Daniel Samson
Afya bora ni sehemu muhimu ya kumuwezesha mwanadamu kutekeleza majukumu ya uzalishaji mali. Lakini ufinyu wa bajeti inayotengwa na serikali katika sekta ya afya huwa changamoto kwa wananchi kupata huduma bora za afya.
Katika Sera ya Afya ya mwaka 2007, Tanzania imeahidi kulinda na kuboresha afya za watanzania kwa kuimarisha mifumo ya utoaji huduma katika vituo vya afya na hospitali zilizopo mijini na vijijini. Serikali inatekeleza Sera na mikakati mbalimbali ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, Malengo ya Maendeleo Endelevu na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA) ambayo inajumuisha afya kama suala la msingi.
Licha ya serikali kuwa na mikakati mizuri ya kuboresha sekta afya, bado juhudu hizo zinakwamishwa na ufinyu wa bajeti inayotengwa kila mwaka kugharamia matumizi ya sekta hiyo. Hali hiyo huathiri mwenendo wa utoaji huduma za afya na kuhatarisha maisha ya watu.
Serikali imeendelea kutafuta wahisani wa nje na ndani ambao watasaidia kukamilisha upungu wa bajeti unaojitokeza. Kutokana na wahisani kujali afya za binadamu wameanzisha miradi mbalimbali ikiwemo kujenga hospitali za kisasa, kutoa elimu ya afya na misaada ya kiutu na fedha.
Changamoto inayojitokeza hapa ni kuwa misaada ya wahisani huja na masharti mbalimbali ambayo yasipotekelezwa na serikali huzuia au kuchelewesha fedha zinazotakiwa kupelekwa katika maeneo husika kuokoa maisha ya watu.
Takwimu kutoka Ripoti ya Matumizi ya Umma (PER) ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (2012) inaonyesha kuwa utegemezi wa sekta ya afya kutoka kwa wahisani umepungua katika miaka ya karibuni lakini si kwa kiwango cha kuridhisha.
Katika mwaka wa bajeti 2006/2007 sekta ya afya ilitenga asilimia 71 ya fedha za ndani na 29% ilitegemea kutoka nchi wahisani. Licha ya serikali kutoiweka sekta ya afya kama kipaumbele chake lakini iliimarisha mfumo wa sekta hiyo kwa kutenga bajeti kubwa.
Katika miaka ya bajeti iliyofuatia utegemezi wa wahisani ulianza kuongezeka taratibu ambapo ilipofika 2010/2011 matumizi ya ndani yalifikia asilimia 53 na karibu nusu ya bajeti iliyopangwa katika sekta hiyo ilitegemea wahisani kwa 47%.
Serikali ilijidhatiti katika mwaka uliofuata wa 2011/2012 ambapo ilitumia pato lake la ndani kugharamia sekta ya afya kwa asilimia 59 na kusubiri misaada ya mataifa ya nje iliyofikia 41% ya bajeti yote ya afya iliyopangwa kwa mwaka husika.
Mwongozo wa Asasi za Kiraia juu ya Ushawishi wa Bajeti ya Afya katika Serikali ya Tanzania (2015), unaeleza kuwa, “Serikali pia inaonyesha kujizatiti kwake katika afya kwa kupanga fedha za umma kwenye shughuli zinazohusu afya. Ingawa mipango ya kufadhili afya ya jamii iliongezeka mara mbili kati ya mwaka 2006 na 2012, ni asilimia 10% tu ya bajeti ya serikali ilipangwa kwa ajili ya afya, asilimia 15 chini ya ilivyopangwa kwenye Azimio la Abuja”.
Azimio la Abuja juu ya Sekta ya Afya (2001) aya ya 26 linasema, “TUNAAHIDI kuchukua hatua zote muhimu kuhakikisha kwamba rasilimali zinazohitajika zinapatikana kutoka vyanzo vyote na kwamba zinatumika ipasavyo na kwa ufanisi. Aidha, TUNAAHIDI kuweka lengo la kupanga angalau asilimia 15% ya bajeti yetu ya mwaka kwa ajili ya kuboresha sekta ya afya.
Licha ya makubaliano hayo ya Abuja, bado bajeti ya afya inayotengwa haizidi 15% ya bajeti yote ya serikali. Hali hiyo huzolotesha juhudi za uzalishaji mali katika nchi kwasababu ya gharama kubwa za afya ambazo wananchi hawazimudu.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Sera na Miradi ya Afya (2016) inaeleza kuwa Mgawanyo wa bajeti kuu ya serikali katika mwaka wa fedha wa 2015/2016, majeti ya afya iliongezeka kwa 11.3% ikilinganishwa na mwaka uliotangulia ambapo ilikuwa 9.1%.
Ukuaji huo wa bajeti ya afya ulitegemea zaidi ufadhili kutoka nje. Asilimia 11.3 za bajeti ya afya ya Tanzania ni kubwa ikilinganishwa na bajeti ambayo inatengwa na nchi zenye kipato kidogo ambayo ni 5.3% lakini kiko chini ya Azimio la Abuja (15%).
Wakati huu ambao serikali inatekeleza mipango yake ya uchumi wa viwanda, inahitaji rasilimali watu ambao wana afya bora na uwezo mkubwa wa kufikiri ili kuvumbua teknolojia itakayoendesha uchumi wa nchi. Jambo hilo haliwezekani isipokuwa kwa sekta ya afya ikitazamwa upya na kuwekeza fedha za kutosha kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini.
Serikali inawajibika katika mipango yake na kuwafanya wafanyakazi wa serikali wanaowajibika kwenye ugawaji wa rasilimali na matumizi yake wanazingatia mambo ya msingi yanayogusa maisha ya wananchi ikiwemo afya.