Licha ya uchumi wa Tanzania kuimarika na kuchangia kukua kwa pato la ndani la Afrika, Tanzania imetakiwa kuboresha miundombinu ya barabara ili kuwavutia wawekezaji kuwekeza katika sekta za uzalishaji na biashara.
Kulingana na takwimu kutoka Benki ya Dunia, Tanzania ni miongoni mwa nchi tano za Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi, ambapo hadi kufikia 2015 uchumi wake ilikuwa umekua kwa zaidi ya asilimia 5.4. Kulingana na takwimu za serikali uchumi umeimarika na kukua kwa asilimia 6.8 kwa mwaka 2017
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Masuala ya Uchumi wa Benki ya Dunia katika nchi za Afrika, Dkt. Albert Zeufack, wakati wa mjadala uliondaliwa na Benki ya Dunia Tanzania kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kujadili Mchango wa Tanzania katika ukuaji wa bara la Afrika, ambapo amesema nchi za Afrika ikiwemo Tanzania zinakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya uhakika kwenye usafirishaji.
Mtandao wa barabara katika nchi za Afrika bado haujaunganisha maeneo muhimu ya uzalishaji licha ya nchi hizo kuwa na rasilimali nyingi ambazo hazijatumika. Afrika ina jukumu la kuimarisha mfumo wa usafirishaji ili wawekezaji wajitokeze kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Afrika ambao unakuwa kwa kiwango kizuri.
“Uchumi wa Afrika umekuwa kwa asilimia 2.4 mwaka 2017 na unatarajiwa kukua kwa 3.2% mwaka 2018. Ukuaji wa Afrika unaakisi kuimarika kwa hali ya uchumi wakati wakitekeleza mikakati ya kutatua changamoto za kutokuwepo kwa usawa wa kiuchumi katika nchi zao”, amesema Dkt. Zeufack
Ameeleza kuwa wawekezaji binafsi kutoka katika nchi zilizoendelea wana mitaji na teknolojia ambayo wanatafuta nchi yenye mazingira mazuri ya kufanyia biashara na miundombinu ya usafirishaji wa malighafi na bidhaa za viwandani.
Ameishauri Tanzania kuweka kipaumbele katika miradi ya barabara ambayo ina manufaa kwa nchi, kuunda vyombo vya usimamizi wa miundombinu ambavyo vitahusika na manunuzi na kufanya utafiti wa maeneo muhimu ambayo yanatakiwa kuunganishwa na mtandao wa barabara ili kuwawezesha wawekezaji binafsi kuziendeleza rasilimali za nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Malawi, Somalia na Burundi, Bella Bird amesema Benki hiyo itaendelea kutoa misaada na mikopo yenye masharti nafuu kwa serikali ya Tanzania ili kuiwezesha kutekeleza miradi ya maendeleo inayolenga kukuza pato la ndani na kuiwezesha Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda.
Amesema wanaisaidia serikali katika miradi ya usimamizi wa maji na uunganishaji wa umeme vijini ili kuwawezesha wananchi kupata nishati itakayowasaidia katika uzalishaji wa viwanda vidogo vidogo na kuchangia katika kukua kwa uchumi.
Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya REPOA, Prof. Samuel Wangwe amesema serikali inapaswa kuwa na mipango endelevu ya kuimarisha mfumo wa ndani wa uwekezaji ambao utazingatia hali halisi ya uchumi wa nchi kabla haijaingia katika utekelezaji wa sera ya viwanda.
“Kwanza kuhakikisha tunatekeleza mipango ya kiuchumi, tunaweka mazingira mazuri kuvutia sekta binafsi kuwekeza nchini na kuwa na tafsiri sahihi ya maendeleo”, amesema Prof. Wangwe.
Hata hivyo, katika mjadala huo wazungumzaji walijikita zaidi kuelezea umuhimu wa kuwekeza katika elimu na tafiti zinazolenga kuibua uvumbuzi na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika sekta za kiuchumi na biashara. Pia kuwawezesha vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa kupata maarifa sahihi.
Mikakati ya Serikali kuelekea Uchumi wa Viwanda
Serikali imeendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ya reli, bandari na barabara ikiwa ni pamoja na kuaanda mazingira mazuri kwa wawekezaji kufanya biashara nchini na kuinua sekta ya viwanda.
Katika sekta ya usafiri wa anga, serikali imeendelea na upanuzi wa uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Dar es salaam na viwanja vingine nchini ili kuziwezesha ndege kubwa kutua nchini. Pia imenunua dege mbili aina ya Bombardier na mwakani ndege mbili kubwa zitawasili nchini.
Pia serikali inatarajia kujenga reli ya kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ambayo itagharimu zaidi ya bilioni 400. Ikikamilika pia itaunganishwa mpaka mkoa wa Mwanza.
Mradi mkubwa wa upanuzi wa bandari unaojulikana kama ‘Dar es Salaam Marine Gateway Project (DMDP)’ ambao unalenga kuifanya bandari hiyo kuwa na hadhi ya kimataifa na kuwezesha kupokea meli kubwa na kuhifadhi mizigo mingi.
Mradi huo wa DMGP umefadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) ambayo ni mshirika wa karibu wa EU ambapo Tanzania imepokea Dola za Kimarekani milioni 345 kukamilisha mradi huo ambapo utaongeza uwezo wa kupokea mizigo kwa tani milioni 25 miaka saba ijayo. Pia utapunguza muda wa kusubiri kutoka saa 80 hadi 30.
Ili kuinua viwanda, Umoja wa Ulaya (EU) imetoa msaada wa bilioni 130 kwa ajili ya miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Nishati ya umeme ni muhimu hususani katika maeneo ya vijijini kwa kuwa inachangia uboreshaji wa huduma za jamii kama shule, vituo vya afya, hospitali, viwanda vidogo vidogo na kilimo.
Mjadala huo ulioandaliwa na Benki ya Dunia ikishirikiana na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) ulikuwa na kauli mbiu “Kukua kwa Bara la Afrika: Kuwekeza katika Ujuzi na Miundombinu ya Uwekezaji”, ambapo uliwakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo kujadili nafasi ya Tanzania katika kukua kwa uchumi wa Afrika hasa katika sekta ya usafirishaji na miundombinu ya barabara .