Imeelezwa kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa watanzania kukosa huduma bora za afya kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kutokana na kupunguzwa kwa bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa asilimia 20.
Hayo yamebainika leo bungeni mjini Dodoma wakati waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 ambapo amesema wameomba Serikali iwapatie billion 893.4 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo.
“Mhe. Mwenyekiti jumla ya fedha kuu ambayo ninaomba Bunge lako tukufu lipitishe katika mafungu yote mawili kwa mwaka 2018/2019 sh. Bilioni 893.4,” amesema Waziri Ummy.
Kiasi hicho cha fedha kilichoombwa kimepungua kutoka trilioni 1.1 za mwaka wa fedha wa 2017/2018 ambapo zimepungua bilioni 171.6 na kufikia bilioni 893.4 mwaka 2018/2019 sawa na asilimia 20.
Waziri Ummy amesema kati ya fedha hizo ambazo wizara yake inaomba, fedha zitakazoelekezwa kwenye matumizi ya miradi ya maendeleo zitakuwa Tsh. bilioni 561.75 sawa na asilimia zaidi 60 ya fedha zote, ambapo matumizi ya kawaida yatagharimu bilioni 304. 47.
“Kwa upande wa matumizi ya kawaida kwa mwaka 2018/2019 wizara ikadiria kutumia kiasi cha sh. Bilioni 304,473,476 (bilioni 304.47) kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo sh. Bilioni 88,465,756 (bilioni 88.46) zitatumika kwajili ya matumizi mengineyo na sh. Bilioni 216,720,000 (bilioni 216.72) zitatumika kwajili ya mishahara ya watumishi,” amesema waziri Ummy na kuongeza kuwa,
“Kwa upande wa miradi ya maendeleo wizara inakadiria kutumia sh. bilioni 4.91 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, sh. Bilioni 1.5 ni fedha za ndani na sh. Bilioni 3.41 ni fedha za nje.” amesema waziri Ummy.
Kwa muktadha huo, bajeti ya afya itategemea fedha za wahisani kwa asilimia 60 kugharimia miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, ukarabati wa majengo na ununuzi wa vifaa tiba na dawa. Hata fedha bilioni 4.91 iliyoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo bado ni ndogo.
Changamoto iliyopo ni kwamba fedha za wahisani wakati mwingine huchelewa kufika au zinaweza zisiingie kabisa nchini kutoka na masharti ambayo yanaweza kuathiri utolewaji wa huduma za afya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba amesema serikali haina nia ya dhati ya kuinua sekta ya afya kwasababu bajeti inayotengwa kila mwaka ni ndogo na haikidhi mahitaji ya wizara ya afya.
“Uchambuzi wa kamati umebaini fedha zilizotengwa kwaajili ya utekelezaji wa shughuli wizara kwa mwaka wa fedha 2017/18, ni kiasi kidogo ambacho hakiridhishi na kinyume na matarajio ya Mpango wa Bajeti ambao Bunge na Serikali tulikubaliana,” alisema Serukamba.
Licha ya bajeti ya afya kupungua kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 kwa asilimia 20, fedha za bajeti iliyopita ya 2017/2018 hazikufika zote kwenye wizara hiyo jambo lilikwamishwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya sekta hiyo.
Serukamba amesema, mpaka kufikia Februari mwaka huu, Serikali ilikuwa imetoa Sh. bilioni 576.52 pekee kati ya Sh. trilioni 1.1 zilizokuwa zimetengwa kwaajili ya Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2017/18,.
Kutokana na bajeti ndogo ya wizara ya afya, wabunge wameshauriwa kuijadili na kuangalia uwezekano wa kuishawishi Serikali kuongeza fedha kwa wizara hiyo ikizingatiwa ni sekta muhimu kwa ustawi wa wananchi ili kuwahakikishia wananchi afya bora.