UTARATIBU wa kituo cha afya cha Idodi, wilayani Iringa wa kukodisha gari lake la kubeba wagonjwa kwa kati ya Sh 20,000 na Sh 70,000 umeelezwa kuwaumiza wananchi wa kijiji cha Kitisi.
Wakizungumza na gazeti hili hivikaribuni, wananchi hao walisema jambo linalosikitisha ni kuona hata wajawazito na watoto chini ya miaka mitano wanalazimika kutoa gharama hizo.
Mkazi mmoja wa kijiji hicho, Emanuel Mduda alisema wakati mke wake akijifungua mtoto wake wa pili alitumia Sh 70,000 kama gharama ya kumsafirisha hadi hospitali teule ya wilaya ya Iringa ya Tosamaganga.
“Alipokaribia kujifungua nilitumia saa moja kumfikisha katika zahanati ya Mapogoro iliyopo kilomita nane kutoka katika kijiji chetu; nilitumia usafiri wa baiskeli,” alisema.
Baada ya kumfikisha katika Zahanati hiyo, aliandikiwa rufaa ili apalekwe katika kituo cha afya cha Idodi kilichopo kilomita nane kutoka Mapogoro.
“Nilitumia Sh 20,000 kukodi ambalance hiyo na tulipofika Idodi mke wangu aliandikiwa rufaa tena ya kwenda hospitali teule ya wilaya ya Iringa ya Tosamaganga,” alisema.
Alisema alitumia Sh 50,000 kukodi gari hilo la wagonjwa kutoka Idodi hadi Tosamaganga na kuuliza dhana ya huduma bure kwa wajawazito na watoto ina maana gani.
Malalamiko ya Mduda yaliungwa mkono na Mwenyekiti wa kijiji cha Kitisi, Jonisia Pinda aliyesema huduma ya afya kwa wakazi zaidi ya 1,500 wa kijiji ni kero kubwa.
Hata hivyo alisema kijiji kimekamilisha ujenzi wa Zahanati yake ambayo haijaanza kufanya kazi kwasababu haina watoa huduma.
“Hivi sasa tunaendelea na ujenzi wa nyumba moja ya mganga; hata hivyo ujenzi wake umekwama kwasababu hatuna fedha,” alisema.
Ili kukamilisha ujenzi wa nyumba hiyo ya mganga, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mkwawa Hunting Safari, Ahamed Huwel ameahidi kuchangia Sh Milioni tatu.
Huwel ambaye kampuni yake imepata kibali cha kuwekeza katika eno la Jumuiya ya Matumizi Bora ya Mali Hai Tarafa ya Idodi na Pawaga (MBOMIPA) alisema anaguswa na matatizo ya wananchi wa vijiji vinavyounda jumuiya hiyo inayopakana na hifadhi ya taifa ya Ruaha na ndio maana anawasaidia.
Kupandishwa kwa umeme sawa ila nashaur kwa sisi wananchi ubaki palepale