CHADEMA wamlipua Mwakyembe kwa ufisadi kama wa EPA

Jamii Africa

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeibua tuhuma nzito za ufisadi wa mabilioni ya fedha, kikidai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hasa kupitia makundi ya wasaka urais, kimeanza kutumia mbinu haramu kutafuna fedha za Watanzania kwa ajili ya kampeni za 2015, kwa namna ile ile iliyotumika kufanikisha wizi wa EPA, wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2005.

Katika mkutano na waandishi wa habari, CHADEMA kimedai kuwa ufisadi huo unasimamiwa na Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe, kikimtuhumu kuwa anatumia madaraka yake ya uwaziri ‘kuipatia’ Kampuni ya CCM iitwayo Jitegemee Trading Company zabuni ya kujenga mradi yenye thamani ya bilioni 10, kinyume cha taratibu kujenga eneo la maegesho kwenye eneo la CCM.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa CHADEMA, Singo Benson Kigaila, amesema kuwa kwa msukumo wa Mwakyembe, Mamlaka ya Bandari (TPA), imetoa zabuni kwa kampuni hiyo inayodaiwa ni ya CCM, kujenga maegesho ya magari makubwa, makontena na malori eneo la SUKITA (Tabata) jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa kwa mujibu wa nyaraka ambazo chama hicho kimezinasa, Kampuni ya Jitegemee imepewa zabuni hiyo kinyume na shera za nchi, hususan ile ya Manunuzi ya Umma (PPRA), akisisitiza kuwa hakuna zabuni yoyote iliyotangazwa ili kuruhusu ushindani wa makampuni mbalimbali yenye sifa kufanya kazi hiyo.

“Ndugu wanahabari, mchezo wanaofanya CCM, hasa kupitia magenge ya watafuta urais, ni ule ule kutumia makampuni yao, mengine yakiwa hewa, kutafuta fedha haramu kwa kuwaibia Watanzania kama walivyofanya kabla na wakati wa uchaguzi wa mwaka 2005, pale makampuni yao yalipoiba fedha Benki Kuu na kusaidia kampeni za CCM kumpeleka Kikwete ikulu.” Alisema Benson na kuongeza;

“Sasa wameanza tena…wameanza kwa kupitia kampuni yao iitway Jitegemee Trading Company. Watalipwa bilioni 10, tena tayari zimeshapangwa kwenye bajeti ijayo. Kampuni hii kwa msukumo wa Mwakyembe, imepewa zabuni ya ujenzi wa maegesho eneo la SUKITA, yaani kampuni ya CCM imepewa zabuni kinyemela, kujenga maegesho kwenye eneo la CCM…kama mnavyojua eneo hilo lililopo Tabata, ni mali ya chama hicho.

“Kuna hoja tano za msingi hapa; kwanza mradi huu unaotaka kufanywa na Mwakyembe kwa kutumia kivuli cha TPA, kampuni hiyo haijafanyiwa tathmini ya upembuzi yakinifu…sawa sawa tuna ilivyokuwa kwa Kampuni ya kitapeli ya Richmond ambayo Mwakyembe huyo huyo akisoma ripoti yake bungeni alisema ni kosa.

“Pili, mradi hu wa Mwakyembe na chama chake, haukufuata Sheria ya Manunuzi ya Umma. Hakukuwa na zabuni iliyotangazwa wala ushindani kwa makampuni mengine yenye sifa kushindana. Tatu; nyaraka zilizopo TPA zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2010 Bodi ya Bandari ilipokea maombi kutoka Manispaa ya Temeke ya kutaka kufanya ubia wa eneo la maegesho huko Kurasini

“Wazo hili halijawahi kufanyiwa kazi badala yake Mwakyembe amekuja na mradi wake. Vyanzo vyetu ndani ya serikali na CCM vinasema kuwa mmoja wa wajumbe wa TPA alipohoji  kwa nini shirika linaingiza feha hizo kwenye mradi huueneo la SUKITA, Mkurugenzi wa Bandari alijibu “huuni mradi wa chama tawala, hivyo ni muhimu tukau-support,” alisema Kigaila akinukuu kikao cha bodi ya bandari.

Aliongezea akisema kuwa jambo la jingine katika mradi huo aliouita ni ufisadi wa kuitafutia CCM fedha kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mkuu wa 2015 na ule wa serikali za mitaa mwaka ujao, ni uamuzi wa serikali kwenda kujenga mradi mkubwa kama huo eneo la Bonde la Msimbazi.

“Kila siku wanawaambia Watanzania wahame mabondeni…leo wanapeleka kujenga mradi huu eneo la bondeni ambako CCM walikuwa wakitumia kufuga ng’ombe na nguruwe na wakasombwa na mafuriko. Sasa leo wanataka magari makubwa, malori na makotena, mali za wateja ziengeshwe pale.

“Mbali na mradi huu kuitafutia CCM na genge la watu wengine wasaka urais fedha haramu kwa mgongo wa kodi za walipa kodi, mradi huu utasababisha hasara kubwa huko mbeleni, hasa pale mvua kubwa zitakapoanza kusomba mali za wateja…kumbukeni Mwakyembe yuko kwenye genge moja la urais na Samuel Sitta, Bernard Membe, anayeungwa mkono na Kikwete,” alisema Benson.

Mkurugenzi huyo wa Oganazisheni na Mafunzo wa CHADEMA alisema kuwa tangu Mwakyembe aondoe uongozi wa zamani wa Mamlaka ya Bandari, yeye na viongozi wapya, wamepuuza miradi yote ya mwanzo na badala yake wameingiza miradi mipya takriban 35, ambayo imeombewa fedha kwa nia hiyo hiyo ya kusaka fedha za urais.

Amewataka Watanzania kuzijua sura mbili za Waziri Mwakyembe, akidai kuwa si kiongozi wa kuaminika, akikumbushia namna alivyolinda maslahi ya CCM kwa kuwaficha Watanzania baadhi ya masuala katika kashfa ya Richmond na kukaa kimya pale maazimio ya bunge yaliyotokana na kamati yake, yalipopuuzwa.

Mwakyembe ndiye alifanikisha kujiuzulu kwa aliyekua Waziri Mkuu, Edward Lowassa,baada ya kuuvalia njuga mradi wa kifisadi ulopewa kampuni ya Richmond Development LLC, kwa njia ambayo sasa anautoa kwa kampuni ya Jitegemee.

Hatua hiyo ilimpa heshima kubwa Mwakyembe, jambo ambalo wadadisi wa mambo wamesema sasa ametumia heshima hiyo "kufanya atakavyo" hata kufikia hatua ya kuingia kwenye ufisadi.

====

Msomaji, nyaraka unaweza kuzisoma kupitia JamiiForums katika mada HII

1 Comment
  • Inasikitisha sana kwa mtu kama mwakyembe aliyekuwa amejizolea umaarufu Tanzania na nje ya Tanzania leo inaingia kwenye mtego wa panya sijui atamueleza nini mheshimiwa sana RICHARD MONDULI na watanzania chezea njaa za watanzania wewe(hakuna aliye msafiiiiiiiiiiiiiiiiiii-By jdeeeeeee)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *