Miaka 56 ya Uhuru: Babu Seya, mwanaye waachiwa huru, Rais atoa msamaha kwa wafungwa wengine 8,157

Jamii Africa
Rais Magufuli ameamua kuwasamehe Familia ya Nguza Viking(Babu Seya) na Johnson Nguza(Papii Kocha) kuanzia leo. - Rais pia ametoa msamaha kwa wafungwa 8,157 ambapo 1,828 wataachiwa huru na 6,329 watapunguziwa muda wao wa kukaa gerezani - Pia awasamehe wafungwa 61 waliohukumiwa kunyongwa; wahusika wafanye process za kuwatoa leo au kesho

Rais John Magufuli ametoa msamaha na kuagiza kuachiwa huru kwa familia ya Nguza Viking maarufu ‘Babu Seya’ na mwanaye Johnson Nguza ambao walihukumiwa kifungo cha maisha kwa makosa ya ubakaji.

Babu Seya ambaye ni Msaani nguri wa mziki wa dansi nchini na mwanaye Johnson Nguza (Papii Kocha) walihukumiwa kifungo cha maisha gerezeni kwa kosa la kubaka na kulawiti watoto 10 mwaka 2003, ambapo Juni 25, 2004 walianza kutumikia kifungo chao. Kwa nyakati tofauti wamejaribu kutumia njia za kisheria kujinasua katika hukumu hiyo lakini hawakufanikiwa, hadi hivi leo walivyopata msamaha wa rais.

Akizungumza leo katika sherehe za miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara zilizofanyika Makao Makuu ya nchi mjini Dodoma, rais Magufuli amesema msamaha huo umetolewa kwa wafungwa wengine 8,157 ambao walikuwa wamefungwa katika magereza mbalimbali nchini na amefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa wafungwa hao wamejirekebisha na wanastahili kurudi uraiani kujenga taifa.

“Kutokana na ibara hiyo hiyo ya 45 nimeamua kumsamehe familia ya Nguza Viking jina lingine anaitwa babu Seya na ndugu Johnson Nguza hivyo nao waachiwe huru kuanzia leo”, amesema rais Magufuli.

Baada ya rais kumtaja Babu Seya ulisikika mlipuko wa shangwe na furaha kutoka kwa wananchi na kuibua hisia tofauti katika uwanja wa Jamhuri ambako sherehe zilikuwa zinafanyika.

Msamaha huo wa rais alioutoa kwa wafungwa 8, 157 unahusisha wafungwa 1,828 ambao wataachiliwa huru kuanzia leo na wengine 6,326 wamepunguziwa muda wao wa kukaa gerezani kulingana na vifungo vyao.

Msamaha huo umetumia Ibara ya 45 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inampa rais mamlaka ya kutoa msamaha na kufuta au kumpunguzia adhabu mtu yeyote aliyehukumiwa na mahakama kwa makosa mbalimbali.

Amebainisha kuwa idadi kubwa ya wafungwa waliopo magerezani ni wanaume na amewataka kujitathmini kutokana na mienendo yao ya uharifu inayowafikisha mikononi mwa vyombo vya sheria.

“Nataka niwaeleze ndugu zangu, Tanzania tuna wafungwa 39,000 mpaka jana kati ya wafungwa hao wanaume ni 37,000, wanawake ni 2000, kwa hiyo katika kufungwa hakuna usawa. Lakini wafungwa waliohukumiwa kunyongwa ni 522, wafungwa waliohukumiwa maisha wako jumla 666 kati yao wanaume wako 651 na wanawake ni 11. Wanaume tuanze kujitambua kwanini hali iko hivi”,

“Wapo wafungwa ambao wametubu kweli dhambi zao, wamekiri makosa yao  kweli kweli. Baada ya kukaa nakufikiria na hasa kwasababu binadamu wote huwa tunaomba kusamehewa”, amesema rais.    

Hata hivyo, rais ametoa angalizo katika msamaha huo kuwa hautahusisha wafungwa waliohukumiwa kwa makosa ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino).

Baada ya rais kutoa agizo hilo, Babu Seya na Papii Kocha wameachiwa na kutoka gerezani Ukonga, jijini Dar es Salaam na kulakiwa na familia na mashabiki wao.

Babu Seya (wa pili kulia) akiwa na mtoto wake Papii Kocha (wa pili kushoto) wakati wa kesi yao

 

Kwa upande wake, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kupitia idara ya Habari na Mawasiliano kimempongeza rais Magufuli kwa ujasiri aliouonyesha wa kumwachia huru Babu Seya na kutaja hatua hiyo ni kutimiza ahadi ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Edward Lowassa ambaye aliitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Lowassa aliwaahidi watanzania kuwa endapo angechaguliwa kuwa rais wa Tanzania angemtoa msanii huyo kwasababu mazingira ya kesi yake yalikuwa na utata.

 

Sherehe kufanyika Dodoma

 Wakati huo huo rais ametanga rasmi kuwa kuanzia sasa sherehe za Uhuru zitakuwa zinafanyika mkoa wa Dodoma ambao ni Makao Makuu ya nchi ambapo maamuzi hayo yanaenda sambamba na kuhamishia shughuli za serikali katika mkoa huo ili kutimiza ndoto ya muda mrefu ya kuuboresha mji wa Dodoma.  Awali sherehe hizo zilikuwa zikifanyika katika uwanja wa uhuru jijini Dar es Salaam.

“Sherehe za uhuru wa Tanzania Bara mwaka huu zinafanyika hapa Dodoma ndio Makao Makuu ya nchi na zitaendelea kufanyika hapa na si mahali pengine”, amesema rais.

Awakumbuka walinzi wa amani waliouwawa Congo DRC

Watanzania wametakiwa kuwaombea wanajeshi  44 wa Tanzania walinzi wa amani ambao walijeruliwa katika mashambulizi na waasi wa Kivu nchini Congo DRC. Katika shambulio hilo wanajeshi 14 wamefariki, 8 wako mahututi na wawili hawajulikani waliko.

 Wito huo ameutoa rais Magufuli katika sherehe za Uhuru ikiwa ni ishara ya kuonyesha mshikamano kwa wanajeshi waliopo Congo kuhakikisha nchi hiyo inarejea katika utawala wa kidemokrasia ikizingatiwa kuwa imekuwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu sasa.

Rais John Magufuli akiwa kwenye gari la wazi wakati akiingia katika viwanja vya Jamhuri mjini Dodoma katika sherehe za miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara

 

Mafanikio yaliyopatikana

Mafanikio mbalimbali yamepatikana tangu Tanzania Bara ipate uhuru wake 1961 katika sekta mbalimbali ingawa bado ziko changamoto zinazokwamisha kufikia maendeleo ya kweli.

 Akielezea mafanikio yaliyopatikana rais Magufuli amesema, “ Nchi yetu imepiga hatua kubwa za maendeleo tangu kupata uhuru”,

“Wakati tunapata uhuru baada ya miaka 76 ya kikoloni nchi yetu ilikuwa na mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 33,600 kati ya hizo kilomita 1,360 tu ndizo zilikuwa za lami. Leo mtandao wa barabara tunao una kilometa 122,500 aidha 12,679.55 ni za lami.

Madaraja ambayo yaliyokwisha kamilika tangu tupate uhuru ni zaidi ya 17. Ukiachia mbali ujenzi wa barabara wakati tunapata uhuru, nchi yetu ilikuwa ina vituo vya kutolea huduma za afya 1,095 leo tuna vituo vya kutolea afya zikiwemo hospitali zaidi ya 7,293.

Wakati tunapata uhuru tulikuwa na shule za msingi 3,100 hivi sasa zipo shule 17,379. Shule za sekondari zilikuwa 41 hivi sasa ziko 4,817, na tulikuwa na chuo kikuu 1 lakini sasa vipo 48. Madaktari waliosajiliwa walikuwa 403 ambapo kati yao watanganyika walikuwa 12 tu leo tuna madaktari waliosajiri 9,343.

Mwaka 1961 wahandisi wazalendo walikuwa 2 tu lakini hadi kufikia mwezi uliopita 2017 nchi yetu imefikisha wahandisi 19,164 waliosajiliwa. Makandarasi walikuwa 2 tu leo tuna makandarasi 9,350.

Hali kadharika, wakati tunapata uhuru wastani wa umri wa mtu kuishi ilikuwa miaka 37 leo hii wastani ni miaka 61”.

 

Historia ya Uhuru wa Tanganyika

Tanganyika ambayo sasa inaitwa Tanzania Bara ilipata uhuru wake 9 Disemba 2017 na kuhitimisha utawala wa kikoloni uliodumu miaka 76. Ikijumuisha  miaka 33 ya utawala wa Kijerumani na miaka 43 ya utawala wa Uingereza .

Harakati za kutafuta uhuru wa nchi yetu ziliongozwa na chama cha Tanganyika National African Union (TANU) ambacho kiliongozwa na Mwalimu Julius Nyerere ambaye kwa kushirikiana na wahasisi wengine wa taifa hili walifanikisha kukombolewa kwa Jamhuri ya Tanganyika mwaka 1961.

TANU kwa kushirikiana na Chama cha Afro Shiraz Party (ASP) , mwaka 1964 walifanikiwa kuuangusha utawala wa Kisultani ambao ulikuwa unaongoza visiwa vya Zanzibar. Mwezi April 1964 Tanganyika na Zanzibar zikaungana na kuunda nchi ya Tanzania yenye serikali mbili yaani ili ya Muungano na Zanzibar.

Mnamo 1977 TANU na ASP viliungana na kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kinatawala mpaka sasa chini ya rais wake, John Magufuli.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *