CAG aibua madudu ya serikali. Akerwa na matumizi mabaya ya fedha za maendeleo

Jamii Africa

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad  amewataka wabunge kuihoji serikali kwa kushindwa kutekeleza bajeti ya mwaka 2017/2018 licha ya ukusanyaji wa mapato kuongezeka.

Akizungumza na wanahabari mjini Dodoma leo wakati wa uwasilishaji wa ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2017, Prof. Assad ameshangazwa na serikali kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wakati ikizingatiwa kuwa imekuwa ikijinasibu kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato hasa ya kodi.

Inaelezwa kuwa serikali katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 ilifanikiwa kukusanya mapato kwa asilimia 94.2 ya malengo iliyojiwekea lakini utEkelezaji wa bajeti haukisi fedha zilizotumika, jambo linaloibua maswali mengi juu matumizi mabaya ya fedha za umma yasiyozingatia sheria na taratibu za kibunge.

Kwa kutambua hilo, Prof. Assad  amewaomba wabunge waingilie kati suala hilo kwasababu mapato na matumizi yote ya serikali yanaidhinishwa na bunge, iweje bajeti haijatekelezwa kama inavyotakiwa.

“Serikali ilikusanya fedha kwa asilimia 94.2, sasa inakuwaje bajeti haijatekelezwa? Wabunge wanapaswa kuhoji hili kwa sababu makusanyo yalipaswa kuakisi utekelezaji wa miradi”, amesema Prof. Assad.

Ameongeza kuwa jambo lingine ambalo linatia mashaka ambalo linaweza kuwa na harufu ya ufisadi ni kutopelekwa kwa fedha za miradi ya maendeleo katika halmashauri mbalimbali nchini licha ya bunge kuidhinisha fedha hizo.

“Serikali za mitaa hazikupelekewa fedha za maendeleo kwa asilimia kubwa. Zaidi ya Sh. Bilioni 320 hazikupelekwa ikiwa ni zaidi ya nusu ya bajeti ya maendeleo ya serikali za mitaa”, amesema Prof. Assad.

Ikumbukwe kuwa  Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) siku ya jana ilitangaza  kukusanya trilioni 11.78 kwa kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, ikilinganishwa na 2016/17 ambapo ilikusanya trilioni 10.86. Takwimu hizo zinabainisha ongezeko la makusanyo kwa 8.46%.

Rais John Magufuli alipoingia madarakani alifanya mabadiko makubwa kwenye sekta ya umma ya fedha ambapo taasisi zote za serikali zilitakiwa kufunga akaunti zao kwenye benki binafsi na kuingizwa kwenye mfumo wa serikali kuu ambapo makusanyo yote ya kodi yanatunzwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Utaratibu huo mpya unazilazimisha serikali za mitaa kuomba fedha kutoka hazina na kutokana na mchakato mrefu uliopo umesababisha fedha kuchelewa au kutofika kabisa kwenye Halmashauri kwajili ya utelekezaji wa miradi ya maendeleo.

Baadhi wa wachambuzi wa uchumi wamesema hatua ya serikali kujitoa katika Mpango wa Uendeshaji wa shughuli za serikali kwa uwazi (OGP) inaweza kuwa sababu nyingine ya fedha nyingi za maendeleo kutojulikana zilipo ilihali zilipangiwa matumizi.

 

Miradi ambayo haikuidhinishwa na Bunge

Kwa nyakati tofauti wabunge na wananchi wamekuwa wakilalamikia tabia ya serikali kutekeleza miradi ambayo haijaidhinishwa na bunge, jambo ambalo linaleta wasiwasi katika uwazi na uwajibikaji wa matumizi ya fedha hizo ambazo taarifa zake hazionekani.

Katika kikao cha tisa cha Bunge, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche aliibua sakata la ujenzi wa uwanja wa ndege wa Chato mkoani Geita ambao unadaiwa kugharimu bilioni 39. Kwa mujibu wa Mbunge huyo alisema mradi huo haukuidhinishwa na bunge na hata serikali ilipoulizwa haikutoa majibu ya kuridhisha.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe wakati akihojiwa na Fikra Pevu hivi karibuni aliitaka Ofisi ya CAG na  Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kuchunguza fedha zilizotumika kujenga uwanja wa ndege wa Chato, ambao haujafuata taratibu za kisheria na haukupitishwa na bunge, ili wananchi wapate taarifa za uhakika na kuondoa mjadala ambao haujapatiwa majibu ya uhakika kutoka serikalini

“Si vibaya kujenga viwanja vya ndege na Chato ni Tanzania kama sehemu nyingine yoyote ya Tanzania na hatuwezi kutopenda wenzetu kupata maendeleo lakini jambo la muhimu ni namna gani ule mradi unatekelezwa haukuwa kwenye mipango ya bajeti, hapakuwa na zabuni ya wazi”, alisema Zitto.

Hata hivyo, CAG mstaafu, LodoviCk Uttoh wakati akihojiwa na kituo kimoja cha runinga nchini alisema wakati mwingine serikali inaruhusiwa kisheria kutumia fedha kabla hazijaidhinishwa na serikali lakini inapaswa kutoa taarifa kwenye kamati ya bunge ya bajeti ili iingizwe kwenye mfumo rasmi wa bajeti.

Lakini alisema suala hilo linaweza kufanyika kama kuna jambo ambalo linatakiwa kufanyika haraka pasipo kusubiri idhini ya bunge.

Serikali imeshauriwa kuwajibika na kutimiza shughuli zake kwa uwazi na kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinaelekezwa kwenye miradi iliyoidhinishwa na bunge ili kuepusha matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka, amesema “Kazi ya CAG ina lawama. Tutazipitia taarifa zote na kutoa taarifa kwa Bunge zima. CAG ametaja kila sehemu upotevu wa fedha. PAC tumejipanga kuhakikisha halitaachwa jiwe.Kipindi hiki tutatoa mapendekezo mazito zaidi”.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *