Asanteni madaktari – mmetuonesha haja ya kutawaliwa ipasavyo!

Jamii Africa

Nimesoma na kurudia mara kadhaa taarifa ya chama cha madaktari kuhusu kusitisha mgomo na niseme kwamba nimeipenda upeo na heshima yangu kwa madaktari wetu imezidi mara elfu zaidi. Yeyote aliyesoma taarifa hiyo anaweza kuiona kuwa ni taarifa ya kutokusalimu amri (non-surrender) bali ni kauli ya kamikaze kukataa kuchukuliwa mateka. Uamuzi wa madaktari kusitisha mgomo kufuatia agizo la mahakama kuu kuwataka warudi kazini ni uamuzi ambao unahitaji kukubaliwa na kupongezwa na wale wote ambao walisimama na madaktari toka mwanzo wa mgomo huu. Binafsi na kutoka moyoni kabisa nasema madaktari wetu asanteni na heshima yangu kwenu imeinuliwa juu zaidi sasa kuliko wakati wowote ule mwingine!

Kukataa kutawaliwa kibabe
Mgogoro huu ulianza kwa sababu kuna watu waliamini kuwa wanaweza kutawala wenzao kibabe bila kujali matokeo ya kutawala huko kwao. Mmetuonesha kuwa mtu kuwa Waziri au Katibu Mkuu kiongozi siyo kibali cha kufanya lolote, kwa yeyote na popote bila kuulizwa. Mmetuonesha kuwa ni jukumu la wananchi kuwahoji viongozi wao na wasiporidhishwa nao kuwapinga. Mmefanya kitu kipya katika Tanzania kufanywa na watu wasio wanasiasa – kukataa kuburuzwa na viongozi wa kisiasa! Mmeonesha kukataa ubabe wa utawala uliolewa madaraka. Kwa hili, mtakuwa mmewapa moyo watu wengine vile vile kutokubali kunyanyaswa, kupuuzwa, kudhehekiwa na kuburuzwa na wanasiasa! Salute!

Mmeonesha mabadiliko yana gharama – wakati mwingine kubwa sana
Mojawapo ya matokeo ya huu mgomo ni gharama yake. Kwa kweli hakuna mtu yeyote aliyejua kuwa mgomo wa madaktari unayekuja ambaye hakujua au kukadiria uwezekano wa matokeo yake hasa katika maisha ya wagonjwa na hisia za wananchi. Madaktari wanapoachwa kugoma – iwe kwa saa moja, siku moja, wiki moja au kwa mwezi mmoja kuna gharama. Na wanapofikia madaktari kugoma kwa zaidi ya siku moja ni ishara tu kuwa wanasiasa wameshindwa kutatua matatizo yao; wanapogomwa kwa zaidi ya wiki moja manake ni kushindwa kabisa na kuporomoka kwa uongozi wa kisiasa!

Madaktari hawatakiwa kuachwa kugoma; Pale tu tishio la mgomo lilipotolewa ilitakiwa uongozi wote wa taifa letu kulipa jambo hili uzito mkubwa sana kuliko ilivyofanywa mwanzoni. Wengi tunakumbuka kuwa mgomo huu ulipoanza kikao cha Bunge kilikuwa nacho kinaanza Dodoma na tunakumbuka jinsi bunge lilivyosuasua hata kujadili hili huku wakililia posho zao! Rais alitolea kauli suala la posho lakini hakutolewa kauli suala la mgomo wa madaktari! Rais alitoa pouwa kwa wafiwa mbalimbali lakini siyo wale walioathirika na mgomo! Mwezi mmoja baadaye ndiyo Rais ametolea taarifa tena vuguvugu.

Matatizo yote yaliyowakuta wananchi na hasa wagonjwa – ikiwemo vifo – yametokana na jambo moja tu! Siyo madaktari kugoma – bali madaktari kuachwa wagome kwa masaa, siku na wiki! Hivi kweli tumeacha madaktari wagome na tulitarajia wagonjwa wapone?

Kuogopa kushinikizwa na wananchi kumeligharimu taifa
Tatizo kubwa ambalo nimelionesha huko nyuma ni hofu ya kijinga kuwa viongozi wakiondolewa kwa mashinikizo basi wengine nao wataondolewa kwa mashinikizo. Tujiulize kama wananchi hawawezi na hawapaswi kuishinikiza serikali yao nani anapaswa kufanya hivyo? Kama wananchi hawawezi kuwakataa viongozi wabovu nani awakatae? Kama wananchi hawawezi kushinikiza mamlaka zilizo juu yao kuwasikiliza nani aje kufanya hivyo? Wawekezaji? Mabalozi? Nchi za Kimagharibi?

Wananchi wanayo haki ya msingi (inherent right) ya kuishinikiza serikali yao na viongozi wao; viongozi hili waliogope lakini wasiinyang’anye haki hii. Madaktari walitumia mbinu mbalimbali za kutatua tatizo hili wakapuuzwa na wakaamua kuweka shinikizo la mgomo; serikali ilitakiwa iitikie mara moja badala ya Rais kuondoka na kuonekana kutokujali kabisa kinachotokea nchini.

Waziri Mkuu amebebeshwa mzigo asiouweza
Kati ya vitu vya ajabu sana ni kuwa watu walitarajia PInda atatue tatizo la mawaziri. Wengi inaonekana hawajui kuwa mawaziri hawateulizi na Waziri Mkuu na Waziri Mkuu wa Tanzania hawawezi kumfukuza Waziri yeyote kwani siyo anayeunda baraza la mawaziri. Waziri Mkuu hana uwezo wa kumuwajibisha Mponda au Nkya! Kikatiba Waziri Mkuu wetu ni dhaifu sana mbele ya Rais kwani yeye naye anafanya kazi kwa ridhaa ya Rais. Japo anapitishwa na Bunge, Bunge haliwezi kumzuia rais kumuondoa!

Kwa vile mgogoro ulihusu mawaziri ni Rais peke yake – aliyewateua na ambaye wanatumika kwa ridhaa yake – alipaswa kuingilia kati siyo Waziri Mkuu. Waziri Mkuu alikuwa na uwezo tu wa kufikisha ujumbe wa Rais lakini hakuwa na bado hana uwezo wa kufanya lolote kwa waziri yeyote nchini. Inaonekana watu wengi wamesahau sakata la Richmond. Waziri wa NIshati na Madini wa wakati ule walilalamikiwa kuhusiana na mkataba wa Richmond; Waziri Mkuu aliingilia kati lakini hakuwa na uwezo wa kumzuia Waziri yeyote kufanya lolote kwa sababu hana uwezo huo. Waziri Mkuu alifanya yale yaliyondani ya uwezo wake lakini kuwawajibisha mawaziri si mojawapo hili alimuachia Rais.

Ndio maana naamini kuwa Pinda inampasa kujiuzulu kumsaidia Rais kuunda baraza jingine. Kama Waziri Mkuu wakati wa kashfaa ya Richmond alivyojiuzulu na kumpa nafasi rais kuunda baraza jingine ninaamini PInda baada ya kuoneshwa kuwa ni dhaifu mara tatu kwenye sakata hili amepoteza credibility ya kuonesha uongozi. Njia pekee – akitaka kuwa na heshima – ni kujiuzulu ili kumpa Rais nafasi ya kujipanga upya. Kwa vile Rais anasuasua katika kufanyia mabadiliko baraza Waziri Mkuu akijiuzulu baraza nalo linavunjika – japo hakuliunda yeye!

Madaktari wamerudi nyuma bila kusalimu amri (retreat withour surrendering)
Walichosema madaktari ni muhimu sana kwa Rais na viongozi wetu wa kisiasa kukifikiria. Je wanaweza kumlazimisha Daktari kurudi kazini bila kuhatarisha maisha ya wagonjwa? Je daktari kurudi kazini katika mazingira yale yale yaliyosababisha mgomo inamsaidia nani hasa? Je daktari kuonekana hospitalini anapima pima na kutembea temba au kuzungumza na wagonjwa hata kama hana dawa, vifaa n.k inasaidia nini? Kama kweli leo kuna hospitali ambazo X rays hazifanyi kazi na zipo zisizo na CT Scans kweli daktari anaporudi hapo tunaweza kusema amerudi kufanya kazi au kuonekana kazini?

Msimamo wao juu ya Nkya na Mponda unatuma ujumbe mzito

Hata hivyo madaktari wametuma ujumbe mzito sana kwa wote wale ambao wanafikiria kuwa wameumaliza mgomo – kwamba mawaziri hao ni tatizo kwa sekta ya afya. Madaktari wanasema hivyo kwani wamewaona wakifanya nao kazi kwa mwaka uliopita, wamezungumza nao mara nyingi na wanawajua uwezo wao. Madaktari wanasema hawa ni tatizo – ni jukumu la rais kuendelea nao au kutokujali maneno ya wataalamu hawa. Kuendelea kuwa nao kwa sababu ya kuogopa shinikizo ni kuhatarisha zaidi sekta ya afya kuliko kuwaondoa.

“Wakati madai yetu yakishughulikiwa (na Rais) tunapenda kusema kuwa hatuna imani na Waziri wa Afya Mhe. Dr. Haji Mponda na (naibu) Mhe. Lucy Nkya na kuwa tunamsimamisha rasmi uanachama wa MAT Mhe. Dr. Lucy Nkya” wamesema madaktari katika tamko lao na kuongeza “madaktari tunatamka kuwa Waziri wa Afya Dr. Haji Mponda na Naibu wake Dr. Lucy Nkya ni maadui wa madaktari na wa sekta ya afya kwa ujumla hapa nchini na tunaahidi kutowapa ushirikiano wowote wa kibinafsi au wakiutendaji”. Kama ujumbe huu wa mwisho haujafungua masikio ya watawala wetu basi hakuna ujumbe mwingine unaoweza kufunguliwa.

Asanteni madaktari
Madaktari asanteni kwa kuliamsha taifa na kutukumbusha kuwa kuna gharama katika kuleta mabadiliko. Gharama ya majina, hadhi, na sifa zetu; kuna gharama ya nafsi zetu na kwa kweli kabisa kuna gharama kwa watu wengine vile vile. Mmetuonesha kile tulichokiona sehemu nyingine duniani – mabadiliko yana gharama kubwa – kuna watu watapoteza kazi, wapo watakaochukizwa na wapo wengine watapoteza hata maisha yao. Niliandika wiki iliyopita kuhusu Steve Biko na kuonesha kuwa alilipia gharama kubwa ya uhai wake kwa kuwaamsha vijana wa Afrika ya Kusini! Mmefanikiwa katika kilichoshindikana – kuiambia serikali haiwezi kutawala kwa mabavu na dharau!

Ni matumaini yangu watawala wetu wamejifunza jambo kidogo katika hili – wawe na haraka ya kutatua matatizo badala ya kutafuta namna ya kulindana na kubebana na kutetea vitumbua vyao. Kwa sababi, kama madaktari wameitikisa kidogo serikali hivi, itakuwaje endapo mgomo mkubwa zaidi utakuja kufanyika? Kuna mistari imechorwa na sasa imeanza kuvukwa. Wasiwalazimishe na wengine kuvuka kwani wasipoangalia nchi kweli kabisa itaishi kutoka mgomo na kashfa hadi mgomo na kashfa nyingine na hivyo kuzidi kujidhoofisha.

Walioathirika wapewe pole kweli
Wapo walioathirika sana na mgomo huu na kwa kweli kila Mtanzania kwa namna moja au nyingine ameathirika. Wapo ambao tumesupport mgomo huu tukijua kabisa kuwa ndugu zetu wanatakiwa kwenda hospitali huko huko na wengine wamepoteza jamaa zao wakati wa mgomo huu. Kama nilivyosema mwanzoni madaktari hawakutakiwa waachwe wagome, na kwa vile ni wanasiasa ndio waliowaacha madaktari wagome ni wao wanasiasa wanabeba lawama zote za madhara ya mgomo huu kwani kama wameweza kuuzimisha kwa kikao cha masaa machache Ikulu wangeweza kufanya hivyo Januari! Hawakufanya na matokeo yake ni haya yaliyotokea.

Kikwete akubali kuwajibika kwa yote yaliyotokea
Kama nilivyosema juzi, namna pekee ya kuanza kwa usahihini kwa Rais kukubali kubeba lawama za mgomo huu wote kuanzia mwanzo hadi hivi sasa. Kama Rais alipaswa kuingilia kati mara moja na ugoigoi wa kufanya hivyo ndio umefikisha hapa tulipofika. Hawezi kukwepa lawama na hana mwingine anaweza kushare naye lawama hizo. Na tunarajia kuwa atawawajibisha hawa viongozi na wakati huo huo kupanga mkakati wa nguvu wa kuboresha sekta ya afya.

Kwa kukubali kusitisha mgomo baadaya kukutana na Rais madaktari wametuonesha nani anastahili kuwajibika. Natumaini naye amejitambua hivyo.

MMM-BGM

5 Comments
  • Safi sana ila bado haitoshi ~ Nchini Sweden Waziri mmoja aligundulika kukwepa kulipia ada ya Kingamuzi inayorusha matangazo ya Televisheni na ilipobainika ni kweli aliachia ngazi mara moja, Ni vigumu kuaminini mdaa wote huu bado Mponda na Naibu wake bado wapo wanangangania nyadhifa wasizo stahili, ni vigumu kuamini bado Wz. Hussein Mwinyi bado yupo baada ya Mabomu ya Mbagala na Gongo la Mboto, wapo wengi……. muendelee kuwa elimisha wanainchi wasirudie haya makosa 2015

  • kwa kweli watanzania tumechoka kufanyiwa mambo ya ajabu,hivi hii nchi inaongozwa na viongozi kweli?wanaoelewa maana ya uongozi?la hasha!hakuna,nahisi kama tupo kwenye filamu za akina kanumba na wenzake,kifupi hatuna viongozi na tumekwisha.

  • Nasimama kutetea madaktari kwasababu najua misingi ya mgomo wao. Kwaupande mwingine, nachelea kuwalaumu wanaotakiwa kujiuzulu kwasababu binafsi najua busara za Mheshimiwa waziri Hadji Mponda (NB: kimsingi sipo kumtetea). Nalazimika kuamini kuwa sura tunayoiona kwa hawa mawaziri si yao bali imebandikwa. Wametwishwa zigo la mavi wanuke wao lakini mapungufu yao si kwakiasi hicho (Hii ni imani yangu).
    Pili; sura ya mgomo wa madaktari na madai yao kimsingi imepotoshwa au haijaeleweka kwa umma m kubwa wa kitanzania. Najua madaktari siwanasiasa lakini kama kuna uwezekano, waufafanue kwawaandishi wa habari ili wananchi wauelewe kuwa nikwamaslahi ya umma na sio maslahi ya madaktari tu kama inavyoeleweka kwasasa.

  • Natamani watanzania waelewe hali iliyopo ktk hospitali za serkali, jinsi mazingira yalivyo magumu ya kutoa huduma, nilifanya kazi ktk hospitali ya Mwananyamala miaka miwili iliyopita, ilifika kipindi hata karatasi za kuandikia dawa, maelezo ya ugonjwa wa mgonjwa hakuna, ivi watanzania wanaelewa kuwa kuna baadhi ya ambulance ambazo zinabeba wagonjwa na kuwapa rufaa kwa sababu ya ukosefu wa vitendea kazi? nimeona wagonjwa wanapewa rufaa kwa kukosekana nyuzi za kushonea, au gauze za kufunga baada ya operation, wanaopewa rufaa kwa ati umeme umekatika ni wengi sanaaaaaaa, gloves hakuna, haya ni mazingira ya kutoa huduma kweliiiiiiiiiiiii, tuamke kwa kweli, kazi ya kutibu ni kazi niliyoitamani toka utoto wangu lakini baada ya kufanya serikalini, moyo wangu uliniuma sana kwa kuwa siwezi kutekeleza majukumu yangu ipasavyo. Mungu isaiddie na ibariki Tanzania yetu

  • Mimi nadhani wakati umefika si watumishi bali wananchi wote tufike mahali pakusema inatosha.Mwalimu anatumwa kwenda Mtwara kutoka chuo cha Ualimu Bunda kutathimini mwalimu mwanafunzi anapewa posho ya Tshs.200,000/= akihoji anaambiwa atachukuliwa hatua ajieleze kwa maandishi kwa unyonge anakubali kufanya kazi katika mazingira magumu lakini swali je hawa watunga sera wanafanyiwa hayo?kwa sababu ni juzi nilisikia waziri sijui kaibiwa sijui kapoteza US$4000/= na shilingi zingine za kitanzania nina imani labda zilikuwa posho na kama zilikuwa posho mbona wao hawakopwi sisi hatutaki $ kama wao basi watupatie stahili zetu ili watu wafanyekazi kwa uadilifu.Daktari anapangiwa kazi Mwanyamala huu ni mfano hapewi nyumba na wakati huo hana mshahara anahifadhiwa na ndugu yake Kibaha hivi hiyo nauli ya kuja Mwananyamala na kwa wakati ataipata wapi na wakati huo hajanza hata kulipwa katika mazingira haya ufanisi utatoka wapi?
    Madaktari hoja yao ya nyumba na vitendea kazi ni ya muhimu wala haina siasa ndani yake.Watawala wamekuwa kila jambo wanajitetea kwa kusema siasa.Ni lini tutangalia hoja kama ilivyo na tukaacha kujitetea kwa kusema hii ni siasa.Halafu tunatafuta makada wa kisiasa nakuja kwenye vyombo vya habari kuwatetea wanasiasa.Na wengine wakaanza kuwaogofya madaktari kwa kutumia jina la Mungu eti wamwogope Mungu.Mimi kwa elimu ndogo ya dini niliyonayo nakumbuka Waisraeli walikuwa wakimlaumu hata Mungu na Mungu alikuwa akiwasikiliza sasa kama huyo Mungu anasikiliza ni kwa nini hawa viongozi wetu wasiwasikilize wanaowatawala eti Katiba inawalinda wasiulizwe.Viongozi wako tayari wananchi wengi wakoswe huduma lakini waziri hawezi kuachia nafasi yake ya uwaziri sasa hao wananchi wakifa watamwongoza nani?
    Hawa viongozi wajifunze kutoka kwa Thabo Mbeki Rais wa pili wa Afrika ya Kusini niliwahi kusikia kuwa aliachia nafasi fulani ya uongozi sikumbuki ni kwa nini?Cha muhimu hakuangalia Maslahi yake aliweka UMMA mbele lakini sisi UMMA nyuma maslahi yangu binafsi mbele mimi KIONGOZI na RAFIKI zangu hao watawaliwa juu yao.WATANZANIA TUTAFAKARI NA TUSHIRIKIANE PAMOJA TUTASHINDA na watawla watfikia mahali waheshimu waliowaweka madarakani

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *