekani kabla ya mashambulizi ya kikundi hicho Septemba 11, 2001 huko Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo vya usalama vya Kenya Bw. Mohammed aliuawa huko Mogadishu Somalia na uchunguzI wa vinasaba vyake (DNA) unafanywa ili kuthibitisha kifo hicho. Hili litakuwa ni pigo jingine kwa kikundi cha Al-Qaida hasa baada ya kuuawa kwa kiongozi wake Osama bin Laden wiki chache zilizopita na kufuatiwa kwa kuuawa kwa kiongozi mwingine wa Al-Qaida huko huko Pakistani.

Fazul Mohammed ndiye aliyesadikiwa kuwa ni kiongozi wa kikundi hicho cha Al-Qaida katika Afrika ya Mashariki akiwa kama Operesheni Kamanda mojawapo ya ngazi za juu katika kikundi hicho akiwa na uwezo wa kupanga na kutekekeleza mashambulizi mbalimbali. Hata hivyo, kiongozi wa kikundi cha Al-Shabaab cha Somalia ameiambia Associated Press kuwa Bw. Fazul hajauawa. Mara kwa mara baadhi ya taarifa za kuuawa viongozi wa maghaidi zimekuja kuthibitishwa baadaye kuwa hazikuwa sahihi.

Washington bado hawajathibitisha kama ni kweli Fazul Mohammed ameuawa. Serikali ya Marekani iliweka dau la zaidi ya shilingi bilioni 5 kwa yeyote ambaye angewezesha kupatikana kwa Fazul Mohammed. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alikataa kuthibitisha mauaji hayo au kuwa na taarifa za mauaji. Fazul Mohammed alishashtakiwa katika mahakama ya New York kwa kuhusika kwake na milipuko hiyo japo serikali ya Tanzania ilikuwa haijaleta mashtaka yoyote nchini dhidi yake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *