‘Birthday’ zatumika kukeketa wasichana mkoani Mara

Gordon Kalulunga

Baada ya serikali kuonekana kuzuia na kukataza mila ya baadhi ya makabila hapa nchini kuwakeketa wasichana, mkoani Mara baadhi ya makabila yanayokeketa yamebuni mbinu mpya, imebainika.

Mbinu inayotumika kwa sasa kuwakekata wasichana hao ni kuandaa sherehe inayofanana na siku ya kuzaliwa(Birthday).

Baadhi ya wananchi na viongzi wa afya na viongozi wa vitongoji wilayani Musoma na Bunda mkoani Mara walioomba hifadhi ya majina yao walisema kuwa kwasasa ukeketaji unafanyika kwa wasichana baada ya shule kufunga.

Walisema mbinu inayotumika ili kukwepa mkono wa sheria kwa wakeketaji ni kuwakusanya mabinti wachache au mmoja mmoja na kuwakeketa huku wakiimba nyimbo za kumpongeza binti kwa kuazimisha siku yake ya kuzaliwa.

‘’Mbinu inayotumika ili kufanikisha ukeketaji na kukwepa mkono wa sheria na kukamata wazazi wa binti na mangariba hao hupanga mbinu nzito na baada ya kuwakeketa wasichana hao huimba nyimbo happybirthday to you’’ walisema kwa nyakati tofauti.

Baadhi ya wasichana wanaoishi wilayani Musoma waliosema kuwa wao tayari wamekeketwa, walisema kuwa hawaoni ubaya wa kitendo hicho kwasababu ndiyo mila na desturi za makabila yao.

‘’Ni kawaida tu mbona hata wanaume wanaenda jando! Tatizo labda ni kwamba ninapotaka kukutana kimwili na mtu asiye wa kabila la kwetu huwa naona aibu kidogo maana hata nikienda nae mimi nachelewa kufika kileleni wakati yeye anawahi na hisia zangu zinakuwa mbali’’ alisema ‘’Judith’’ jina siyo halisi.

Dhana hiyo ya kukeketa baadhi ya makabila yanaamini kuwa kukeketa kutalinda ubikira wa wasichana na kuwafanya wanawake wasiwe wahuni (Malaya).

Baadhi wanasema kuwa hali hiyo inaongeza raha ya kujamiiana kwa waume zao, na kitendo hiki kinaaminika kuongeza uwezekano wa wanawake kuolewa na kuimarisha uwezo wa kuzaa.

Madhara yanatajwa na wataalam wa afya kuwa ni msichana akikatwa via vya uzazi kunaweza kusababisha kutoka damu nyingi. Hii inaweza kusababisha kifo au upungufu mkubwa wa damu.

Pia mambukizi ya magonjwa inaelezwa kuwa yanaweza kutokea kwasababu ya kutumia vifaa vichafu na pia yanaweza kutokea kwa kutumia dawa za kienyeji za kuponyesha vidonda.

Maambukizi yanaweza yakaenea hadi kwenye tumbo la uzazi, mirija ya kupitishia mayai, na kwenye mayai ya uzazi na kusababisha maumivu ya mara kwa mara hata ugumba. Mambukizi ya magonjwa yanaweza kusababisha kifo.

Hata baada ya vidonda kupona mwanamke aliyeshonwa uke, tundu linaweza likawa dogo mno kuweza kutoa mkojo.

Wasichana waliohojiwa walisema kuwa baada ya kukeketwa wanaweza kubana mkojo kwa masaa au siku kwa sababu ya maumivu au kwa kuogopa kupitisha mkojo kwenye vidonda.

Sanjari na hayo, tafiti kutoka kwenye mitandao mbalimbali zinasema kuwa kama mlango wa uke ni mdogo sana kiasi cha kutoruhusu damu ya hedhi kutoka vizuri, damu inaweza kukusanyika ndani ya uke na tumbo la uzazi.

Hii inaweza kusababisha maambukizi ya magonjwa, na tumbo la uzazi kuvimba kwa sababu ya damu ya hedhi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *