Uchimbaji wa Dhahabu kwenye Hifadhi unavyoharibu Mazingira

David Azaria

SHUGHULI za uchimbaji wa madini katika hifadhi ya Taifa ya Moyowosi wilayani Biharamulo Mkoani Kagera,zinadaiwa kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti katika hifadhi hiyo.

Uharibifu huo unafanyika katika hifadhi hiyo iliyopo katika kijiji cha Mavota Kata ya Kaniha wilayani biharamulo Mkoani Kagera,karibu na Mgodi wa Tulawaka.

Ofisa Maliasili wa wilaya ya Biharamulo Seleman Mnyeke anasema uharibifu wa mazingira umekuwa ukifanywa na wachimbaji hao,hali ambayo inatishia uhai wa kuendelea kuwepo kwa hifadhi hiyo.

A

Hii ndiyo hali halisi ya uharibifu wa mazingira unaoendelea kufanyika ndani ya hifadhi ya Moyowosi wilayani Biharamulo Mkoani Kagera.

“Mpaka sasa hatujafanya tathmini  sahihi ili kubaini kiwango cha uharibifu,lakini ukitizama tu kwa macho ni zaidi ya hekta 100 za hifadhi zimeharibiwa kutokana na shughuli za uchimbaji zinazofanyika ndani ya hifadhi…..’’ anasema Mnyeke.

Uchimbaji huo wa madini unafanywa na wachimbaji wadogo ndani ya hifadhi hiyo  katika eneo ambalo mgodi wa wa Tulawaka inayomilikiwa na kampuni ya Barrick ilitaka kuanzisha mgodi mwingine ambalo ilifanya utafiti na kuanza zoezi la uchimbaji kabla ya kuzuiwa na serikali kuendelea na zoezi la uchimbaji katika eneo hilo.

Hata hivyo askari polisi waliowekwa katika eneo hilo kwa ajili ya kulilinda ili lisivamiwe na wachimbaji hao,ndio wanaodaiwa kuwa chanzo kikuu cha uharibifu huo wa mazingira kwa kuwaruhusu wachimbaji kuingia na kuchimba madini baada ya kuwalipa ujira wa fedha.

Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa makala haya katika eneo hilo umebaini kuwa hadi kufikia mwishoni mwa Mwezi Desemba mwaka jana,zaidi ya Ekari 20 za miti ilikuwa imeteketezwa katika hifadhi hiyo kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini.

Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini ambao wamekuwa wakiingia katika hifadhi hiyo na kufanya shughuli za uchimbaji,wamekiri kuharibu hifadhi ya mazingira katika eneo hilo kutokana na ukataji wa miti wakati wa kuchimba dhahabu.

John Petro anasema kwenye hifadhi kuna dhahabu nyingi,kuna mambo mawili wanayokabiliana nayo,kwanza ni wingi wa miti iliyopo kwa sababu ni hifadhi ambayo wanalazimika kuikata na kupata nafasi ili tuweze kuchimba dhahabu.

“Lakini pili ni kukamatwa,tumekuwa tukifukuzwa na wakati mwingine kukamatwa na Askari wanyamapori ambao wanahusika na ulinzi wa hifadhi…’’ anasema  Petro ambaye ni mchimbaji wa dhahabu kutoka katika kijiji cha Runzewe.

Anasema wamekuwa wakiingia katika hifadhi hiyo kwa kujifichaficha,kwa sababu wamekuwa wakiwindwa na Askari Polisi walioko katika operesheni maalum ya kuulinda mgodi wa Tulawaka,ambao wamekuwa wakiwatoza fedha kabla ya kuwaruhusu kuingia katika hifadhi hiyo na kuchimba dhahabu.

Mchimbaji Mabula Nanji anasema Karibu njia zote za kuingia kwenye hifadhi ambapo kuna dhahabu zinapita kando ya mahali wanapoishi askari polisi wanaolinda Mgodi wa Tulawaka,kwa hiyo wakati mwingine wamekuwa wakiweka kizuizi na kuwatoza fedha kiasi cha kuanzia shilingi 20,000 hadi 100,000 kwa wachimbaji wadogo ambao wanakuwa wamebeba ‘Kiroba’ (mfuko wenye ujazi wa kilo 50)

C

Hii ni mifuko yenye mawe ya dhahabu maarufu kwa jina la Viroba baada ya kuchimbwa na wachimbaji wadogo ndani ya hifadhi ya Moyowosi.

Akifafanua Nanji anasema kwa siku wamekuwa wakiingia zaidi ya wachimbaji 400 kwenye hifadhi hiyo ambapo wakati mwingine askari hao wamekuwa wakiingia katika maeneo yenye mashimo na kuhakikisha kwamba wanamchangisha kila mchimbaji anayeingia ndani na kuwasimamia wakati wa kuchimba wakiwa na Bunduki mkononi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mavota Paschal Joakim anakiri kuwepo kwa wimbi kubwa la wachimbaji wadogo wanaoingia kwenye eneo la hifadhi kwa ajili ya uchimbaji wa dhahabu kwa vile hawana maeneo kwa ajili ya shughuli zao za uchimbaji.

Anasema kutokana na kuzuiwa kuingia kwenye hifadhi hiyo wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali ilimradi wafanikiwe kuingia na kuchimba dhahabu,na kwamba baadhi ya askari wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakitumia mwanya huo kuwatoza fedha kwa madai kuwa wanalinda eneo hilo.

“Ninachofahamu mimi ni kwamba hawa askari wapo kwa ajili ya kuulinda mgodi wa Tulawaka,na si kwa ajili ya kuulinda msitu wa hifadhi,hiyo kazi mara zote tumekuwa tukiona ikifanywa na Askari wanyamapori,wanaotoka Biharamulo…’’ anasema Mwenyekiti huyo.

Anasema taarifa ambazo amekuwa akizipata kutoka kwa baadhi ya wananchi.Askari wamekuwa wakiwaruhusu wachimbaji wanaotoa fedha na kuwazuia wale wanaoshindwa kutoa pesa,jambo ambalo anadai ni kinyume kwa sababu askari hawako kwa ajili ya kuilinda hifadhi.

Hata hivyo anasema wachimbaji wengi wanaotoa fedha nyingi kwa ajili ya kuchimba dhahbu ndani ya hifadhi hiyo wengi wao wanatoka nje ya kijiji hicho,ambapo baadhi yao wamekuwa wakija na kufanya mazungumzo na askari hao kabla ya kuingia na kutoa fedha kisha kuwatafuta vijana katika kijiji hicho na kuwaajiri kwa ajili ya kuchimba dhahabu usiku kucha na kuwalipa ujira wa fedha taslimu ama mifuko ya mawe.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wengi wanatokea huko Geita,Kahama,Bukombe na maeneo mengine,na kwamba hao wakifika kwenye eneo hilo wanatoa fedha kwa askari hadi shilingi milioni moja,na baada ya hapo wanachukuwa vijana wa kijijini hapo na kuwapa kazi ya kuchimba dhahabu kwenye mashimo ambayo wao wanajua kwamba yana dhahabu nyingi.

Uchunguzi umebaini kuwa kuna wachimbaji ambao wamekuwa wakitoa kati ya shilingi 50,000 hadi 200,000 kwa askari hao ili kuingia katika hifadhi hiyo,huku wengine wanaoaminika kwamba ni wachimbaji wa kati wamekuwa wakitoa kati ya shilingi 500,000-1,000,000 kwa askari na kuruhusiwa kuingia ndani ya hifadhi na kuchimba dhahabu.

“Hizo fedha unazosema wanatoa ni kweli, binafsi mimi siwezi kuingilia jambo hilo kwa sababu hao ni wafanyabiashara wanaweza hata kukuua wakigundua kwamba wewe unawawekea vizingiti katika kazi yao….’’ Anasema Mwenyekiti.

B

Hapa miti ikiwa imeangushwa na wachimbaji wadogo wakati wakifanya zoezi la uchimbaji wa madini ya dhahabu ndani ya msitu wa hifadhi wa Moyowosi wilayani Biharamulo.

Hata hivyo katika hali ya kushangaza askari wa operesheni kutoka idara ya misitu wanapoingia katika eno hilo la hifadhi kwa lengo la kuwaondoa wachimbaji,askari polisi wenye silaha ambao wamekuwa wakiwaingiza wachimbaji na kuwasimamia wakati wa uchimbaji,wamekuwa wakitimua mbio na silaha zao begani kuwakimbia Askari wanyamapori.

Desemba 7 mwaka jana, nilishuhudia askari wakitimua mbio katikati ya kundi la wachimbaji wadogo, baada ya Askari wa wanyapori wanaojihusisha na ulinzi wa msitu huo kuingia katika eneo hilo,huku wakiwa wameficha Bunduki zao.

Mkuu wa Operesheni ya kulinda hifadhi hiyo kutoka idara ya misitu wilaya ya Biharamulo Stewart Mtondwa, anasema shughuli za uchimbaji wa dhahabu ndani ya hifadhi hiyo,umesababisha uharibifu mkubwa wa msitu huo kutokana na miti mingi kukatwa ovyo wakati wa zoezi la uchimbaji.

Anasema pamoja na kwamba wamekuwa wakifanya ulinzi kwenye hifadhi hiyo lakini pindi wanapoondoka wachimbaji huvamia eneo lenye dhahabu na kuanza kuchimba.

Hata hivyo Mtondwa anasema chanzo cha wachimbaji kuanza kuingia katika eneo hilo na kuanza kuchimba dhahabu hali iliyosababisha uharibifu wa Msitu,ni baada ya mgodi wa Tulawaka kuingia katika hifadhi hiyo na kuanza kuchimba dhahabu kabla ya kuzuiwa na serikali.

Anasema eneo hilo liko umbali wa kilomita 4 kutoka ilipo Kinu cha kusaga mawe ya dhahabu,ambapo walikuwa wakichimba mawe na kuyasafirisha hadi kwenye kinu hicho.

Uongozi wa Mgodi wa Tulawaka kupitia kwa msemaji wake Nectar Foya,unasema una leseni maalumu ya uchimbaji, yaani Special Mining License (SML) namba 157/2003 ambayo inajumuisha eneo la sasa la shughuli za uchimbaji zinazoendelea, mtambo wa dhahabu (process plant), karakana na maeneo ya kuishi wafanyakazi ndani ya mgodi.

Pia leseni hiyo maalumu inajumuisha maeneo ya Mojamoja na West Zone, ambayo yako takriban kilomita 4 magharibi mwa mtambo wa dhahabu.

“Wachimbaji haramu wa dhahabu wako kwenye eneo hilo na mara kwa mara wamekuwa wakijaribu kuingia kwenye eneo la Mojamoja na West Zone ambayo yako ndani ya eneo la leseni yetu…’’ anasema Foya.

Anafafanua kuwa wafanyakazi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (Tanzania Forest Service – TFS), ambao wanafanya doria kwenye hifadhi ya msitu, wamekuwa wakifanya jitihada za kuwaondoa wachimbaji hao kwenye eneo hilo.

Anabainisha kuwa Mgodi wa Tulawaka haufanyi shughuli zozote za uchimbaji madini nje ya eneo la leseni yake maalumu ya uchimbaji,Eneo hilo siyo sehemu ya shughuli za sasa za uchimbaji dhahabu za Tulawaka,na kwamba Jeshi la Polisi la nchini pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ndiyo wanaofanya doria kwenye eneo hilo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *