Nimepokea kwa masikitiko makubwa, kutokuamini na mshtuko taarifa za msiba wa Mhe. Regia Mtema. Kifo chake kimekuja wakati ambapo moto wa mabadiliko nchini umekuwa ukipamba kwa kasi zaidi na nyota yake ikizidi kuangaza kila kukicha. Regia alikuwa ni mmoja wa vijana ambao wametupa matumaini kuwa kuna vitu vinawezekana nchini na vinaweza kufanywa na vijana.
Msimamo wake, uthabiti wake na kujiamini vilikuwa ni tunu ambazo zilimsimamisha bila woga kutetea kila alichoamini. Kwa baadhi yetu ambao tumepata nafasi ya kuzungumza naye nje ya mitandao hii na wale ambao tumemjua kwa muda mrefu kabla ya kuibuka na kuwa mwanasiasa tunaweza kusema kuwa Regia alikuwa ni mwanasiasa aliyesukumwa sana na moto wa mabadiliko. Moto ambao alitamani kuwa sehemu yake katika kuona cheche zake zinawafikia wengi zaidi.
Alitamani kuiona Tanzania ikiwa bora zaidi na ambayo watu wake wanafurahia matunda ya nchi yao kwa haki, usawa na umoja. Tunaposema alikuwa ni mwanaharakati hatutii chumvi. Wengi tumeshuhudia jinsi ambavyo amekuwa ni miongoni mwa wanasiasa ambao wamekomazwa kwenye mitandao hii. Amekuwa jasiri kuliko wanasiasa wengi wakongwe kuja na kupitishwa kwenye tanuru la maoni ya JF na kila wakati ambapo ulifikiria kuwa labda amekwazika na hatorudi tena Regia alirudi na alirudi akiwa mpya kabisa. Aliweza kusimama katika moto bila kuungua na kama aliungua haikuwa rahisi kujua!
Kwa upande wangu, Regia alikuwa ni mshiriki mkubwa wa mambo mengi ambayo nimeyafanya na yeye ameyafanya. Aliponiomba wakati wa kampeni ya 2010 kumsaidia kupitia Ilani yake kwa Wana Kilombero niliona ni heshima ya pekee. Mapema mwaka huu tulikuwa tumeanza kuzungumzia baadhi ya mambo ambayo tungeweza kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na wengine katika Bunge lijalo. Bahati mbaya mbingu imebadili mipango hiyo. Ninaamini hata hivyo huko aliko anatutie shime ya kuendelea kutekeleza mipango mbalimbali.
Regia alikuwa mchangamfu, mcheshi, mwenye kupenda utani, na kwa hakika kabisa alikuwa makini. Kitu kimoja ni kuwa hakuogopa kusema alichokuwa anafikiria au kilichomgusa moyoni. Alisema hisia zake na na mawazo yake pasi ya kutaka kuonesha kumwogopa mtu au kumpendelea mtu. Aliamini katika kutetea msimamo wake na akishawishiwa kuona mapungufu hakuchelewa kujirudi. Kwa kweli haikuwa rahisi kuzungumza naye bila kujikuta unatabasamu. Alikuwa amejaliwa kipaji cha kujenga urafiki na watu wengi na hata kuwa kwake Mbunge hakukuwa kwake kiuzizi cha kuwa karibu na marafiki zake. Hakujiona ni “kigogo” wa aina fulani aliyependa kutukuzwa au kuogopwa. Alijiona yeye ni mwanasiasa na kweli alikuwa hivyo. Lakini alikuwa ni zaidi ya mwanasiasa – alikuwa ni binti wa Kitanzania aliyejaliwa vipaji vingi na mwenye njozi nyingi kwa nchi yake!
Rambirambi zangu nyingi – na labda nawasemea wengine vile vile – ziwaendee familia yake ya Mzee Estelatus Mtema pamoja na tena kwa namna ya pekee kwa pacha wake Remija Mtema. Remija kuliko mtu mwingine yeyote duniani amepoteza sehemu yake na mzigo huu ni mkubwa kupita kiasi. Wakati kwa wengi wetu tumepoteza rafiki, mwanaharakati, mwanasiasa na mshirika wa mabadiliko kwa ndugu zetu hawa wamepoteza binti, dada, shangazi na ndugu yao wa karibu. Ni msiba mkubwa kwao. Nawaombea faraja wote hawa na wale wote ambao wameguswa na msiba huu mkubwa.
Mungu ailaze roho ya Marehemu Regia pema peponi na atujalie sisi wengine dhamira na kiu ya kuendeleza na kusimamia kile ambacho dada yetu alikisimamia na kukipigania. Namna sahihi ya kuenzi maisha ya Regia ni kuendelea kuipigania Tanzania na Watanzania bila kujali jambo jingine lolote linalowatofautisha kama mtu mmoja mmoja.
Hata kama nyota imezimika, mwanga tulioushuhudia unatupa matumaini kuwa zipo siku njema mbeleni!
Mpaka Tuonane tena Paradiso!
Mzee Mwanakijiji
Maneno yake haya ya mwisho ni ya kugusa moyo:
Naomba nichukue fursa hii pia kuwashukuru wanaJF wote kwa support yenu kwangu kwa hakika ninawashukuru sana tena sana. JF imekuwa ni nyumbani, JF imekuwa ni darasa, Vile vile JF imekuwa ni Tanuru la Moto maana wakati mwingine huwa ninaingizwa kwenye moto hasa. Na mwisho nichukue fursa hii kuwaomba radhi wale wote niliowakwaza kwa namna moja ama nyingine, tuanze upya mwaka ujao.. With Love Regia
nitakukumbuka sana dada regia, nakuombea kwa mungu akupumzishe kwa amani. ni wanawake wachache sana wenye moyo kama wako.
kwaheri dada regia
bwana ametoa bwana ametwaa jina lake lihimidiwe amin