Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeeleza kuwa asilimia 74 ya watoto nchini Tanzania wanaishi katika umasikini, jambo linalowafanya kukosa haki na mahitaji muhimu ya kijamii kustawisha maisha yao.
Kwa mujibu wa ripoti ya NBS kwa kushirikiana na Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) walifanya utafiti kuhusu ustawi wa watoto nchini Tanzania tangu mwaka 2012/2013 ambapo wamebaini kuwa umasikini wa kaya umechangia kwa sehemu kubwa watoto kukosa haki zao za msingi zinazowafanya waishi.
“Tanzania kama ilivyo kwa maeneo mengine duniani, haki nyingi za watoto hazitekelezwi. Haki hizo zinajumuisha chakula na maji, huduma muhimu kama afya na elimu; kwa kiasi kikubwa watoto hawapati haki hizo kwasababu wanaishi katika familia masikini ambazo hazina kipato cha kutosha kukidhi mahitaji na huduma”, imeeleza sehemu ya ripoti hiyo ambayo ilitolewa 2016
Ripoti hiyo inaeleza kuwa umasikini na kukosa haki kwa watoto kunajitokeza katika sura mbalimbali kulingana na umri wa watoto na maeneo wanakoishi ikiwa na maana mjini na vijijini.
“Kwa ujumla kiwango cha kukosa haki na umasikini kwa watoto kiko juu. Asilimia 74 ya watoto wote nchini Tanzania wanaishi katika umasikini wa viwango mbalimbali huku asilimia 29 wanaishi katika familia zilizo chini ya mstari wa umasikini na kiwango cha umasikini ni kikubwa kwa watoto walio na umri wa miaka 5-13 na 14-17”.
ASILIMIA YA WATOTO WANAISHI KWENYE UMASIKINI WA KIPATO NA AMBAO HAWAPATI CHAKULA CHA UHAKIKA
Watoto wanaoishi kwenye umaskini wa kipato watoto wasiopata chakula cha uhakika
Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu
NBS na UNICEF walikusanya taarifa muhimu kutoka familia 5,010 ikijumuisha familia 3,947 zenye watoto ambapo waliwapanga watoto hao katika makundi 4 kulingana na umri (mwezi 0-23, miezi 24-59, miaka 5-13, miaka 14-17). Pia walitazama vigezo 8 muhimu ambavyo ni lishe, afya, ulinzi, elimu, habari, usafi, maji na makazi.
Inaeleza kuwa, “Mfano mtoto mmoja anaweza kuwa anapata mlo kamili lakini hajaandikishwa kwenda shuleni, mwingine anaweza kuwa aapata huduma nzuri za usafi na maji akiwa nyumbani lakini anahitaji ulinzi. Kutengeneza sera na programu za kutatua mambo haya, ni muhimu kuelewa kwanza mtoto yuko kwenye kiwango gani cha umasikini na kunyimwa haki zake”.
Watoto wanaoishi vijijini ndio wameathirika sana kwa kukosa mahitaji muhimu yalivyotajwa hapo juu huku wale waishio mjini wana hali ya kuridhisha . Asilimia 81 ya watoto wa vijijini hawapati mahitaji 3 au zaidi, huku asilimia 33 wanaishi katika umasikini ukilinganisha na maeneo ya mjini ambako asilimia 40 hawapati mahitaji 3 au zaidi na 10% wanaishi kwenye umasikini wa kipato.
Kwa kutumia kigezo cha makazi, watoto wa mjini wanakosa haki ya kuishi sehemu salama ambapo huchochewa zaidi na idadi kubwa ya watu na makazi duni. Zaidi, watoto wengi wenye umri mkubwa (miaka 5-17) katika maeneo ya mjini na vijijini hawapati lishe bora hasa chakula cha asubuhi.
Suluhisho la kudumu
Ongezeko la kipato linaweza kupunguza mahangaiko kwa watoto wanaoishi katika familia masikini na kwa sehemu katika familia zenye uwezo. UNICEF inashauri kuwa miradi ya kukuza kipato katika kaya masikini ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ikaongezewa fedha ili kuwafikia wananchi wengi katika meneo ya vijijini kuokoa maisha ya watoto ambao hawapati haki za msingi za kuishi.
Pia wazazi waongezewe elimu ya makuzi ya watoto ili kuhakikisha wanapata huduma muhimu za afya, maji, elimu, makazi na ulinzi tangu wakiwa wadogo. Elimu hii itawawezesha wazazi kuwa na maarifa sahihi ya jinsi ya kuwalea na kuwakuza watoto katika malezi mazuri.
Kulingana na lengo la 1 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya mwaka 2030 yanalenga kupunguza nusu ya kiwango cha umasikini kwa wanaume, wanawake na watoto wa umri wote kwa kutumia jitihada mbalimbali za kitaifa na kimataifa.