Bunda: Watoto ‘njiti’ hatarini kupoteza maisha kwa kukosa umeme!

Mariam Mkumbaru

Watoto wanaozaliwa chini ya miezi tisa (Njiti) wapo hatarini kupoteza maisha kwa sababu ya kukosa joto la uhakika katika hospitali teule ya Bunda.

Tatizo la kukosekana kwa joto katika chumba maalumu cha kuwapatia joto kwenye hospitali hiyo linasababishwa na kukatika kwa umeme mara kwa mara na kuwepo kwa mita ya luku katika hospitalini hiyo.

Revocatus Kato ni Muuguzi Mkuu katika hospitali teule ya Bunda alisema kuwa, kuna hatari ya kuwakosa watoto wanaozaliwa chini ya miezi tisa kwa sababu ya kutokuwa na umeme wa uhakika hapa hospitali.

"Kuna chumba maalumu cha kuongeza joto ambacho ndio kinatumika kiwakuza watoto njiti, chumba hico kinatumia kifaa maalumu cha kutoa hewa ya joto ili watoto njiti  waweze kukua vema, lakini umeme ndio changamoto kwa sababu tumefungiwa mita ya luku na TANESCO ambayo umeme wake muda mwengine unaisha saa tano usiku hospitali na kuwa kiza na chumba hicho cha njiti kinashindwa kutoa joto kwa kukosa umeme," alisema Kato

Kato alisema kuwa hospitali ina jenereta lakini matumizi ya jenereta ni ghalama kubwa sana kulitumia kipindi umeme wa luku unapoisha usiku aua kukatika, kwa siku unaweza kutumia lita 70 hadi lita 100 ya disel na lita moja inauzwa sh. 2,130 hadi 2,150 kwa siku unatakiwa kuwa na pesa zaidi ya sh.2,15000 za kununua mafuta ya kutumia katika jenereta pindi umeme unapokatika au luku ikiwa imekwisha usiku wa manane.

"Tunaiomba TANESCO kutubadilishia mita hii ya luku na kutufungia mita ya kawaida kwa sababu inachangia vifo kwa watoto njiti na wajawazito akiwa katika chumba cha upasuaji halafu luku imekwisha au umeme unakatika ghafla kuna uwezekano mkubwa wa mgonjwa huyo kupoteza maisha,"alisema Kato.

Kwa upande wake Muuguzi wa wodi ya wajawazito na vichanga hospitali hapo Peter Sungwa alisema kuwa, watoto wanaozaliwa chini ya miezi tisa ni wengi sana katika wilaya ya Bunda na wengine wanatoka katika wilaya ya Musoma Vijijini na seregeti wote wanahitaji kuhifadhiwa katika chumba hicho ili kupata joto na kukua vema.

Mwaka jana zaidi ya watoto  32 njiti wazaliwa na mwaka huu mpaka kufikia mwezi wa March zaidi ya watoto 12 njiti wamezaliwa katika hospitali hii.

mtoto-njiti

Sungwa alisema kuwa sio tuu tatizo la umeme bali kuna tatizo la uhaba wa maji katika hospitali hii, kila mgonjwa anayelazwa lazima aje na ndoo ya maji ya kuoga na kufua nguo kila siku.

"Maji nayo ni tatizo sugu katika hospitali ya Bunda tunaiomba wizara husika kutuangalia kwa jicho la huruma katika suala la upatikanaji wa maji ili iwe rahisi kuendesha shughuli mbalimbali za matibabu zinazotegemea maji,"alisema Sungwa.

Rainer Kapinga ni Mganga Mkuu wa wilaya ya Bunda alikili kuwepo kwa changamoto ya umeme na maji katika hospitali teule ya Bunda, changamoto ambayo inachangia kuzorotesha utoaji wa huduma kwa wakazi wa wilaya ya hiyo na nje ya wilaya.

"Kwa sasa tunajipanga kuandika barua kwa Tanesco kuwaomba watuondolee mita ya luku na kutuwekea mita ya kawaida ili shughuli za upasuaji na mambo mengine ya matibabu yanayo hitaji huduma ya umeme yafanyike kwa wepesi," alisema Kapinga

Wilaya ya Bunda ina wakazi wasiopungua 3,75,000 wote wanategemea kupatiwa huduma katika hospitali hiyo ambayo inatatizo la upatikanaji wa umeme na maji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *